Walimu wabomoa chungu
cha ujinga
Na Ndimara Tegambwage
SASA
unaweza kusoma Sayansi kwa Kiswahili. Kikwazo cha lugha ya kigeni kimeanza kuondolewa. Chungu cha ujinga
kimebomoka.
Walimu
na wadau wengine, wamefanikisha uchapishaji wa kitabu cha somo la Kemia kwa
Kidato cha I.
Kitabu
kinaitwa: Furahia Kemia/Enjoy Chemistry – Kwa wanaoanza kujifunza/A textbook for beginners. Kimechapwa mwaka
2011.
Fungua
kitabu. Kushoto ni Kiswahili, kulia ni Kiingereza. Kimesheheni maarifa,
maelekezo na michoro ya vifaa vya kufanyia mazoezi. Ni sayansi.
Waandishi
wanaelekeza: “Soma sentensi, kifungu cha maneno au mada nzima kwa Kiingereza.
Pale tu unapoona kwamba huelewi kila kitu ndiyo usome sentensi, kifungu cha
maneno au mada hiyo kwa Kiswahili.”
Hapa
waandishi wamejikita katika maana na uelewa. Kama
hukuelewa, au hukuelewa vizuri kile ulichosoma, basi unageukia lugha nyingine.
Inaelekezwa
mwanafunzi asome kwanza Kiingereza. Akielewa, basi aendelee. Asipoelewa, apate
msaada wa Kiswahili. Kwa msingi huo, kitabu kinafundisha Kiingereza kwa msaada
wa Kiswahili.
Furahia Kemia hakiondoi umuhimu wa
kuwa na vitabu vya kiada vya sayansi vilivyoandikwa kwa Kiswahili moja kwa moja
– lugha ya mwalimu na mwanafunzi nchini – bali ni moja ya njia za kufikia huko.
Angalia
mbele – miaka minne ya kuchapisha vitabu vingine kwa ajili ya vidato vingine na
kwa masomo mengine ya sayansi. Kutakuwa na tofauti.
Iko
wapi basi, sababu ya kutokuwa na msimamo katika matumizi ya lugha ambayo wote –
walimu na wanafunzi – watakuwa wanaelewa vizuri; huku wakijifunza lugha
nyingine zozote watakazo?
Ibrahim Kipepe wa MwanaHALISI amehoji wanafunzi jijini Dar es Salaam juu ya
kitabu hiki. Rosemary Kelvin wa sekondari ya Zanaki anasema, “Kitatusaidia sana sisi ambao
hatukutokea shule za Kiingereza.”
Janeth
Julius (Zanaki) anasema, “Wanafunzi watapata msamiati muhimu unaotokea kwenye
mitihani.”
Ramadhani
Mohamed wa sekondari ya Makoza, Tabata anasema, “Tunaosoma shule za Kata,
tutanufaika zaidi kutokana na mafundisho ya sasa kutokidhi uelewa wa masomo.”
Eric
Bayona wa sekondari ya Migombani, Segerea, “Kitabu kinaweza kuchanganya
wanafunzi ambao wataegemea kwenye Kiswahili na hatimaye mitihani ikaja kwa
Kiingereza.”
Bakari
Salum wa sekondari ya Tambaza anasema, kitabu hiki kilicho madukani sasa, “Kitaleta
ongezeko la wanaofaulu kwa vile wengi watakuwa na uelewa mpana.”
Hussein
Juma wa sekondari ya Ananasif anasema, “Unajua tumefundishwa kwa Kiswahili hadi
darasa la saba. Hatujui kusoma wala kuandika Kiingereza. Hiki kitakuwa
mkombozi.”
Naye
Justina Kakuru aliyemaliza Kidato cha IV miaka mitatu iliyopita anasema,
“Ningepata msingi kama huu, ningesoma
sayansi.”
Furahia Kemia kimechapishwa na kampuni
ya Mkuki na Nyota Publishers ya Dar es
Salaam kwa udhamini wa HakiElimu – asasi ya kijamii
nchini inayopigania uwazi, haki ya kupata elimu bora na demokrasi; na asasi
nyingine ya Faire Welt Rastatt e. V.
Hata
katika mazingira ya uchumi huria, kitabu hiki ni mkuki kwa mikonga ya kibeberu ya uchapishaji, ambamo kwa miaka
mingi, watawala wamenaswa na kukataa kuamua juu la lugha ipi itumike kuvuna elimu
na maarifa.
0713
614872
No comments
Post a Comment