Header Ads

LightBlog

TUNAFIKIRI VIZURI NA KWA WEPESI KATIKA LUGHA TUNAYOJUA VIZURI ZAIDI



Serikali inavyoua lugha za asili Tanzania
•Sera zake zina sura ya ‘ndumia kuwili’

Na Ndimara Tegambwage

SERIKALI ina tabia ya “ndumila kuwili” kuhusu nafasi ya lugha za asili. Inaonekana ina utashi wa kuua lugha hizo kwa madai ya kukuza Kiswahili.

Katika Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997 serikali inasema, “Jamii zetu zitaendelea kutumia na kujivunia lugha zake za asili kwa kuwa ndio hazina kuu ya utamaduni na maarifa.”

Lakini katika Sera ya Habari ya mwaka 2003, serikali hiyohiyo inasema, “Lugha zitakazotumiwa na vyombo vya habari hapa nchini ni Kiswahili na Kiingereza.”

Katika sera moja serikali inatambua kuwepo utamaduni na maarifa katika lugha za asili; katika sera nyingine serikali inasema hizo lugha zilizosheheni maarifa, zisitumiwe kwenye vyombo vya habari.

Huu ni mpango wa kunyonga lugha za asili kwa kuzinyima pumzi – zisijitokeza kwenye vyombo vya kisasa vya mawasiliano mapana na hivyo kuteketeza hazina kuu ya utamaduni na maarifa.

Utamaduni na maarifa ni mazao ya akili. Ni matunda ya watu wanaofikiri na kutenda. Kinachoitwa hazina ya utamaduni ni mkusanyiko wa fikra na matendo ya watu katika jamii; katika kipindi maalum cha maisha yao.

Katika maana yake halisi, maarifa ni sehemu ya utamaduni pale tunapoainisha utamaduni kuwa ujumla wa maisha ya watu na mazingira yao katika jamii husika.

Sasa kwa nini maisha ya watu wengi, walioko katika mila, desturi na maarifa yao, yawekwe kando katika matumizi ya vyombo vya habari?

Huu ni ubaguzi wa aina yake, wenye sura ya unyanyapaa kwa mamilioni ya watu wasiozungumza Kiswahili wala Kiingereza.

Kuzuia matumizi ya lugha za asili kwenye mikutano na katika vyombo vya habari, ni ubaguzi wenye madhara yafuatayo:

Kwanza, ni kutaka kuua lugha husika. Ni kuua utamaduni na maarifa yaliyomo ambayo yalipatikana na yanaendelea kupatikana kupitia lugha hizo.

Maarifa hayo, ama yanaendelea kuundwa, yapo na yalikuwa hayajafahamika kwa mapana na, au hayakuwa yamesambazwa wala kuhifadhiwa katika lugha nyingine.

Pili, kunyang’anya wanaotumia lugha za asili uwezo wa kuelewa, kubaini na kushiriki maongezi na mijadala inayowahusu.

Tatu, kupandikiza utatanishi, woga na kutojiamini miongoni mwa wanaotumia lugha za asili. Hali hii inaletwa na shinikizo la kila mmoja kutumia lugha ya shuruti.

Nne, kuondoa mfumo na mtiririko wa kufikiri ambao watumiaji wa lugha za asili walikuwa wamezoea.

Tano, kupunguza, kuzuia au kufuta kabisa, mawasiliano mapana, kwa njia ya lugha na vitendo na hivyo kudumaza au kufisha maarifa katika jamii husika kwa kupunguza au kuondoa uwezo wa kuzalisha mawazo mapya.

Sita, kupunguza wepesi wa kufikiri na kuelewa na kuondoa mshikamano wa jamii zinazotumia lugha za asili.

Saba, kuvunja haki za binadamu kwa kuingilia, kutibua, kudhibiti, kukandamiza na kuzima lugha za asili – ambazo ni chombo cha fikra na maarifa kwa jamii husika.

Uvujaji huu wa haki za binadamu umechukua sura ya kuhujumu:

Kwanza, uhuru wa “kuwa wewe” na kuwa sehemu ya jamii yako kwanza kabla ya kuwa sehemu ya jamii pana.

Pili, uhuru wa kufikiri; tena kufikiri kwa wepesi na mtiririko. Tatu, uhuru wa kuwa na mawazo na kutoa na kupokea mawazo ya wengine. Nne, uhuru wa kutofautiana na mwenzako au yeyote; hata kama ni mtawala. Tano, uhuru wa kurithishana utamaduni na maarifa.

