Header Ads

LightBlog

POROJO ZA SERIKALI NA MISHAHARA YA WAFANYAKAZI

SITAKI

Porojo za serikali kuhusu mishahara


Na Ndimara Tegambwage

SITAKI waziri anayejifariji kwa kauli ndogo na rejareja hasa katika masuala yanayohitaji busara na hekima.

Anachokifanya Profesa Juma Kapuya, waziri wa kazi, ama kwa utashi binafsi au kwa kuagizwa na serikali, kinamuumbua na hata kuumbua serikali.

Wafanyakazi wamesema watafanya mgomo kuanzia 5 Mei mwaka huu kushinikiza serikali kushughulikia maslahi yao. Wamesema pia kwamba hawamwaliki rais kwenye sherehe zao za Mei Mosi mwaka huu.

Profesa Kapuya, kwa mizaha yake, akijua kuwa madai ya wafanyakazi ni nyongeza ya mishahara, amekurupuka na kusema mishahara katika sekta binafsi imeongezwa kwa asilimia 100.

Aliwaambia waandishi wa habari Jumanne iliyopita kwamba Mwanasheria Mkuu wa serikali atatangaza hivi karibuni, katika gazeti la serikali, ongezeko la asilimia 100 kwa mishahara katika sekta binafsi.

Serikali au Kapuya wanapata wapi ujasiri wa kuongeza mishahara ya sekta binafsi lakini wanashindwa kuongeza mishahara kwa watumishi wake? Wana uhakika gani kwa viwango hivyo vitalipwa na vinakubalika?

Kama Kapuya anasema nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa serikali inahitaji majadiliano zaidi, kwa nini majadiliano hayo ya kina yasihitajike katika sekta binafsi inayolipa kodi serikalini?

Waziri wa kazi anasema mwanasheria “atatangaza hivi karibuni” nyongeza ya mishahara. Hivi karibuni ni lini hasa? Baada ya Mei Mosi? Kabla ya mgomo wa 5 Mei? Baada ya mgomo?

Kama serikali ina uwezo wa kuahidi kitu “hivi karibuni,” ilishindwa vipi kuchukua hatua muda wote tangu wafanyakazi wadai mafao na kufikia hatua ya kutaka kufanya mgomo?

Hili ndilo linafanya wengi wajenge mashaka juu ya nia na shabaha ya serikali. Au, kwa vile serikali inasema haishughulikii mishahara ya watumishi wake, basi itumie sekta binafsi kuepusha songombindo hili?

Hivi nani amemwambia Kapuya na serikali yake kwamba wafanyakazi wanataka “tangazo la mwanasheria mkuu” wa serikali? Tangazo ni la nini hasa? Mbona katika madai ya wafanyakazi hakuna tangazo?

Je, tangazo la mwasheria wa serikali linaloahidiwa “hivi karibuni,” likija kweli hivi karibuni na kusema mishahara itaongezwa lakini itakuwa mwaka kesho, litakuwa limekidhi haja ipi?

Kapuya na, au serikali, wameongea lini na wafanyabiashara, wenye viwanda na wakuu wa maeneo mbalimbali ya sekta binafsi?

Lini na wapi serikali ilikubaliana na watawala wa sekta binafsi kuwa kuanzia sasa walipe asilimia 100 ya mishahara ya wafanyakazi wake?

Lini serikali ilikutana na wafanyakazi au viongozi wake; kujadili kwa kina na kukubaliana kuwa hicho ndicho kiasi wanachotaka – siyo zaidi wala pungufu – na hivyo kuanzisha mijadala na waajiri?

Nani ameidanganya serikali kuwa inaweza kutoka usingizini wakati wowote; au inaweza kuchomoka katika fukuto la woga wa migomo ya wafanyakazi na kuamuru waajiri kutoa viwango vya mishahara kama inavyotaka?

Sasa baadhi ya waajiri katika sekta binafsi wameanza kusema kuwa hawataongeza mishahara. Wengine wanasema wanaweza kuongeza mishahara lakini itabidi wapunguze wafanyakazi.

Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), kikiongea kupitia msemaji wao Aggrey Mlimuka kilieleza kidiplomasia juzi Ijumaa kuwa kinaangalia mwenendo huu na kuchunguza la kufanya.

Kwa vyovyote vile, sasa serikali imechokoza nyuki. Kwanza imeleta ubaguzi kwa kusema itatangaza mishahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi na kuwataka watumishi wake “kusubiri.”

Hivi hao watumishi wa serikali watasubiri hadi lini ili wapate angalao tangazo la kupandishiwa mishahara kinadharia kupitia mwanasheria mkuu wa serikali; achilia mbali kulipwa?

Pili, serikali imeingiza waajiri katika mgogoro wake. Nao wameanza kuitilia mashaka na kupinga hatua yake; siyo kwa kauli rejareja bali kwa vitendo vya kupunguza idadi ya wafanyakazi – jambo ambalo serikali haikutegemea.

Tatu, imekuza mapambano dhidi yake kwani wafanyakazi sasa wanaona kuwa serikali inataka kutumia mbinu ya kuwagawa kwa misingi ya sekta – binafsi na umma – ili kuwadhoofisha.

Profesa Kapuya na serikali wanakumbuka kuwa wakati fulani walitangaza nyongeza ya mishahara bila kushirikisha waajiri na waajiri, hasa wenye viwanda, wakakataa mapendekezo na amri za serikali.

Baadhi ya wenye viwanda walikuja na mapendekezo yao wakitaka serikali ikubaliane nao kwa mujibu wa maelezo kuhusu mapato, matumizi na matarajio ya viwanda.

Kama kuna wakati serikali iliumbuka na kudhalilika, basi ni wakati huo. Ilibidi waziri wa kazi afanye kazi ya ofisa wa uhusiano wa makampuni hayo – akieleza jinsi ambavyo viwanda havitamudu kulipa mishahara hiyo – na kufikia hatua ya kuweka viwango vipya.

Yote haya yamekuwa yakifanywa kwa kasi na bila kuwa makini kwa vile kwa kipindi kirefu serikali inadharau matakwa, wito na madai ya wafanyakazi. Hivyo inakurupuka hatua za lalasalama na kulazimika kutumia hata viinimacho.

Hata baada ya Rais Jakaya Kikwete kutoa kauli iliyofanana na kuwaangukia wafanyakazi, bado hakuna hatua za haraka zilizochukuliwa kukutana nao na kuwasikiliza kwa makini.

Tatizo kubwa ni kwamba watawala Tanzania, baada ya kurithishana madaraka kwa miaka yote hii – nusu karne – wamekuwa na tabia ya kuamini kuwa yanayosikika nchi za nje; ya wafanyakazi kugomea rais na serikali yake, hayawezi kufanyika hapa.

Hakuna wafanyakazi wenye musuli la vyuma. Hakuna wenye damu ya kijani. Kote duniani wafanyakazi wamekomazwa na mazingira yao.

Mahala pengi wamekomazwa na tabia na vitendo vya watawala. Bila kukohoa, kupaza sauti, kukemea, kukemea, kupanga na kupangua, kuandamana na kugoma, basi haki haipatikani.

Hilo ndilo linaunganisha wafanyakazi kote duniani: Kwamba kazi wanafanya lakini wananyonywa, wananyanyaswa na hawasikilizwi. Bila kuungana hawafiki popote.

Kwa njia hii huwezi kusema wafanyakazi wa Tanzania wana damu ya kijani na hivyo watakuwa na upole wa kondoo. Hapana.

Acha wasimame imara kudai chao. Wasipokipata leo watakipata kesho, mradi hawalazi msuli. Na kama serikali haitasikia leo, bila shaka itasikia kesho, na huenda katika mazingira tofauti na leo. Kapuya upoo?


0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

No comments

Powered by Blogger.