Header Ads

LightBlog

KAWAWA NA 'USIMBA' WAKE

SITAKI


Wanaotaka kuzika ‘ujasiri’ wa Kawawa


Na Ndimara Tegambwage

SITAKI Watanzania wasahau Rashid Mfaume Kawawa; ingawa hakika watamsahau. Kama wamesahau Julius Kambarage Nyerere, sembuse “kibarua” wake.

Kawawa – Waziri Mkuu, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais na wakati huohuo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, aliaga dunia juzi, Alhamisi akiuza uyoga.

Tusemezane. Tuambizane ukweli. Wakati aliyewahi kuwa na madaraka, nyakati hizo, ya kuumba na kuumbua anakufa akiuza uyoga, karani mmoja wa Benki Kuu (BoT) anajengewa nyumba kwa Sh. 1.4 bilioni.

Msanii wa viwango vyake, Kipanya, amefafanua nyumba ya karani wa BoT kama ifuatavyo: “Tumetumia bilioni moja point four tu kujenga my haus…Vere spesho haus. Ukija moto inajizima, yakija mafuriko inapaa.” Utaongeza nini hapa?

Pamoja na vyeo vyote alivyokuwa navyo, Kawawa hakuweza kujichotea mabilioni ya shilingi au kutumia nafasi yake kulainisha wahusika ili apate fedha za kufanyia biashara, kujenga nyumba za kifahari au kulalia katika mto (takia) au mfaliso. Wanasema kwa kejeli, “Yule alikuwa mjinga kama Nyerere kaka yake, au alimwogopa.”

Kwa hiyo katika mazingira haya, Kawawa aweza kusahaulika haraka. Hapana. Tuseme ukweli. Aliishasahaulika. Jina lake limerejeshwa na kifo chake; misururu ya kumuaga, kumzika na kutandaza unafiki wa kisiasa wa kutoa sifa kemkem kwa mtu ambaye uwezekano wake wa kuwakemea haupo tena.

Na atafutika haraka kweli. Hii ni kwa sababu Kawawa hakuandika vitabu. Hotuba zake hazikuhifadhiwa na kutungwa uzi na kuwa vitabu. Hakuandikwa sana na kufanyiwa utafiti kama Nyerere. Yeye hakuandika.

Juhudi za msomi mmoja ambaye hivi karibuni alitembelewa na busara za kuandika kitabu juu ya Kawawa, ni miongoni mwa watu wachache sana ambao wamehifadhi tunda la kichwa na mikono ya Kawawa.

Vinginevyo, Kawawa alikuwa mtekelezaji zaidi kuliko mwana-nadharia. Nyerere, ambaye aliamini na kuheshimu akiishasema, basi. Fikra au agizo linalotoka katika kichwa kinachoaminika kuwa sahihi, linapaswa kutekelezwa kuliko kufanyiwa porojo. Huyo ndiye Kawawa.

Kawawa hakuzalisha mawazo kwa njia ya nadharia. Alitenda. Alitekeleza kilichoamuliwa. Hakuwa na nia, sababu wala muda wa kurudia miito. Vyombo vya habari vilinukuu amri zake. Havikumchabua. Ama viliogopa, hasa wakati wa mfumo wa chama kimoja; au vilikuwa na ukame wa waandishi wenye upeo mkubwa.

Kuishia kudonoa na, au kuchambua maamuzi, sera, kanuni na taratibu; bila kujadili, kuchambua na kutafiti vitendo vya Kawawa, kumefanya mwanasiasa muhimu katika Tanzania kuwa na ukame wa fikra. Kumbe wenye ukame ni wale walioshindwa kutafsiri utendaji wake na kuupa nadharia.

Rashid Mfaume Kawawa hakutaka mjadala juu ya kilichoamuliwa. Alitaka utekelezaji. Hata pale Mwalimu Nyerere alipoonyesha kutoelewa au kutoafikiana na jambo fulani, yeye alikuwa wa kwanza kutenda, kwa njia ya kurekebisha, ili lifanane na Mwalimu alivyotaka.

Katika nyakati za mfumo wa chama kimoja na magazeti mawili – la serikali na la chama (TANU), ambako watawala walikuwa wakitumia kauli, “kama nchi tumeamua;” Kawawa, kama wanasiasa wengine, alisema chochote alichokuwa nacho huku akijiaminisha kuwa “vijana wetu” – waandishi wa habari – “watayaweka sawa.”

Ni nyakati hizo waandishi wa habari walitakiwa kujua viongozi wanataka kusema nini. Hata pale walipokosea kuelezea sera au siasa za nchi, mwandishi alitakiwa kuwa makini na kufafanua, kana kwamba ni yeye aliyekuwa anahutubia, msimamo na utashi wa serikali na kuweka wazi kuwa ndiyo hayo yaliyoelezwa na kiongozi, au Kawawa.

Chukua mifano hii. Nyerere aliongelea unyonyaji unaofanywa na wenye maduka na kueleza kuwa hali ingekuwa tofauti iwapo kungekuwa na maduka ya ujirani.