Lakini watawala, ambao pia ni watunga sera zinazogongana, wamekuwa wakidai kuwa lugha za asili zinawagawa Watanzania. Wanataka Kiswahili na Kiingereza tu.

Inabidi uwe mwendawazimu wa kiwango fulani ili uweze kuwasomea Wasukuma au Wamasai, wasiojua Kiswahili au Kiingereza, taarifa za habari za vijijini mwao, taifa au za kimataifa na kudai kuwa kwa njia hiyo unaunganisha taifa!
Nimepata fursa ya kuhudhuria warsha ya 10 ya Mradi wa Lugha za Tanzania (19 -20 Juni 2009), juu ya “Nafasi ya lugha za asili katika jamii ya Tanzania,” ukumbi wa hoteli ya Beachcomber nje ya jijini la Dar es Salaam.

Wachunguzi walikuwa wakionyesha, pamoja na mambo mengine, kazi walizochapisha juu ya lugha za watu wa jamii mbalimbali na kudhihirisha kuwa lugha ya kwanza kwa wananchi wengi, siyo Kiswahili.

Hoja hii inakuja kufuatia matokeo ya tafiti nyingi duniani kuwa watoto wakifundishwa katika lugha yao ya kwanza ambayo walimu wao wanaijua vema, angalau kwa madarasa ya awali, hupata uwezo wa kuelewa haraka na hata kupata msingi wa kushika lugha na masomo mengine.

Kama ada, takwimu za aina hiyo lazima zilete mgongano kati ya watetetezi wa lugha za asili na wale wanaopenda Kiswahili na Kiingereza hata kwa mgongo wa kifo cha lugha za asili.

Kuna wasomi waliosema lugha za asili hazina maana na kwamba hakuna maarifa yoyote ya kuchota kutoka kwa watumiaji wa lugha hizo (!)

Pamoja na kwamba wenye kutumia lugha za asili ni wengi na bado wanafikiri na kutenda katika lugha hizo kuliko Kiswahili na Kiingereza; kuna waliosema lugha hizo zimepitwa na wakati; zinyofolewe baadhi ya misamiati na istilahi na kuachwa zife.

Bali hoja kuu inabaki bila kujibiwa: Mbona kuna kasi, mabavu ya sera za serikali na mpogoko wa hoja za baadhi ya wasomi katika kuhujumu lugha za asili?

Tatizo basi siyo kwamba lugha za asili zinawagawa Watanzania. Tatizo ni kwamba wananchi wakiendelea kuwasiliana katika lugha zao, ambamo wanaelewana vizuri na kutenda kwa muwafaka, yafuatayo yatadhihiri:

Kwanza, watafikiri, tena kwa wepesi na kuelewana vizuri. Pili, wataungana zaidi na kuwa na mshikamano zaidi. Tatu, watasimamia utashi na kauli zao na hata kuvunja mikatale iliyowafunga miaka nendarudi.

Kwa msingi huu, malalamiko ya watawala kuwa lugha za asili zinagawa wananchi, na kuchochea ukabila, yanalenga kuhujumu uwezo huo wa kufikiri na kutenda kwa uhuru.

Suala la ukabila bado limo katika vichwa vya wasomi wengi wenye vyeti vya hadhi ya juu katika taaluma mbalimbali. Huu nao ni msiba. Bado kuna wanaofikiri kuwa kuongea Luhaya au lugha yoyote ile ya asili, ni kuwa na ukabila.

Hawa hawajui au wamesahahu au wanakataa kukubali kuwa mtu anafikiri haraka katika lugha yake ya karibu zaidi; mifano yake inakuja haraka kupitia lugha hiyo; anakuwa mwepesi kuwasilisha na kutoa majibu katika lugha yake na hasa anapokuwa anaongea na wanaofahamu lugha yake.

Hata baadhi ya wasomi vyuoni bado wana matatizo na Kiswahili na Kiingereza. Sharti wafikiri kwanza, kwa mfano kwa Luhaya, ndipo waweke kwenye Kiswahili na baadaye watoe sauti kwa Kiingereza.

Watu hufikiri vizuri na kwa usahihi zaidi katika lugha zao na hii ni haki yao kama walivyo na haki ya kuishi. Bali watawala na wengine waliomezwa na mkengeuko wameng’ang’ania dhana dhaifu kuwa lugha za asili zinaligawa taifa.

