WATU NA MIFUGO YAO WATAKUFA
SERIKALI IMEKWENDA WAPI LOLIONDO?
Na Ndimara Tegambwage
SITAKI kuambiwa kuwa kuna serikali. Haipo. Kama ipo imelala, tena usingizi wa pono? Imezimia? Waliolala hawaamki? Waliozimia hawazinduki? Haipo!
Wafugaji wilayani Ngorongoro wanasema, tena kwa sauti kubwa kuwa kuna ukame. Kuwa mifugo yao – ng’ombe, mbuzi na kondoo haina chakula. Hakuna malisho. Hakuna maji. Mifugo inakufa. Serikali haipo.
Mwandishi kutoka Loliondo anapaza sauti, kwa simulizi na takwimu: Hakuna maji. Hakuna nyasi. Mifugo inakufa. Ng’ombe sasa anauzwa kwa Sh. 2,000 hadi 20,000. Serikali kimya.
Mfugaji anapaza sauti. Anadhani serikali haijasikia. Anasema maji yapo; wamekuwa wakiyatumia. Lakini maeneo yenye maji yamefungiwa kwenye mipaka ya vitalu vya uwindaji ambavyo serikali imegawa kwa watu wa nje – “wawekezwaji” – wale waliowekezwa badala ya kuwekeza. Serikali tebilimu!
Kuna vilio, kwamba ng’ombe wawili wameuzwa kwa debe moja la mahindi. Kwamba bei ya debe la mahindi ni kati ya Sh. 8,000 na 10,000/=. Kwamba lazima ng’ombe auzwe haraka, hata kama ni kwa hasara, kabla hajafa. Serikali haipo.
Sikilizeni sauti zao, hao wafugaji. Kwangu ng’ombe wamekufa watano. Kwangu wamekufa 20. Kwangu wamekufa 50. Elias Kagili wa kitongoji cha Kirtalo anasema: Kwangu wamekufa 100. Ni hatari tupu. Vifo. Vifo. Mwandishi kaona. Kasikiliza waathirika. Kaona na kupiga picha za mizoga. Serikali haipo.
Sikilizeni kilio cha Ole Taki Saile wa kitongoji cha Ilichooroi. Ng’ombe wake 60 wamekufa. Wengine walio karibu kuwa taabani kawauza kwa bei ya kati ya Sh. 2,000 na 5,000. Naye Lekaneti Shekuti wa kitongoji cha Sekunya anasema karibu kila siku wanakufa ng’ombe wake 10. Serikali kimya.
Kauli ya Shekuti hii hapa. “Maji yapo pale. Nyasi zipo pale, lakini ng’ombe wetu wanakufa. Kampuni ya Thomson Safari inatuzuia kunywesha mifugo yetu pale,” anaonyesha sehemu husika kwa fimbo.
Maji yako Ngorika – mwekezwaji hataki. Maji yako Polelete; mwekezwaji hataki. Maji yako Sukenya, mwekezwaji hataki. Maji yako Olkimbai, mwekezwaji hataki. Maji yako Walaasaye, nako mwekezwaji hataki yanywewe. Kote huko ni visima na vijito vilivyoko katika ardhi waliyopewa wawekezwaji ili wafanyie “utalii wa uwindaji,” au ujangili ulioruhusiwa kisheria, ndani ya nchi ya wafugaji wanaotaabika.
Teremka kijitoni au kisimani wakukute; utakiona cha moto. Sukuma mifugo yako kijitoni na wakukute; ndipo utajuta kwa nini ulizaliwa. Huu ndio ukatili unaosababisha vifo vya mifugo. Serikali haipo.
Katika mazingira ya Ngorongoro na Loliondo, vifo vya ng’ombe, mbuzi na kondoo maana yake ni vifo vya watu. Wanaohangaika kutafuta chakula na maji kwa ajili ya mifugo, wao hawana chakula. Ni mizoga inayotembea; inahangaikia mifugo yake. Siku moja itadondoka njiani. Serikali tebilimu!
