Tunataka kuendelea kulinda uhuru wetu wa mawazo na uhuru wa kujieleza, kwani uhuru huo ni haki yetu. Na uhuru hauna kikomo, wala hakuna wakati tunapoweza kusema uhuru tulionao unatosha. Hapana. Kila hatua inazaa matakwa mapya ya uhuru wa binadamu.

Wednesday, July 4, 2012


Huku ndiko kuingilia mahakama

Alhamisi 28 Juni 2012, wakati nikijadili mtandaoni, hoja ya “kuingilia mahakama,” niliandika ifuatavyo; ninanukuu:

“Huwezi kwenda mahakamani kuomba nafuu; ukarudi kesho yake kukaza nguvu ya amri ya kukupa nafuu; na kesho yake ukatoka kifua mbele, kwa kutumia nafuu ileile, kuwakomalia wale uliozuia, na isivyo haki, lakini ilivyo halali kisheria. Utakuwa umetumia nguvu ya mahakama kujinufaisha binafsi na utakuwa unajigamba kana kwamba umeweka ‘mahakama mfukoni.’”

Hili ndilo limetokea. Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imekwenda mahakamani. Ikaomba nafuu. Ikapewa. Ikatoka mbele. Ikawakomalia madaktari. Ikaanza kuwashambulia. Kuwafukuza kazi kabla ya kile ilichoita “shauri kuu kusikilizwa na kumalizwa.”

Haya basi, siyo matumizi sahihi ya nafuu ya mahakama. Serikali ilikuwa na uwezo wa kufanya iliyofanya bila kutumia nguvu ya mahakama. Haikuhitaji ruhusa ya mahakama kufukuza madaktari.

Kwahiyo, serikali imeonyesha jinsi ilivyohitaji mahakama kufunga mikono, miguu na midomo ya madaktari, ili yenyewe (serikali) ipate nafuu na kuweza kuwacharaza wagomvi wao. Huku ni kuingilia mahakama.

Hapa ndipo vyombo vya habari vinajikuta vimetwishwa jukumu la kupaza sauti za wananchi na madaktari; na hata sauti ya mahakama – kupinga  matumizi mabaya ya mhimili mwingine wa dola (mahakama); tena  kwa sababu dhaifu.

Nawasilisha.

ndimara

No comments: