ADHABU YA KIFO IMEPITWA NA WAKATI
Kunyonga siyo adhabu, ni kuua tu
Na Ndimara Tegambwage
SITAKI kuona wananchi na watawala wakishabikia hukumu ya kunyonga, hata kama kuna sheria ya nchi inayoruhusu mtu “kunyongwa hadi kufa.”
Sheria iliyopo ni katili, chovu, inayopaliliwa na kuendelea kurutubishwa na mfumo unaoendeshwa na watu ambao wamekuwa wagumu kuelewa mantiki ya thamani ya maisha na umuhimu wa adhabu.
Iwapo hawatakata rufaa, au wakikata rufaa na kushindwa, Masumbuko Madata, Emmanuel Masangwa na Charles Kalamuji, waweza kuuawa kutokana na hukumu iliyotolewa na Jaji Gabriel Rwakibalila.
Jumatano iliyopita, mjini Kahama, Jaji Rwakibalila aliwakuta vijana hao watatu na hatia ya jinai ya kuua Masumbuko Dunia, mtoto wa shule, umri wa miaka 13 na mwenye ulemavu wa ngozi (albino). Sasa kuna wanaoshangilia hukumu ya kifo.
Kifo cha Masumbuko kiliuma na kuumiza wengi, hata kama hawakuwa na uhusiano wowote naye. Umri wake mdogo; nafasi yake katika jamii iliyosababisha kuitwa majina ya kumtelekeza; utu wake ambao ulikuwa na bado ni sehemu ya utu wa kila mtu; ni sehemu tu ya chimbuko la uchungu.
Uchungu unakuwa mkubwa pale jamii inaposhuhudia mauaji yakilenga watu wenye ulemavu wa ngozi; wadogo kwa wakubwa, kwa sababu dhaifu, za kijinga na potofu – eti kupata viungo vya kuwawezesha “kuwa matajiri.”
Uchungu huu usio na udhibiti, unapokutana na sheria ambayo hata Jaji Mkuu Augustino Ramadhani amewahi kusema kuwa hafurahii kuitumia, ndipo unazaliwa ukatili mpya; ule wa kuondoa uhai wa aliyepatikana na hatia ya kuua.
Mahakama Kuu nchini Tanzania iliishawahi kutamka kuwa adhabu ya kifo ni ya kikatili na ya kudhalilisha na kutaka ifutwe. Pamoja na maeneo mengine, maneno “katili” na “kudhalilisha” ni ya msingi sana katika kuchambua hukumu ya kifo.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano inakataza ukatili na udhalilishaji. Kwa hiyo kuwepo sheria inayoruhusu kuua; hivyo kuendesha “ukatili” na “udhalilishaji,” ni kuvunja katiba ya nchi. Lakini Mahakama ya Rufaa haikuafiki.
Hakuna ubishi kwamba vijana watatu wa Kahama, kwa kupatikana na hatia ya kumuua Masumbuko, walivunja haki za binadamu. Bali “haki za binadamu” haziwekwi na watu; zipo na zinahusu kila mmoja.
Watawala, sheria na hata Katiba za nchi, haziweki haki za binadamu. Ngazi zote hizo hazina uwezo wa “kugawia” watu haki za binadamu. Kinachofanyika ni kwa watawala, sheria na Katiba kutambua kuwepo kwa haki hizo na kutafuta jinsi ya kuzilinda na kuziendeleza.
Kwa hiyo, hapa siyo mahali pa hoja za jino kwa jino. Hoja ni kutovunja haki za binadamu. Kutoua. Kutofanya ukatili. Kutodhalilisha.
Hoja hii inaleta maana zaidi pale tunapojadili “thamani” ya adhabu anayopewa mkosaji. Watatu wa Kahama wamepatikana na hatia. Wamevunja haki za binadamu kwa kumuua Masumbuko. Wanastahili adhabu na ikiwezekana iwe adhabu kali.
Tujiulize. Je, hukumu inayoruhusu kifo ni adhabu? Je, kifo kinaweza kuwa adhabu? Je, adhabu hufanywa na aliyekufa? Kama sababu ya kuadhibu ni kutaka mtu ajirudi na kurejea katika utu wa jamii yake je, aliyeuawa anajirudi vipi, lini na wapi?
Hizi zinaonekana hoja ndogo kwa waliovimba vichwa na vifua, kwa hasira na uchungu wa kweli wa kupoteza watoto, ndugu, jamaa, rafiki au wenzao katika tabaka au kundi tambulishi kama walivyo albino.
Bali hasira zilizokaba koo za wafiwa; chuki zilizotunisha misuli ya shingo za ndugu wa aliyeuawa; na woga uliokumba nyoyo za wahusika; vyote vinaziba mifereji ya fikra kuhusu uhai wa mtu mwingine na nafasi ya muuaji mpya.
Vijana watatu wamepatikana na hatia ya kuua. Sheria inaruhusu wauaji kuuawa. Jaji, kwa mujibu wa sheria hajakosea kutamka hukumu hiyo kwa shabaha ya kulinda sheria na kazi yake. Bali Jaji aweza kuwa anaasi “shangazi wa mtima” wake.
Majaji wengi duniani wameeleza jinsi wanavyosutwa na dhamira zao pale wanapotamka hukumu ya kifo. Wameeleza jinsi kunavyokuwa na mapambano makali “rohoni” mwao na hatimaye kuanguka na kuwa mateka wa sheria na mfumo.
