Header Ads

LightBlog

SERIKALI NA SHERIA ZA KISHETANI

SITAKISheria ya kishetani ya Waziri Mkuchika


Na Ndimara Tegambwage

SITAKI kuamini kwamba Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika anafanya kazi ya serikali. Hii ni kwa kuwa serikali nzima haiwezi kuwa na fikra finyu kiasi hiki. Haiwezekani.

Ijumaa iliyopita Mkuchika alitangaza kufungia gazeti la KuliKoni kwa siku 90. Waziri anadai gazeti limekiuka Sheria ya Usalama wa Taifa kwa kuandika “habari za jeshi.”

Waziri anasema “kosa” lilitendeka 27 Novemba 2009 pale gazeti lilipoandika juu ya kuvuja kwa mitihani ya jeshi na kuwepo uwezekano wa upendeleo kwa wasiostahili.

Mkuchika, kama Sheria ya Magazeti ya 1976 inavyosema, ana mahakama yake binafsi. Iko akilini mwake. Iko mikononi mwake. Iko mdomoni mwake. Anatamka kuwa habari iliyoandikwa na KuliKoni “ni ya uwongo.”

Ushetani wa Sheria ya Magazeti ni kwamba inasema anachosema waziri ndicho. Sheria iliyotungwa na binadamu mwenye kasoro na walakini kadha wa kadhaa, inampa waziri mamlaka ya kuumba na kuumbua, bila kupitia mahakamani.

Sasa Mkuchika anasema gazeti limesema uwongo. Hiyo ni katika mahakama ya akilini mwake kama alivyopewa mamlaka na sheria ya magazeti ambayo inamruhusu pia kufungia na hata kufuta gazeti bila kutoa sababu yoyote.

Kama kuna nchi ambako serikali zinaweza kuja na kupita na wakati huohuo kujiviringisha katika mazingaombwe na kuyarithisha kwa serikali zinazofuata, basi ni Tanzania.

Kwani kuwa na sheria ambayo inampa waziri uwezo wa kuamua anavyotaka, ni kufanya taifa kuwa la wanasesere wanaochezeshwa kwa vidolegumba.

Ukweli ni kwamba wengine – sisi – siyo wansesere. Hata kabla ya Tume ya Jaji Nyalali (1992) tulikuwa tumepaza sauti na kusema Sheria ya Magazeti ni ya kishetani; ni ya kishenzi.

Ripoti ya Tume ya Nyalali ilipokuja, ikaleta hoja kuwa sheria hiyo ama ifutwe au ifanyiwe marekebisho makubwa. Watawala wamekaa kimya. Wanaipenda. Wanaipakata. Wanampa Mkuchika aitumie atakavyo. Mkuchika anataka.

Ukiona watawala wanapenda sana sheria chafu, ujue kuwa roho, nia na shabaha zao ni chafu. Huwezi kulinda chema kwa kutumia sheria chafu. Huwezi kulinda kitakatifu kwa kutumia sheria ya kishetani. Utatumia sheria chafu kulinda kichafu. Huo ndio muwafaka. Mkuchika anataka.

Sisi, katika tasnia ya habari, tulianza kupaza zaidi sauti za kutaka sheria ya magazeti ifutwe tangu zaidi ya miaka 30 iliyopita. Ushahidi upo. Kila tulipopaza sauti ndivyo watawala walivyoweka sheria hiyo mbelekoni; kipenzi chao.

Leo KuliKoni imekumbwa na mkasa ulioikumba MwanaHALISI. Imefungiwa na Mkuchika kwa siku 90 kwa uamuzi wa waziri asiyependa kwenda mahakamani wala asiyeshawishi wahusika kwenda Baraza la Habari Tanzania.

KuliKoni imekumbwa na sheria inayoruhusu waziri kutumia utashi binafsi, mapenzi, chuki na hata husuda kufungia gazeti – mdomo wa umma. Mkuchika anataka sana.

