Header Ads

LightBlog

POLISI NA MAUAJI YA SHELABELA YA WATUHUMIWA

SITAKI Na Ndimara Tegambwage

Polisi wanaoua vyanzo vya taarifa

SITAKI mauaji ya kila siku. Kila wiki. Kila mwezi na wauaji wakiondoka tu bila kukamatwa. Bila kuhojiwa. Bila kusutwa. Bila kukemewa. Bila kuchunguzwa.

Hii ndiyo wanaita tuumachi! Polisi wanachukua bunduki. Wanaangamiza roho ya mtu mmoja, wa pili, wa tatu, wa nne, wa tano. Wanakunja sime. Wanaondoka. Nisikilizie: Tumeua majambazi. Halafu? Kimya. Utadhani hakuna kilichotokea.

Taarifa za magazeti zimeeleza kuwa saa nane na nusu mchana; kweupe kabisa kwa tarehe 29 Novemba – wiki iliyopita tu – watu watano waliuawa katika kijiji cha Park Nyigoti wilayani Serengeti, katika mkoa wa Mara.

Eti polisi wakishirikiana na askari wa hifadhi ya mbuga ya Serengeti, waliwapiga risasi na kuwaua watu watano “wanaosadikiwa kuwa majambazi.” Ama walipiga mmojammoja au kwa risasi zilizotoka kwa mpigo; waliwateketeza wote fyuu!

Kama kawaida, polisi wakaondoka tu bila kujikamata. Bila kujihoji. Bila kujisuta. Bila kujikemea. Bila kujichunguza. Lakini pia bila kuhojiwa, kusutwa, kukemewa wala kuchunguzwa.

Ilikuwa 19 Novemba, wiki mbili na nusu zilizopita, watu sita waliuawa na polisi mkoani Dodoma. Hao pia “walisadikiwa kuwa majambazi.” Gun! Gun! Gun! Hadi sita. Polisi wakaondoka. Hawakujikamata, hawakujihoji, hawakujisuta wala kujichunguza. Vijana wanasema “imetoka hiyooo!”

Kama unataka maelezo juu ya ilivyotokea, sharti uwe unajua lugha na mwepesi wa kuchambua. Maneno yanayotumika ni istilahi maalum ya kipolisi: “Waliuawa wakati wa kujibizana kwa silaha na polisi.” Hayo ndiyo mazingira ambamo wanakufa wale wanaoshukiwa, wanaodhaniwa na, au wanaosadikiwa kuwa majambazi.

Siku sita baadaye, ilikuwa 25 Novemba, polisi waliripotiwa kuua kwa kupiga risasi, “majambazi” sita huko Biharamulo mkoani Kagera. Gun! Gun! Gun! Wote sita, chini. Taarifa zinasema walikutwa na silaha za moto.

Kama kawaida, hakuna polisi aliyekamata polisi kwa kuua. Hakuna aliyemhoji mwenzake. Hakuna aliyemsuta mwenzie. Hakuna mwenye nia ya kumchunguza mwenzake. Kimya. Utadhani umo kwenye tumbo la papa.

Kumekuwa na taarifa za kutupiana risasi, kati ya polisi na “majambazi” lakini kama ilivyo kwa sinema za Chuck Norris, mara zote hizi polisi ndio washindi – hawafi na kama wameumia sana, basi ni michubuko.

Mtindo huu wa polisi kuua “majambazi” au “wanaosadikiwa” kuwa majambazi au “wanaoshukiwa” kuwa majambazi hautalifikisha taifa hili popote katika vita dhidi ya ujambazi. Hatimaye polisi wataitwa wauaji tu. Ikitokea hivyo, hawataweza kujitetea.

Polisi aliyekabidhiwa bunduki ni yule aliyejifunza jinsi ya kuitumia kitaalam. Anapotumwa kwenye kazi ya kusaka majambazi, haendi au hapaswi kwenda kwa nia moja tu; kuua. Hapana. Kuna mambo mengi yanatarajiwa.

Polisi amefunzwa kulenga shabaha. Amefunzwa jinsi ya kutokuwa na kiwewe na harara katika mazingira ya “uwindaji” wa aina hiyo. Amefunzwa jinsi ya kurudi na ushahidi unaoongea ambao ni muhimu sana kwa mipango na operesheni za baadaye. Polisi hapelekwi tu kuua na kurejea na maiti.

Tena wajuzi wa kutumia silaha – wale wenye shabaha ya kuonea wivu – ndio wanahitajika sana; siyo kwa kupasua ubongo au moyo; bali kwa kupiga mguuni na takoni ili waweze kulegeza muhusika, kumkamata na kumhoji kwa manufaa ya kazi zao za baadaye.