Je, tumekuwa na makabila au nchi au mataifa madogo? Twende Bukoba. Tarehe 8 Julai 1931, Omwami Rwagugira alikabidhiwa nishani aliyopewa na King George wa Uingereza (usijali sababu).

Katika hotuba yake ya kukabidhi nishani, Bwana PC (mtawala wa jimbo – Provincial Commissioner) alisema, “Mwami Rwamugira amepewa nishani kwa uhodari wake na kazi alizofanya toka sisi tumeingia katika nchi hii ya Bukoba…”

Tarehe 28 Mei 1933, Omukama wa Ihangiro alikaribisha masultani kutoka Dar es Salaam kwa kusema, “…Sina budi kutoa shukrani kwa watemi hawa waliofika katika mji wangu wa Rubungo na nchi yangu ya Ihangiro…” (Kutoka:Kitabu ya barua kakobi, 1931).

Kwa ufupi, hapa kulikuwa na watu. Wana utawala wao na lugha yao katika taifa lao. Waliongea, kufikiri na kutenda katika lugha yao.

Wageni, kama Bw. PC na masultani walipata wakalimani na kumbukumbu ziliwekwa; tofauti kabisa na ubwege wa sasa ambako mzungu mmoja anafanya warsha ya wananchi 60 kuendeshwa kwa lugha ya Kiingereza.

Kauli hizi za Bakama kuhusu “nchi zao” hazikuja na ukoloni wa Uingereza. Wakoloni walizikuta na hali yake halisi. Kumbuka hiyo ni miaka 47 tangu Afrika ikatwe vipande kama keki ya harusi (1884).

Historia imejaa kumbukumbu, siyo tu za Tanganyika, ambako walitangulia Wajerumani na kabla ya hapo Waarabu, bali Afrika nzima inaonyesha kuwepo kwa tawala imara, zikiwa mataifa kamili, hata kama hazikuwa na silaha kama za wavamizi.

Vita vya kupambana na wavamizi Afrika viliendeshwa na viongozi wa mataifa ya Afrika yaliyokuwa yameimarika katika tawala zake. Ujio wa teknolojia mpya hauondoi ukweli wa utaifa.

Historia imejaa orodha ya watawala na viongozi wa vita walionyongwa au waliojiua kuliko kuchukuliwa mateka na wavamizi. Mapambano yote hayo yaliendeshwa katika lugha za asili zilizolingana na maendeleo ya teknolojia ya wakati huo.

Kitu kikubwa kiliwashinda wavamizi wote katika historia. Walishindwa kuua lugha walizozikuta. Ukinzani kati ya makundi mawili ya “kigaidi” – wamisionari na wakoloni – ulizaa mbegu moja ambayo haikuwa imekusudiwa.

Wamisionari walishikilia baadhi ya lugha za asili na kuandika na kutafsiri vitabu vya dini katika lugha za wenyeji.

Hawa walijua “neno halitapenya” kwa lugha ya mbali. Halitazungumzwa baada ya mahubiri. Halitakaa moyoni kama halina mfano wa karibu. Halitakumbukwa kama halikuwekwa katika mvumo unaoeleweka na uliozoeleka.

Kama kuna kitu kimoja tunachoweza kujivunia kwa kushinda uvamizi uliofanywa Afrika, ni kubakiwa na lugha za asili zilizosheheni maarifa ya jamii mbalimbali.

Ndani yake kumefunikwa upendo na mshikamano wa jamii; chuki na hasira dhidi ya wavamizi; mbinu za kujikinga na kuendelea kuishi; ujasiri wa kukabiliana na adui; hekima ya kufanyia maamuzi; maarifa ya kuendeleza jamii na fursa za kuingizia maarifa mapya.

Kwa hiyo, hapa kulikuwa na tawala, siyo makabila wala vikabila. Kulikuwa na lugha za mataifa zilizohudumia jamii anuwai katika kila nyanja.

