Header Ads

LightBlog

NGUVU ZA UNAFIKI NA SIASA ZA NJIAPANDA



Yusuf Makamba: Mara joto, mara baridi…

Na Ndimara Tegambwage
SITAKI tabia ya Yusuf Makamba, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kuwa mara baridi, mara joto, mara vuguvugu na mara baridi, tena katika muda mfupi.

Kwa mbunge, mteule wa rais, kiongozi mkuu wa utendaji katika chama kinachopanga ikulu, kuwa na tabia ya kubadilika kila kukicha au pale kipenga kinapopulizwa; siyo ishara ya kuwa makini.

Joto lilipokuja – kwa msukumo wa chama au makundi au mtu binafsi – Makamba alifura kwa hasira na kutangaza ubabe. Alifanya hivyo baada ya vikao vya CCM vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu jijini Dodoma hivi karibuni.

Alimwakia spika Samuel Sitta na wajumbe wa chama chake kumkaripia, kumtishia, kumpa onyo na kutaka kumlegeza. Ni Makamba aliyesimama na kusema, “Kama siyo CCM, Samwel Sitta ahojiwe na nani?”

Ndani ya vikao vya CCM, Samwel Sitta alikuwa anakabiliwa na tuhuma nyingi zilizopelekwa kwa njia ya mjadala juu ya hali ya hewa ndani ya chama na serikali.

Kwamba spika amejitwisha jukumu lisilo lake la “kupambana na mafisadi.” Kwamba ana upendeleo – anatoa nafasi mara nyingi kwa wenye “kupinga serikali” na hata wapinzani, kuhutubia bunge kuliko wale wanaotetea chama na serikali.

Ofisa mdogo katika ofisi ya Makamba, John Chilligati, kwa ushirikiano na Makamba au kwa kutumwa na chama chake, aliwawakia wale ambao wanadaiwa kupewa muda mwingi na spika “kukemea ufisadi,” akihoji nani aliwapa wajibu huo.

Ikaja asubuhi, ikaja jioni, siku zikapita. Makamba yuleyule, wiki iliyopita, akaenda jimbo la Urambo, mkoani Tabora. Huko ndiko nyumbani kwa spika Samwel Sitta. Akachukua sura ileile ya kuumbika na kuumbuka.

Aliwaambia viongozi wa chama chake vikaoni na wananchi kwenye mkutano wa hadhara, kwamba CCM inatambua kuwa Spika Samwel Sitta anafanya “kazi yake vizuri” na hasa anafanya kazi ya chama.

Makamba wa leo siyo wa jana, wa kesho wala keshokutwa. Anaumbika na kuumbuka au kuumbuliwa. Anafura kwa hasira, lakini dakika chache zifuatazo, anatoa kicheko – cha kweli au cha unafiki.

Vyombo vya habari vimemnukuu Makamba akisema kuwa Sitta ni mbunge wao imara na kazi anayofanya bungeni ni kazi nzuri ya chama chake; na kuwataka wamuunge mkono hata katika uchaguzi ujao. Hata walokole hawafikii hatua hii.

Joto la ndani ya vikao vya CCM ndilo lilifanya Makamba awe mkali, jeuri na aongee kwa kujiamini. Wajumbe walioongea kwa kukandia Sitta, tena mbele ya mwenyekiti wa chama na rais wa Jamhuri, Jakaya Kikwete, huku wakipendekeza afukuzwe uanachama, ndio walikuwa msukumo wa Makamba.

Msukumo mwingine ulikuwa “Kamati ya Mwinyi” iliyoundwa rasmi kuchunguza “msuguano” kati na baina ya spika, bunge na serikali. Kamati iliundwa katika kikao cha Halmashauri Kuu.

Kwa maandalizi ya vikao hivyo vya Dodoma; kwa taarifa kwamba wajumbe kutoka Zanzibar walikuwa wameandaliwa rasmi kumkabili Sitta na hivyo ndivyo ilivyojitokeza; na kwa wingi wa wajumbe walioongea kutaka “Sitta amalizwe,” hakika Makamba asingekuwa na mtu wa kutembelea Urambo anayeitwa Samwel Sitta – spika.

Tabia ya Makamba ya kubadilika haraka – kutoka joto sana hadi baridi na huenda kesho atakuwa vuguvugu – huenda ndiyo inamfaa yeyote anayetaka kuwa katibu mkuu wa CCM ya sasa.