Ni kweli polisi waliotumwa kazi waweza kujaa kiwewe na woga uliopindukia na kuanza kufyatua risasi hata bila kutumia utaalam waliopata vyuoni. Ni kutokana na uwezekano huo kunakuwa na haja ya kutaka kujua jinsi operesheni zinavyoendeshwa.

Ndio maana hata kwa upande wa polisi kuna haja ya kuulizana: Mbona mmeua wote? Mbona hamkuleta hata mateka mmoja? Mazingira yalikuwa vipi hadi mkaishia kuua tu? Ndio maana kuna haja ya kujikamata, kujihoji, kujisuta, kujikemea, kujichunguza na hata kujiadhibu.

Hivi ni kweli kwamba polisi wa Tanzania wanatumwa kuua tu? Hawataki mateka? Kama hawarudi na mateka watapata vipi taarifa za majambazi au wanaotuhumiwa kufanya ujambazi?

Gun! Gun! Gun! Watu 17 katika siku 20; ambao ni wastani wa kuua mtu mmopja kila siku; hakika hii haiwezi kuwa kazi bora ya polisi na hata ikilazimishwa kuwa, haiwezi kuwa na tija. Hii ni kwa kuwa hakuna maghala ya majambazi kiasi cha kufikiri kuwa jinsi wanavyouawa, ndivyo wanavyopungua katika maghala.

Uhalifu unamea katika ngazi mbalimbali katika jamii kwa vishawishi na motisha kadha wa kadhaa. Hapa umekomaa na kuwa wa matumizi ya kalamu ndani ya mabenki na serikali; pale umekomaa na kuwa wa matumizi ya silaha; pengine bado haujafumuka na labda kwingine ungali unasuasua.

Kwa hiyo, kuua raia kwa kuwa umemshuku au kwa kuwa amekutwa na silaha, hakusaidii polisi wala serikali. Moja ya kazi kubwa za heshima ambazo zinapaswa kufanywa na polisi, ni upelelezi.

Kupeleleza kunahitaji vyanzo vya taarifa. Vyanzo vizuri vya taarifa, hata kama itabidi taarifa hizo kuchambuliwa kwa makini sana, ni mateka na siyo wafu. Ukiua vyanzo vya taarifa na kurudi unajipiga kifua, utashindwa kumaliza uhalifu.

Kuua kunaweza kuwa na shabaha nyingine. Shabaha ya kuficha ushahidi muhimu. Ili waliouawa wasijulikane wana uhusiano na nani katika polisi, katika biashara au katika utawala.

Mauaji yakiendelea kwa miaka mingi yanakuwa njia ya kuondosha watu wasiokubaliana na polisi, watu mashuhuri au serikali. Katika baadhi ya nchi mauaji ya aina hiyo yamewakumba wapinzani wa watawala.

Hapo kuua huwa kunazoeleka na yeyote aweza kuokotwa kokote, kupelekwa Serengeti, Ngorongoro au hata Loliondo, kuuawa hukohuko na taarifa zikasambazwa kuwa “alikuwa mmoja wa majangili sita bali wengine aliokuwa nao wamekimbia.”

Kuruhusu polisi kuendelea kuua watuhumiwa wa ujambazi, kunaweza kuleta madhara zaidi kwa taifa. Kunajenga unyama usiomithilika nyoyoni mwa wauaji na woga miongoni mwa wananchi.

Kunadumaza utaalam katika idara ya upelelezi ambayo sasa inabakia kutegemea uvumi. Kwani, upelelezi hukomaa zaidi katika mazingira ya uhalifu na huimarisha nyanja mbalimbali za sheria ambako mbongo huchuana na kuweka misingi mipya ya kutafsiri sheria zilizopo na hata kutunga nyingine.

Kuendelea kuua watuhumiwa kunaharibu jina, sura na tabia ya nchi na wananchi – kwamba nchi na watu wake wanaitwa wauaji; lakini pia kunajenga mazingira ya kuviziana na hata mafisadi kutumia mwanya huo kuangamiza wasiowaabudu.

Kuua siyo njia bora ya kukabiliana na uhalifu. Hakika kuua kunaweza hata kuchochea uhalifu zaidi. Siku zote polisi waende kukamata, kupata vyanzo vya taarifa vya kuwasaidia katika uchunguzi na baadaye katika hatua za kukabiliana na ujambazi.

Penye mfumo mzuri wa matumizi ya polisi, mauaji ya watu watano, watano na baadaye sita, katika siku 20 tu, hayawezi kufumbiwa macho. Kama ndani ya jeshi la polisi na serikali hawaulizani “kulikoni,” basi wananchi wana kila sababu ya kuuliza.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

No comments

Powered by Blogger.