Ndani ya kitabu cha nyimbo za Luhaya za Kanisa la Kilutheri cha hadi miaka ya 1950 kulikuwa na wimbo uliotungwa kwa msingi wa kizalendo na kwa mantiki zote ulikuwa wimbo wa taifa:

Mukama Katonda linda
Eihanga lya Buhaya
Abantu n’eitunga lyamwo
Ensi ogihe omugisha
Linda amaju n’ebibanja
Endimilo ozezege
Nabo abantu bakusiime
Bakuhulile wenka


Tafsiri ya karibu ni:
Ee Baba Muumba
Dumisha taifa la Buhaya
Watu na mali zao
Nchi uipe neema
Linda kaya na mashamba
Mavuno yawe teletele
Ndipo watu wakuhimidi
Na kukutii wewe tu


Kanisa lilitambua utaifa wa mataifa mengi lakini katika lugha zao. Angalia jinsi ubeti wa wimbo uleule ulivyobadilishwa kukidhi maendeleo ya kisiasa (chapisho jipya):

Mukama Katonda linda
Ensi ya Tanzania
Naichwe abantu otulinde
Ensi ogihe omugisha
Kandi abemiluka yoona
Obahe obwesigwa
Singa waitu otubele
Chwena tukuhulile

(Kutoka: Empoya, Northwestern Publishers, 1992)

Tafsiri ya karibu:
Ee Baba Muumba
Dumisha taifa la Tanzania
Nasi watu utukinge
Nchi uipe neema
Na wote wenye majukumu
Uwape uadilifu
Eee Mungu utuwezeshe
Sote tukutii wewe


Pamoja na mabadiliko kutoka taifa la Buhaya kwenda taifa la Tanzania, bado nafasi ya lugha ya asili ni muhimu kuelezea kilichotokea ili kieleweke vema kwa wengi, kijadiliwe, kizame na watumiaji wa lugha hiyo waweze kufuatilia na kupima mabadiliko.

Hivyo, kuzima lugha za asili kunalenga kuweka kando wananchi waliopevuka ndani ya lugha zao na kufanya jamii zenye uelewa mpana kupitia lugha za asili, kuwa kama misukule ya kuswagwa bila utashi.

Kuhujumu lugha za asili ni kueneza ujinga. Watu hawatajua jinsi serikali ilivyoshindwa kutekeleza ahadi zake za kuondoa ujinga, umasikini, rushwa, magendo na ufisadi. Hivyo hawatachukua hatua.

Kwani watawala wana tabia ya kupakata umasikini na ujinga. Umasikini hufanya wengi kubaki hohehahe, tegemezi na hata ombaomba.

Ujinga hufanya wasijue na hasa mara hii wanapokuwa wanaelezwa kwa lugha ngeni, ngumu ambazo hawajui vema au hawajui kabisa na hawawezi kuzitumia kung’amua kinachoendelea. Kwa hiyo, ujinga na umasikini ni mtaji na ngao kuu za watawala.

Kwa upande mwingine, matumizi ya lugha za asili katika vyombo vya habari yangewezesha jamii pana kuelewa kinachojadiliwa; kuchangia na kukuza hoja na hata kuunga mkono au kukataa hoja.

Nani atashindwa kufarijika kwa kuona wenye ujuzi wa lugha za asili wakiajiriwa katika vyombo vya habari na serikali ikijitahidi kujua kilichomo kwa kuajiri wakalimani. Ajira.
Mbona umoja wa watu wenye lugha anuai na wanaoelewa umuhimu na shabaha yao, unaweza kuwa imara kuliko umoja wa kushinikiza kupitia lugha moja au na nyingine ya kigeni?

Bado Kiswahili kinaweza kuendelea kutumika na kukuzwa, kama kuna juhudi za kufanya hivyo. Bali kuwepo kwa lugha za asili, nyingi kama zilivyo, siyo tishio, ni fursa.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
(Makala hii itachapishwa katika gazeti la MwanaHALISI,toleo la Jumatano, 1 Julai 2009)

1 comment

Mzee wa Changamoto said...

Heshima kwako Ta Ndimara.
Kuna mengi nimejifunza ya kihistoria na naamini wahusika wanasikia. Lakini tuna tatizo kubwa ambalo laonesha kuwaathiri hata viongozi wetu. Ziggy Marley aliimba akisema "why we lose ourself when we find who we are?". Kwangu naona serikali ni kama muhogo. Muhogo ambao ukiwa m'bichi unalika na ukipikwa ukaiva unalika, lakini ukipikwa usiive vema hauliki. Na hapo ndipo tulipo. Wanataka tupoteze tulichonacho ili kuiga kigeni, ilhali hatuna uwezo wa kufikia kiwango kizuri cha kile kigeni na kwa bahati mbaya tumeshapoteza tulichokuwa nacho.
Asante saana na Mukama alinde

Powered by Blogger.