Akiombwa na kundi moja linalopingana na lingine kuwa aandae mazingira ya uhasama na mashambulizi, basi afanye hivyo. Akiambiwa sasa apoe, ananyamaza kama aliyekwenda safari.

Lakini akitekenywa kwamba amwakie fulani, kwa sababu zozote zile, atafanya hivyo. Vilevile akiambiwa kurejesha amani, atawaangukia aliokorofishana nao na kukumbuka walivyopeana pipi wakiwa darasa la pili.

Makamba anakuwa mkuu wa maabara isiyofuzu – CCM. Hawaamini kuwa waliishamaliza utafiti juu ya utengenezaji hewa ya oksijeni. Kwao utafiti ni utafiti tu usioisha hata kama waliishapata matokeo; ili mradi waonekana wako kazini, wanalipwa na wanatumiwa na waajiri wao.

Safari ya Makamba nyumbani kwa Sitta imekuja baada ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa kubanwa na wananchi na balozi za nchi za kigeni zilizoko Dar es Salaam, kuhusu vitisho alivyofanyiwa spika na nia mbaya ya kumdhoofisha.

Kama kwamba Rais Kikwete alijua kuwa hali hiyo ingedhoofisha uhusiano kati ya serikali yake na wananchi, asasi za kijamii zinazopigania haki za binadamu na hata nchi wahisani, akatafuta jinsi ya kulegeza msimamo kwa kutoa “maelezo ya nyongeza” kwa yale yaliyotolewa na Makamba na Chilligati.

Rais Kikwete alisema wiki iliyopita, katika kujibu “maswali ya wananchi ya papo kwa papo” katika televisheni kwamba, halmashauri kuu iliyokemea wabunge “wenye msimamo mkali,” ililenga tu kuleta nidhamu na siyo kuwatishia.

Alisema wabunge walikuwa wanatakiwa kujadili mambo ya chama chao ndani ya vikao vya chama na siyo hadharani; na kwamba kwa hatua hiyo, chama kamwe hakikulenga kuwanyamazisha.

Kama kauli ya Kikwete ilikuwa ndiyo kauli ya halmashauri kuu ya CCM, basi Makamba na Chilligati hawajui kuripoti na kuwasilisha taarifa za chama chao kwa wananchama, wananchi na dunia.

Lakini kama taarifa zao, na hasa Makamba, ziliwakilisha yaliyojiri ndani ya vikao vya chama chake; na kauli za Kikwete ni tofauti na zilizolenga kupoza wanachama na kurejesha “amani” ndani ya CCM, basi kuna mgogoro ndani ya chama hiki.

Bali kinacholeta nuru juu ya yaliyotendeka ndani ya vikao na iwapo yalilengwa; ni kwamba hakuna hatua yoyote waliyochukuliwa Makamba na Chilligati kwa kutoa taarifa tofauti na zile za chama na tofauti na kauli za mkuu wa kaya.

Dunia ya nje isiyotafiti wala kuchokonoa, yaweza kuamini kuwa aliyosema Kikwete ni sahihi na yale ya Makamba na Chilligati ni kauli binafsi au taarifa za chama zilizotiwa hamila. Kumbe sivyo.

Makamba ni mchekeshaji wa kweli. Aweza kutumika kwenye sherehe na kwenye misiba. Si yumo katika vikao vya kumsulubu Sitta? Leo kapewa ngwe ya kumpaka mafuta kwa mgongo wa chupa.

Hadithi zatufundisha: Lini sungura anakuwa rafiki wa simba? Ni pale tu simba anapokuwa ameshiba au anapokuwa na swala upandeni. Bali ni urafiki wa muda.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
(Makala hii haikuchapishwa katika toleo la Tanzania Daima Jumapili, 20 Septemba 2009 katika safu ya SITAKI kwa sababu ambazo mhariri aliniambia kwa simu kuwa ni "matatizo ya kiufundi.) Badala yake makala ilichapishwa katika gazeti la MwanaHALISI toleo la Jumatano 23 Septemba 2009).

1 comment

Sisulu said...

yeye ni mnafiki wa siku zote,yeye ni mtu anayeendeshwa na matukio badala ya ufikiri ndio maana huwa hana msimamo

Powered by Blogger.