Header Ads

LightBlog

UJANGILI ULIORUHUSIWA NA SERIKALI

Uwindaji wa leseni ni ‘ujangili’ pia
• Maliasili ya Tanzania, dunia itaisha

WAFUGAJI wanaofukuzwa kwenye makazi yao katika mbuga wana mengi ya kusema. Wengi hawana elimu ya darasani lakini ni wajuzi wa mazingira yao na wepesi wa kutambua mabadiliko. Hapa wanasema wanachoona ambacho serikali inaweza kufuatilia ili kuokoa maliasili wanyamapori.


Na Ndimara Tegambwage

WAMECHOMEWA makazi. Wakapigwa na wengine kuswekwa rumande kwa madai kuwa wamekaidi amri ya kuhama mbuga ambamo wameishi kwa miaka nendarudi. Lakini bado wana uchungu na nchi yao.

Wana uchungu na maliasili za Tanzania. Wanapendekeza kuwa uwindaji katika mbuga ungesimamishwa ili kuruhusu wanyamapori kuongezeka na kurejesha utajiri mkubwa wa taifa na dunia.

Wafugaji wa ng’ombe, mbuzi na kondoo ambao wameishi kwa kuingiliana sana na wanyamapori, wanasema serikali ingeweka sheria kali, kama hazipo, au kusimamia zilizopo ili kuokoa maisha ya wanyamapori.

“Sisi ndio walinzi wa wanyama hawa, usione wanatufukuza. Tungewabughudhi wasingekuwa hapa. Wala hatuwali. Sisi tunakula mifugo yetu. Lakini kwa mtindo wa sasa, wanyama watatoweka,” anaeleza mkazi wa kijiji cha Ololosokwan.

Kuna masimulizi mengi na marefu juu ya wanyamapori wanavyouawa kwa wingi. Mwanaume wa umri wa kati kijijini hapa anasema, “Kwa mfano, simba ni simba tu. Hawana mbadala. Kama simba watamalizika, hakuna tunachoweza kuona katika nafasi yake kiitwacho simba.”

“Tumeona mengi humu Loliondo. Hata wenzetu kutoka mbali wamekuja na kusimulia kuwa hali ni hiyohiyo. Wawindaji kutoka nje ya nchi wanaua hata watoto wa simba,” anaeleza.

Kijana wa umri upatao miaka 25 wa kijiji cha Magaiduru-Lorien anadakia na kusema, “Nimewahi kuona watalii wamebeba watoto wa simba na puma ndani ya gari lao.”

Kijana mwingine anaingilia kati, “Unasema simba tu? Mwaka jana wanamgambo wanaohudumia jumba la mfalme wa Umoja wa Nchi za Kiarabu (UAE) pale kilimani, walipita wakitangaza kuwa atakayepata chatu akiwa hai atalipwa shilingi milioni moja (1,000,000/=).”

Swali: Kwa hiyo na wewe uliingia vichakani kuwinda chatu?
Jibu: Hapana. Mimi nina shughuli zangu. Angalia ng’ombe wote hawa (kama 1,200).
Swali: Si ungemwambia mdogo wako akachangamkia hilo?
Jibu: Tuliacha wengine wanaohitaji fedha za haraka watafute.
Swali: Sasa chatu alipatikana?
Jibu: Alipatikana. Tulisikia walipatikana sita, wakubwa kwa wadogo. Waliwachukua wakiwa hai.
Swali: Kwani wewe umewahi kuona wanyama wakisafirishwa wakiwa hai?
Jibu: Si unaona uwanja wa ndege ule pale (ndani ya Loliondo)? Madege makubwa yanatua hapo hata yenye uwezo wa kubeba magari makubwa. Nendeni ukaulize maeneo yale utapewa taarifa. Hata simba na chui wachanga wanasemekana kuchukuliwa…lakini usinifanye shahidi wako.

Ni madai makubwa na mazito. Yanahitaji kuthibitishwa. Wafugaji wanasema walichoona. Huenda wanyama wanaodaiwa kuchukuliwa kutoka mbugani wakiwa hai ndio tunawakuta katika “hifadhi za wanyama” mijini (mazuu) katika baadhi ya nchi za nje.

Maelezo ya aina hii yanafanya wafugaji wakazi wa mbuga za Loliondo wachukiwe na watu kutoka nje ambao walipewa mbuga kufanyia biashara ya utalii na bila shaka baadhi ya maofisa wa maliasili wanaoshirikiana nao.

Mbuga za Loliondo ziko chini ya kampuni ya Ortelo Business Corporation (OBC) ya Umoja wa Falme za Kiarabu ambayo imekuwa ikiendesha biashara ya utalii wa uwindaji wanyama na upigaji picha kwa karibu miaka 17 sasa.

Wafugaji wanachukiwa kwa kuwa “wanasema uongo.” Kusema uongo, katika hali hii ni kusema ulichoona; kwamba wanaoitwa watalii wanafanya zaidi ya kile walichotarajiwa kufanya.