Mkuchika anasema amelalamikiwa na jeshi. Jeshi lina uwezo wa kwenda kwenye Baraza la Habari na kulalamika. Jeshi linaweza pia kwenda mahakamani. Kwani jeshi ni nini kama siyo Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa? Waweza kulalamika popote.

Waziri Mkuchika hataki jeshi lihangaike. Hataki hata jeshi liunde Tume ya kuchunguza kama lilivyopendekezewa. Anakaa kitini na kusema gazeti limesema uwongo kwa kuwa sheria inamruhusu kuumba na kuumbua. Mkuchika anataka.

Taarifa ya gazeti, inayosema mfumo wa utungaji na ufanyaji mitihani ya kijeshi unawapa nafasi maofisa wasiostahili, inawezaje kuwa kitu cha kubomoa “usalama wa taifa?” Tangu lini usalama wa taifa umekuwa mweroro kiasi hicho?

Gazeti limetoka leo na malalamiko ya wahusika yanatoka siku hiyohiyo, hata kabla ya kuulizia wala kufanya uchunguzi. Kanusho la aina hiyo lina uzito gani?

Msajili ya Magazeti ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Tanzania (MAELEZO). Huyu anaamuru tu: “Jieleze kwa nini usichukuliwe hatua.” Basi. Yeye hafanyi uchunguzi angalu kupata mwanga na kusaidia walalamikaji.

Anaposema hakuridhika na kauli au majibu uliyotoa, ina maana kuwa ni suala la binafsi linalotokana na kutojua kinachoendelea au ni la kushinikizwa na aliyemlalamikia au woga tu kwamba jeshi limetajwa.

Katika mazingira haya, waziri anadai kuwa taarifa ya gazeti imefedhehesha “jeshi letu na kulipaka matope.” Mkuchika amepata wapi fedheha? Amepata wapi matope wakati hata aliyelalamika hajaweka ushahidi wake hadharani mbele ya chombo chenye hadhi ya kutoa maamuzi?

Hata katika suala la kujieleza; waziri anataka maelezo yenye ushahidi ili ayatumie wapi wakati yeye hafanyi uchunguzi wala hana chombo cha haki cha kutoa maamuzi?

Gazeti la MwanaHALISI bado lina kesi na serikali inayotokana na hatua ya Mkuchika kulifungia kwa siku 90 bila sababu ya msingi. Hapana, ni zaidi ya hapo.

Kuna kesi mahakamani, inayotafuta kufutwa kwa sheria ya magazeti. Haijaamuliwa. Ilichochewa na kufungiwa kwa MwanaHALISI na ndio walalamikaji.

Hata kabla kesi hiyo haijatolewa maamuzi, Mkuchika anaendeleza ubabe wake. Anaita taarifa za gazeti juu ya mitihani ya jeshi kuwa ni za “uchochezi” na analifungia kwa siku 90. Wako wapi wanasheria wa KuliKoni?

Huyo ndiye Mkuchika chini ya mwavuli wa serikali. Sheria ipo. Watawala wanaipenda. Mawaziri wanaoteuliwa huipenda, kuitii na kuinyenyekea kwa kuwa tatizo lao kuu ni “mlo.”

Hajapatikana waziri wa kukataa kutumia na kutumikia sheria chafu; angekuwa ametoa funzo. Hajapatikana wa kuasi utumwa wa sheria hii kwa kuwa wengi wanatafuta mlo.

Huwezi kutumikia umma ambao umeufunga mdomo. Basi huutumikii bali unausulubu katika utumwa wa mawazo na hatimaye katika vitendo. Utapataje mawazo yake? Utapataje malalamiko yake? Utapataje ushauri wake?

Ni heshima na halali, kwa waziri, msajili wa magazeti, maofisa wa habari serikalini, waandishi wa habari, wadau wengine wa habari na wananchi, kuasi sheria katili.
Kwa pamoja tunaweza kuvunja mikatale hii.

0713-614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

No comments

Powered by Blogger.