Serikali imetoa ardhi ya wananchi kwa makampuni kutoka nchi za nje, iwe sehemu ya kuwindia kwa ajili ya kujifurahisha. Katika mazingira ya sasa, nyasi na maji vinapatikana katika maeneo ambako wawekezwaji hawaruhusu mifugo kuingia.
Hata hivyo, kuanzia Aprili mwaka huu, nyumba na maboma ya wafugaji yamekuwa yakichomwa moto kwa nia ya kuwafukuza wafugaji kutoka makazi yao ili wawindaji wa wanyamapori wapate kustarehe. Ni starehe ya wawekezwaji na adha kwa wananchi.
Ni ukatili. Ni unyama usiomithilika. Haustahili kusimamiwa au kuvumiliwa na wanaojigamba asubuhi, mchana na jioni kuwa wao ni walinda haki na watetezi wa demokrasi na haki za binadamu. Haiwezekani. Ni kwa kuwa serikali haipo. Serikali tebilimu!
Kama serikali ipo inasubiri nini? Inasubiri mifugo ife na kumalizika? Ili iweje? Ili wafugaji wawe masikini? Ili wawe ombaomba? Au ili wafe kama mifugo yao, huku wawekezwaji kutoka nje wakimeremeta; wakitweta kwa shibe na kunenepeana kwa faida na ziada ya uwindaji Loliondo?
Wawekezaji hutegemewa kuleta fedha. Wawekezaji hutegemewa kuongeza ajira. Je, wawekezwaji wanaleta nini kama siyo adha; wanaongeza shida na dhiki. Wanasababisha roho mbaya. Wanafungia maji na nyasi “kabatini;” ili mifugo ife; ili wenye mifugo wafe au wahame.
Sitaki kuamini kuwa kuna serikali. Ipo? Inamlinda nani? Inalinda wawekezwaji ili watanue, huku ng’ombe wa wafugaji wakifa? Huku mbuzi na kondoo wanakufa? Huku wafugaji wakisubiri kufa pia?
Kungekuwa na serikali ingeona mahangaiko ya wafugaji wa Kimaasai. Tuseme ipo lakini haioni? Ingekuwepo ingesikia kilio cha wafugaji, waandishi wa habari, wanaharakati na wafanyabiashara wanaonunua ng’ombe mmoja kwa Sh. 2,000. Tuseme haina masikio au yameziba?
Kungekuwa na serikali, kwa maana ya watawala, ingekumbuka kuwa iliapa kutumikia watu, kuwalinda na kuwatendea haki; na iliapa kwa Mungu kuwa aisaidie kuyatenda kwa ukamilifu. Tuseme imesahau kiapo? Au wafugaji na maeneo yao siyo sehemu ya Tanzania? Au kiapo kimelainika? Nani amelainisha kiapo cha serikali?
Hata kama mambo haya yangekuwa yanatendeka Nigeria au Kongo; huwezi kukaa kimya juu ya unyama wanaotendewa binadamu wa Ngorongoro. Risasi za moto zinatafuta nini katika makazi ya Wamaasai na mifugo yao?
Alikuwa Desmond Tutu aliyesema, “Ukiona mguu mnene wa tembo umekanyaga mkia wa panya, na ukaangalia pembeni na kusema hayakuhusu na wewe huna upande; panya hataelewa msimamo wako wa kutokuwa na upande katika ukatili huu.”
Kuna kila sababu ya kuwa na upande katika kutetea haki. Na haki ya wananchi kuishi kwao na kufurahia matunda ya ardhi yao, haiwezi kupitwa na ujanjaujanja wa wawekezwaji hata kama wanamwaga mabilioni ya shilingi kwa yeyote yule.
0713 614872
ndimara@yahoo.com
(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, toleo la tarehe 11 Oktoba 2009 chini ya safu ya SITAKI)
No comments
Post a Comment