Kuna masimulizi kuwa “watalii” – ambao wananchi hapa wanapenda kuwaita “majangili wenye leseni” – wanaua hata wanyamapori ambao hawapo kwenye orodha ya kuwindwa na kuchukua hata wanyama hai.

“Uwongo” wa aina hii ni aghali. Vijana wengi wanasema wakijulikana kuwa wametoa taarifa kwa watu wa nje, huenda wakakamatwa na “kuwekwa ndani.”

“Kweli, mfano tukijulikana kuwa tuliongea nanyi kuhusu mambo haya, wanaweza kutupoteza au kututupa rumande kwa muda mrefu mpaka tukakuta mifugo yetu yote (ng’ombe 210, mbuzi 90 na kondoo 45) vimeibwa,” anaeleza kijana akitupa macho huku na kule.

“Sisi tunawajua wanyamapori. Wakiongezeka tunajua; wakipungua tunajua,” anasema Mzee Ngirimba mwenye umri wa miaka 59 kutoka kijiji cha Arash ambaye alikutwa Ololosokwan.

Bali kama ambavyo hakuna mbadala wa simba, vivyo hivyo hakuna mbadala wa swala, tembo wala digidigi.

Kwa mfano, taarifa kuhusu idadi ya wanyamapori zinaeleza kuwa swala-twiga wamepungua sana katika mbuga nyingi nchini. Tandala wadogo na tandala wakubwa – wote wamepungua kwa kiasi kikubwa.

Wanyama wengine ambao wakazi wa mbugani na baadhi ya maofisa wanyamapori wanakiri wamepungua ni digidigi wadogo ambao hutembea wawili-wawili na palahala.

Lakini wazee sita waliohojiwa juu ya wingi wa simba katika maeneo yao, walisema hata simba, chui, duma na mbwamwitu wamepungua.

“Hatuna elimu juu ya taratibu za wanyamapori na uwindaji, lakini tunajua kuwa siyo wanyama wote wanaowindwa. Lakini huku kwetu huwa tunaona wanapiga tu kila mnyama,” ameeleza mmoja wa wazee wa Olorien.

“Kwa mfano tumeona walioua twiga na siku zote tunaambiwa kuwa twiga siyo mnyama wa kuwinda,” anaeleza.

Anasema amesikia kuwa hata simba, duma na chui hawastahili kuwindwa lakini wameona wawindaji wa kitalii wakiburuta mizoga ya wanyama hao.

Masimulizi juu ya uwindaji shelabela – unaoua wanyama wakubwa na “watoto wao;” ukamataji wanyama hai na usafirishaji wake nchi za nje, ni mambo ambayo wafugaji katika mbuga wanasimulia kwa uwazi.

Wauaji wakuu wa maliasili wanyamapori ni wale wenye leseni za kuwinda. Wanadaiwa kuua wanyama wengi kuliko idadi ya waliopangiwa na wanaua hata wale wasio kwenye orodha ya kuwindwa, wenye mimba na wachanga.

Wawindaji wa aina hii basi, hata kama wana leseni, ni wahujumu ambao tunaweza kukubaliana na wananchi wa eneo hili wanaowaita “majangili wenye leseni.”

Uwindaji wa aina hii unateketeza wanyamapori; unaua vizazi vya maliasili hii adimu duniani. Walinzi wa mbuga na wanyama waliomo wana mapendekezo, kama anavyosema mmojawao katikamahojiano:

Swali: Kwa hiyo unaona afadhali utalii wa kuwinda wanyamapori upigwe marufuku?
Jibu: Wewe! Nani atakubali hilo? Hawa wazungu na waarabu wanaokuja wanataka kujiburudisha na serikali yetu inataka fedha. Unadhani nani atakubali hilo?
Swali: Kwa hiyo waendelee kuwinda?
Jibu: Hapana. Sisi tunaona wakisimamisha uwindaji kwa miaka kumi (10) wanyama watazaana na kuongezeka. Kuanzia hapo uwekwe utaratibu wa kuzuia kuangamiza wanyamapori.
Swali: Unadhani uuaji wanyama bila kujali nani ana mimba, nani ana umri mdogo na nani hastahili kuwindwa unatokana na nini?
Jibu: Sisi hayo hatuyajui. Hatuna majibu. Tunaona ni ukatili tu. Labda pia hawana mtu wa kuwaongoza ili kuwaambia ‘huyu msiue.’ Lakini tunaambiwa kuna masharti wanayopewa kabla ya kuingia kwenye mbuga kuwinda.
Swali: Na hili la kubeba wanyamya hai?
Jibu: Kwanza hilo hatukulikubali haraka. Tulidhani vijana wanasema hovyo. Jinsi siku zinavyokwenda ndipo tukapata ukweli. Inaonekana hakuna usimamizi. Hilo halipo hapa Loliondo peke yake. Tunasikia hata Serengeti katika eneo la Gumeti (Grumet).

