Header Ads

LightBlog



Dawasco, Dawasa na Darasa la waziri
·      Ahoji kutoitwa waandishi wa habari?

Na Mwandishi Maalum

JUMAMOSI iliyopita, waziri wa maji Profesa Jumanne Maghembe na naibu wake, Injinia Dk. Binilith Mahenge, waliandaa darasa “gizani.”

Kwenye kikao chao na wafanyakazi na watawala wa DAWASCO na DAWASA, jijini Dar es Salaam, mawaziri hao waligawa maswali kwa wenyeji wao.

Ni kama kusema, “…jibu maswali hayo, turudishie, halafu sisi tutatafuta jinsi ya kufanyia kazi majibu yenu.” Mmoja wa wafanyakazi aliyehudhuria kikao hicho, amekiri kuwepo mazingira hayo.

Dawasco ni Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam na Pwani; na Dawasa ni Mamlaka ya Majisafi na Majitaka.

Kampuni na Mamlaka, vyote vya umma. Vina wafanyakazi “wengi tu.” Vina mfumo wa utawala unaofanana. Vina matumizi kama kampuni nyingine nchini. Vina makazi katika jiji moja – Dar es Salaam. Vinafanya kazi moja – kazi ya maji. Rejea virefu vyake hapo juu.

Waziri na naibu wake walikuwa katika makao makuu ya Dawasco, Gerezani, Dar es Salaam. Walikwenda kukutana na wafanyakazi wa Dawasco, Dawasa na utawala.

Prof. Maghembe aliondoka mapema ili ahudhurie mkutano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwenye viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam. Alimwacha naibu wake amalizie kazi.

Lakini kabla ya kuondoka aligawa, maswali yaliyokuwa yamechapishwa, kwa watawala na wafanyakazi. Wajaze. Wakusanye. Wampe naibu wake.

Lilikuwa darasa la aina yake. Kuombana kalamu. Kuchungulia majibu ya mwenzake. Kumaliza mapema na kumaliza wa mwisho. Kwa neno moja: Mshikemshike.

Mtihani wa waziri ulikwenda kwa njia hii, bila kujali mtiririko wala idadi ya maswali na maneno sisisi yaliyotumika:

1.           Katika miji yote shughuli za maji zinaendeshwa na chombo kimoja. Je, kuna haja ya kuwa na mashirika mawili (Dawasa na Dawasco) Dar es Salaam? Ukisema ndio au hapana, lazima utoe sababu.
2.           Je, kuna matatizo katika menejimenti ya Dawasco? Kama jibu ni ndiyo toa sababu na eleza nani ana matatizo gani na ameshindwa kutatua au kushughulikia matatizo gani?
3.           Je, kuna vitendo vya wizi ndani ya Dawasco? Kama jibu ni ndiyo, taja majina ya wahusika na maeneo yanayohusika.
4.           Makusanyo katika mwaka wa fedha 2010/2011 yalipungua ikilinganishwa na mwaka 2009/2010. Je, ni kwa nini?

Mtihani wa waziri ulikuwa “mtihani wa umma” lakini ulitolewa na kufanyiwa gizani. Hakukuwa na waandishi wa habari.

Ilikuwa baada ya Prof. Maghembe kuondoka, naibu wake Dk. Mahenge alihoji sababu za kutokuwepo waandishi wa habari katika “mkutano mkubwa kama huu.”

Alihoji, kama hakuna matatizo kwa nini hawataki wawepo waandishi wa habari ili waeleze umma?

Kwenye matengenezo ya bomba la maji Wazo na Salasala jijini Dar es Salaam, ambako naibu waziri alihudhuria na watu walikuwa wachache, waandishi wa habari walialikwa.

Waziri alipokwenda kutembelea mitambo ya maji, waandishi wa habari walialikwa. Mtoa taarifa anasema, akimnukuu naibu waziri, “…iweje leo katika mkutano mkubwa hivi wasiitwe ili waeleze umma?”

Bahati nzuri waziri hakuwa anatafuta jibu. Alikuwa akiwasukumia changamoto. Walitazamana tu.

Awali, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Arcard Mutalemwa alisoma risala ya mamlaka yake iliyoonyesha kutetea kuwepo kwa “mashirika” mawili (Dawasa na Dawasco) yote yakishughulikia jambo moja katika eneo moja.

Dawasa wanachimba visima. Wana mpango wa kuchimba visima 40. Hadi sasa visima sita (6) vimekamilika na waziri ameombwa kuvifungua.

Taarifa zinasema waziri “amesita kufanya hivyo,” akielekeza kuwa atafungua vikifika visima 20 na iwe kabla ya bunge la bajeti mwaka huu (kesho); jambo ambalo haliwezekani.

Risala ya Dawasco kwa waziri ilisomwa na makamu mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi, Salim Yusuf wa Mamlaka ya Mapato (TRA). Hii ilisema, pamoja na mambo mengine, kuwa Dawasco “hakuna matatizo.”

Risala ilisema kuna mambo yaliyoandikwa magazetini kuhusu Dawasco. Ilisema yalikuwa ya “kikundi cha watu wachache wenye maslahi binafsi;” na kwamba hilo “tunalifanyia kazi.”

Katika risala yao, Dawasco walilamikia fedha zinazokatwa kwenye mapato yao kwenda Dawasa, kuwa zimekuwa nyingi (zaidi ya asilimia 40); hasa baada ya ongezeko la bei kwa wateja. Wakaomba kiasi hicho kipunguzwe.

Waziri anasema atafanyia kazi majibu ya wafanyakazi. Yaweza kuwa wiki hii au ijayo au wakati wowote “atakapojisikia.”

Lakini ameacha kiwewe Dawasco na Dawasa. Je, nani ana kazi na nani yupoyupo? Nani anaweza kuondolewa na yupi anaweza kubaki? Kwa ufupi, nani atalia na nani atacheka.

Mmoja wa viongozi wa mamlaka hizo za maji, labda katika kuweweseka, alisikika kwenye kikao akisema, yeye ndiye (akitaja cheo chake) na kwamba bado hajasikia vyombo vya habari “vikitangaza mwingine.”

Mfanyakazi wa Dawasa amemwambia mwandishi wa habari hizi kuwa Jumamosi ilikuwa siku ya “kuanza kufikiria mahali pa kukimbilia endapo moja ya taasisi hizo itauawa.”

Mwandishi: Una maoni gani juu ya kuwepo kampuni moja…?

Mfanyakazi: Ukweli ni kwamba kazi za taasisi hizi zinaweza kufanywa na moja tu na kupunguza matumizi.

Mwandishi: Uliandika hivyo katika mtihani wenu?

Mfanyakazi: Hiyo ni siri yangu. Subiri waziri atangaze matokeo (kicheko).

Mwisho









No comments

Powered by Blogger.