Leo kuna vijana watatu wa Kahama. Wanakabiliwa na mauti na siyo adhabu. Atakayeua vijana hao ni nani kama siyo muuaji?
Kuna tofauti gani kati ya aliyeua albino kwa panga na anayeua muuaji wa albino kwa kamba ya shingoni? Haipo. Wote ni wauaji. Mmoja anakanwa na sheria na mwingine anaruhusiwa na sheria. Wote wanatoa uhai wa watu wenye thamani ileile.
Ninaelewa ugumu wa wafiwa kuzingatia hoja hii haraka. Lakini malezi ya jamii hayawezi kwenda kwa misingi ya walioko madarakani kujipa fursa ya kuua na kujikinga na sheria walizotunga wenyewe.
Niliishawahi kuuliza katika safu hii wakati wa kujadili somo hilihili: “Kama serikali inaua, nani ataua serikali – ambayo sasa ni muuaji?” Sikupewa majibu.
Kuna haja ya kufikiri upya kuhusu sheria inayoruhusu kunyonga watu. Kunyonga ni kuangamiza maisha; siyo adhabu ya kurejesha mtu kwenye mstari wa maandili na utu wa wote.
Kunyonga ni kunyima aliyepatikana na hatia fursa ya mabadiliko katika maisha. Ni mabadiliko haya ambayo huweza kuwa mfano mkuu kwa jamii na kufanya watu wengi kukiri udhaifu wao na kuwa wanyoofu maishani.
Kuua hakuleti nafuu kwa mfiwa. Hakuna mafao kwa serikali. Hakuleti faida kwa jamii. Kunaendeleza vilio. Kunasimika hasira na chuki mpya. Kunafanya jamii ishindwe kuelewa nani anaweza kuikinga na ukatili huu.
Sheria zinazoruhusu mauaji kwa njia ya kunyonga ni za kuviziana; za kumalizana na mara nyingi, kama siyo mara zote, zinawaelemea wa tabaka la chini katika jamii. “Wakubwa” wana kila njia ya kuzipinda na hata kuzikatakata.
Sheria za kunyonga zinafanya jamii ianze kuona kuwa maisha hayana thamani. Zinafundisha usugu na kutothamini uhai binafsi na ule wa mtu mwingine. Zinazaa tabia ya “nitakuua hata kama wataniua.”
Sheria zinazoruhusu mauaji zinakomaza chuki na ghadhabu na zinafuta msamaha na tabia ya kujirudi ambayo ni nguzo kuu katika kupata suluhisho na muwafaka. Zinainyang’anya jamii ujasiri wa kufunza waliopogoka na kuikosesha jukumu la kufunza vizazi na vizazi.
Adhabu ilenge kurekebisha muhusika; kumfanya ajutie tendo lake na kutamani kurejea katika utu wake wa asili. Aliyekufa hajutii makosa yake; harekebiki pia.
Natamani kuona hukumu ya kifo ikifutwa na nafasi yake kwa sasa kichukuliwa na adhabu ya kifungo cha maisha. Aliyeua akiuawa, aliyeua muuaji anakuwa amekamilisha ukoo wa wauaji.
Katika ukoo huu, mauaji hayataisha. Hayataogopwa. Hayatapingwa kwa kuwa hayatachukiwa. Natamani yaishe. Jamii ivunje kimya.
0713 614872
ndimara@yahoo.com
(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili toleo la 26 Septemba 2009 chini ya safu ya SITAKI)
1 comment
Lakini mzee Ndimara, utakubaliana na mimi kuwa tawi bovu la mti sharti liondolewe, huwezi mzee NDIMARA leo ukaumia mguu na ukaoza ukasema msinikate huu mguu na wenyewe una thamani ya kuwepo.
Ndio, una thamani lakini ni hatarishi kwa afya yako. adhabu ya kifo haipitwi na wakati kabisa kwa wauaji hawa wa albino,Ni MUNGU tu ambaye kwake hakuna kosa kubwa wala dogo lakini kwetu sisi kuua albino au mtu yeyote ni kosa kubwa kabisa, kuwatisha watu wakati mwingine ni njia ya kuwaokoa na janga lililo mbele yao,wauaji wa albino heri na wao wafe kabisa kwani ni sheria inayowaua si hakimu.
KUWAUA ALBINO NI KAMA VITA DHIDI ASIYEPIGANA VITA na wakati huo huo kuwanyonga wauaji ni VITA DHIDI YA WAVAMIZI WA AMANI NA UTU ndani ya jamii.
kwa hiyo lazima wale uchungu wa thubutu yao ya kuua ndugu zetu maalbIno kwa hiyo mzee hawa wakatili WANYONGWE TU binadamu kitabia hubadilika-badilika huwezi sema eti tumpe fursa ya kubadilika kwa kumuweka jela miaka thelasini anarudi akiwa amezeeka. huyu muuaji ni mguu uliooza sharti ukatwe ndio maana hata wakoloni hawakuachwa eti watabadilika waliondoshwa tu JAPO SIKU HIZI WANARUDI KWA MTINDO MPYA, kwahiyo siungi mkono hoja Mzee Ndimara!
Post a Comment