Kila mwaka? Kama ndivyo, basi!
Na
Ndimara Tegambwage
SASA
bia wanywe wao. Soda wanywe wao. Sigara wavute wao. Sisi basi. Ebo!
Hivi
hapa ndipo mahali pekee ambako serikali inaweza kupata fedha za bajeti?
Twende
kwenye bia. Kama serikali inajali, kwanini
isiteremshe bei ya bia. Ili watu wengi waweze
kunywa au watu walewale waweze kunywa bia nyingi.
Ili kampuni ziweze kutengeneza bia nyingi.
Ili kampuni zipate mapato makubwa. Ili kampuni ziweze kulipa kodi kubwa. Ili
serikali iweze kunufaika kwa kodi kubwa. Kwanini?
Twende
kwenye soda. Kama serikali inajali, kwanini
isiteremshe bei ya soda. Ili watu wengi waweze
kunywa au watu walewale waweze kunywa soda nyingi.
Ili kampuni ziweze kutengeneza soda nyingi.
Ili kampuni zipate mapato makubwa. Ili kampuni ziweze kulipa kodi kubwa. Ili
serikali iweze kunufaika kwa kodi kubwa. Kwanini?
Twende
kwenye sigara. Kama serikali inajali, kwanini
isiteremshe bei ya sigara. Ili watu wengi
waweze kuvuta au watu walewale waweze kuvuta sigara nyingi.
Ili kampuni ziweze kutengeneza sigara
nyingi. Ili kampuni zipate mapato makubwa. Ili kampuni ziweze kulipa kodi kubwa. Ili
serikali iweze kunufaika kwa kodi kubwa. Kwanini?
Sasa
wanywaji hawana hamu tena! Ama serikali inywewe bia; inywe soda na ivute
sigara. Au wavitumie wanaovitengeneza.
Huo
hapo juu waweza kuonekana kama muweweseko wa
wanywaji soda, bia na wavuta sigara; bila kujua uchumi wa uzalishaji na masoko.
Lakini kwa viwango vyovyote vile, kuna mantiki.
Ukitokea
mgomo wa “kunywa” na “kuvuta,” mwezi wa sita wa mwaka wowote ule, nchi ikiwa
chini ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), bajeti haitasomwa kamwe. Haitakamilika.
Kila
mwaka ni bia, soda na sigara; hadi wenye viwanda wakaonya kwamba mwaka huu wakipandishiwa
kodi zaidi ya asilimia 10, hawataielewa serikali.
Kujaribu
kuonyesha “ubunifu,” serikali imekuja na pendekezo la wanaotaka usajili wa
magari kwa utambulisho wa taarifa za mtu binafsi – majina, labda na picha na
chochote kile – kulipa Sh. 5 milioni kwa miaka mitatu.
Ni
yaleyale ya bia, soda na sigara. Serikali inasema itakusanya Sh. 50 milioni katika
miaka mitato; kwa kutoza Sh. 5 milioni kwa atakayetaka urembo.
Hii
ina maana serikali imelenga watu 10 tu. Wakilipa milioni 50 kila mmoja,
serikali itakuwa imeridhika. Masikini!
Kama serikali inahitaji
fedha kwa njia hii, kwanini isitoze Sh. 200,000 kwa mwaka kwa gari kwa maelfu
ya magari ya vijana wanaotaka mbwembwe? Itapata zaidi.
Ukiangalia
orodha ya magari binafsi yaliyosajiliwa hadi sasa katika mfumo mpya, utaona
yametoka AAA hadi CAG. Haya ni maelfu ya magari. Serikali haitaki wanaoyamiliki
washiriki.
Kinachoonekana
hapa ni kwamba, watunga bajeti wanataka watu wachache (10), na huenda mafisadi
wachafu zaidi, wapate nafasi ya kujitambulisha kwa mbwembwe.
Kwamba
wezi wakubwa, wenye mabilioni ya shilingi ya kusambaza; mabilioni waliyopora umma
wa nchi hii; wapate nafasi ya kuwakoga wananchi na kuonyesha kwamba wao ni
tofauti.
Kwamba
mafisadi walioshindikana, sasa wapate nafasi ya kurudi upya katika umma, kwa
kuutisha, kuushangaza, kuukoga na kuudhalilisha kwa fedha walizowaibia.
Lakini,
hata kama kiwango kisingekuwa Sh. 5 milioni, au laki mbili; wazo lenyewe la
mikogo, katikati ya umasikini unaoandama wananchi, hakika ni la kibwege sana.
Aliyetoa
wazo hilo
barazani na “wataalam” walioliunga mkono ili kupata Sh. 50 milioni,
wamedhihirisha uchovu mchafu.
Hiki
ni kiasi ambacho serikali inaweza kupata katika siku nne tu kutokana na faini
kwa makosa ya barabarani katika jiji la Dar es Salaam peke yake!
Serikali
yaweza kupata kiasi hiki katika wiki moja au siku saba, kwa kusimamia kwa
makini, ukusanyaji kodi kwenye masoko.
Fedha
zinazohitajika ili kukidhi mbwembwe za kifisadi, zinaweza kupatikana – tena
mara kumi au ishirini au zaidi – kwa siku moja tu, kwa kufuta wilaya moja
iliyoundwa kisiasa na isiyo na manufaa kiuchumi kwa wananchi.
Watunga
bajeti hawaoni wezi wanaokwapua madini kweupe. Hawaoni mafisadi wenye kodi za
wananchi kwenye akaunti zao Ulaya. Hawaoni mabomba yanayovujisha mabilioni ya
shilingi kwa njia ya mishahara hewa.
Hawaoni!
Hawaoni safari za ndani na nje za watawala zinazokausha hazina na madarasa ya
Ngurdoto yanayokamua walipakodi. Hawaoni dege la serikali lilalo mafuta kama ibilisi. Hawaoni!
Hoja
ni hii. Kuna muda mwingi na mrefu wa kuandaa bajeti. Kitendo cha kuonekana serikali
inakwanyiakwanyia – shika hili shika
lile – dakika za mwisho, ni ushahidi watawala wanaishi kama
wapitanjia.
Na
mpitanjia hajengi.
0713
614872
No comments
Post a Comment