Mzee huyu anasema hawajui iwapo wawindaji wa kitalii wanaruhusiwa kubeba nyama na kupeleka kwao

Wafugaji ndio wamekuwa walinzi wa mbuga. Wanyama wote waliomo wamekusanyika, kuzaana na kuishi bila bughudha kwa kuwa wafugaji hawakuwawinda.

Dunia nzima inayokusanyika katika mbuga za Tanzania inakuja kushuhudia, bahati mbaya bila kujua, utashi, ujasiri na mapenzi ya wafugaji kwa wanyamapori. Bali leo hii wafugaji na mifugo yao wanaswagwa nje ya makazi yao na mali zao kuharibiwa.

Laiti wanyama wangekuwa na uwezo wa kutambua kuwa marafiki wao wa karibu, wa miaka mingi, wanatendewa ukatili. Wangepinga kwa maandamano na kauli kali.

Tetesi hizi ni muhimu kwa serikali na dunia nzima. Wanaopenda wanyama na mapato kutokana na wanyamapori, sharti wachukue baadhi ya hatua zifuatazo:

Kwanza, kufanya uchunguzi juu ya madai ya walinzi wa miaka mingi wa wanyamapori. Hawa ni wafugaji ambao wamekuwa karibu na wanyama kiasi cha kujua hata tabia zao.

Pili, uchunguzi uongoze katika kuchukua hatua madhubuti za kusimamisha uwindaji wa kiharamia katika mbuga zote nchini. Hii ni kuzuia uteketezaji maliasili ya dunia.

Hatua hizi zitazuia pia ukamataji na usafirishaji wanyama hai nchi za nje, kama utakuwa umegundulika na kuthibitika; na au kusitisha uwindaji kwa kipindi kirefu ili kuruhusu wanyamapori kuongezeka.

Tatu, kuangalia jinsi ya kusimamisha uwindaji wa aina fulani ya wanyamapori na kuweka usimamizi wa kutosha wa mamlaka ya wanyamapori katika hatua zote za uwindaji.

Nne, kubadili masharti ya miliki au ukodishaji wa mbuga ili kuondoa ukiritimba wa wamilikishwaji au wenye leseni.

Wamiliki au wenye leseni za kukodi wanapokuwa na mamlaka kama yale ya nchi, waweza kufanya wapendalo ikiwa ni pamoja na kuua kishelabela na hata kuhamishia wanyama nchi za nje.

Tano, kuacha kuchoma makazi ya wafugaji na kusitisha hatua za sasa za kuwafukuza, wao na mifugo yao, kutoka kwenye mbuga. Badala yake watengewe maeneo ya kilimo na mifugo pale walipo.

Mashamba madogo ya mahindi ya wafugaji, chini ya kilima ambacho kilele chake ndiko liliko “kasri” la mfalme wa UAE, yanaonyesha mabadiliko muwafaka katika maisha ya wafugaji.

Wafugaji hawa, wanaoanza kuwa wakulima pia, wanaendelea kuwa walinzi wa wanyamapori na chanzo cha taarifa muhimu za kunusuru maliasili ya Tanzania na dunia. Huu nao ni ulinzi wa aina yake. Serikali yaweza kuanzia hapa.

Wako wapi akina Luteni mstaafu, mfugaji na mkulima, Lepillal ole Molloimet, ili wajiunge na jumuia ya kimataifa katika kusemea wasio na sauti na kupigania maliasili za taifa na dunia?

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

(MAKALA HII ILICHAPISHWA KATIKA GAZETI LA MwanaHALISI TOLEO LA 19 AGOSTI 2009)

1 comment

Mzee wa Changamoto said...

Heshima kwako Mzee Tegambwage.
Haya yasemwayo na yatendekayo ni ya kusikitisha saana.
Sina hakika na muelekeo wa nchi yetu iwapo inashindwa kusimamia rasilimali zetu kiasi hiki. Lakini ni machache ya kushangaa hapa kwani hii ndio TANZANIA YANGU. Ambayo kwake KINGA ni msamiati usiofikika wala kutimilika. Ambayo inapenda kuvuna isipopanda na ambayo inaonekana kufanya mambo kinyume. Kuweka mipango mikubwa ya KUENDELEZA UTALII ilhali unauza viwaletavyo watalii ndiko nilikokuandika kama KUUZA BAISKELI ILI KUNUNUA KENGELE.
Hakuna tunakoonekana kuboresha kwa manufaa ya wananchi. Ni sera za kubishana kwenye udini na mengine yasiyo na maana ilhali wananchi na rasilimali zateketea na kutoweka.
Inasikitisha saana na twashukuru kwa kuendelea KUCHAMBUA haya na mengine mengi. Ipo siku TAIFA LITAAMKA na natumai hatutakuwa tumechelewa sana.
http://changamotoyetu.blogspot.com/search/label/Tanzania%20yangu

Powered by Blogger.