Palepale Kawawa alianza kwa kuamuru maduka ya watu binafsi yafungwe kwa kuwa yalikuwa ya “kinyonyaji.” Nchi ilitikisika chini ya kilichoitwa “Operesheni Maduka.” Bidhaa zikakosekana karibu na walipo wananchi. Haraka ya kutenda ambayo ilikuwa sura kamili ya Rashid Mfaume Kawawa. Ilichukua muda kurekebisha hilo.

Mfano wa pili. Waliokuwepo watakumbuka Kawawa alivyoamuru Umoja wa Vijana wa TANU kusimamia operesheni ya kuvaa nguo za heshima. Vijana wa kike waliovaa nguo fupi walikamatwa na baadhi yao kushikiliwa katika mazingira ya kutatabishwa yaliyoitwa “udhalilishaji.”

Kama siyo Nyerere kuingilia kati na kusema mavazi ni “fasheni tu” – zinakuja na kupotea, maisha mijini, na hasa Dar es Salaam, yalikuwa yameanza kuwa magumu kwa vijana wa kike. Lakini ni utekelezaji.

Chukua mfano mwingine wa kuhamia vijijini. Kawawa akiwa mtendaji mkuu, alitaka kila mmoja ahamie kwenye vijiji vilivyopimwa na alisisitiza sera hiyo kama ilivyoelezwa, kufafanuliwa na kuelekezwa na TANU na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.

Ninajua vema kilichotendeka. Nilikuwa mwandishi niliyeshuhudia uhamishaji katika wilaya ya Kahama. Nyumba na maboma ya mifugo vilichomwa moto. Mifugo ilisambaa. Watu walisombwa kwa malori hadi “vijiji vilivyoandaliwa” ambako hakukuwa na nyumba bali kusanyiko la wengine waliosombwa kama mizigo.

Tukiwa katika ziara na Mwalimu Nyerere, mikoani Shinyanga na Mwanza, wananchi walijitokeza na kumwambia Mwalimu kuwa walitoka kwenye neema na kupelekwa kwenye majuto. Mzee mmoja aliyesimamisha msafara wa rais alisema, “Kuku wangu akitoka nje, tayari ameingia kwa jirani; sasa hapa ni kijiji kweli. Tunaishi kwa kugombana.”

Hata matatizo ya kuku, maji, nyumba alitwishwa Kawawa. Wakati Nyerere aliyezalisha mawazo alibaki shujaa wa kufikiri, msimamizi wa utekelezaji alivuna lawama na laana: Rashid Mfaume Kawawa.

Karibu sera zote za TANU na baadaye CCM, zilizojaa fikra fikirishi – kuanzia Azimio la Arusha – hazikuwa na mipango mkakati wala mipango ya utekelezaji. Ndiyo maana hata sera nzuri kama “Elimu ya Kujitegemea” ilikosa mwelekeo.

Miaka 20 baada ya Azimio la Arusha, kwenye kongamano la walimu wa siasa katika vyuo vya TANU, lililofanyika Chuo cha Kivukoni, Dar es Salaam, walimu walipoombwa kutoa maana ya elimu ya kujitegemea zilitokea tafsiri saba (7).

Walitofautiana juu ya utekelezaji kwa vile hawakuwa na mpango mkakati wala mpango wa utekelezaji. Yote haya alilundikiwa Kawawa. Mwalimu alifikiri, Kawawa alisimamia utekelezaji na kuvuna lawama.

Lakini Kawawa, kama Mwalimu Nyerere hawakukimbia matunda ya kazi zao. Nyerere ndiye alianzisha utaratibu wa kukiri makosa, hata kabla hajaulizwa, na kupendekeza masahihisho. Kwa njia hii alimnusuru “mpiganaji mwenzake” mara nyingi kabla hajalaumiwa, kushutumiwa na kulaaniwa.

Lakini Kawawa anakumbukwa kwa kile wengi wanaita “uaminifu.” Historia haionyeshi mahali popote ambapo Kawawa alionyesha jeuri kwa Nyerere; kupingana naye waziwazi au kumhujumu. Inaonyesha tumshikamano, kukubaliana na kutenda “bila swali.”

Huu ulikuwa woga au utii? Kuna majibu mengi kwa swali hili. Lakini kinachoonekana wazi na haraka ni kwamba kulikuwa na mshikamano wa kikomredi, kati ya Nyerere na Kawawa – kila mmoja akisema na kuapa kuwa “tunachofanya ni kitu chetu hadi mwisho.”

Sasa Kawawa hayupo nasi tena. Alazwe mahali pema anapostahili. Katika hili hatuna uamuzi. Bali kwa nini tusimkumbuke kwa haya machache – ujasiri wa kutenda hata pasipo na mpango kazi; urafiki na ukomredi usio na unafiki; na kutopenda makuu. Hivi havijafa.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

No comments

Powered by Blogger.