Header Ads

LightBlog

BAJETI INAYOPIGA MIAYO




MJADALA WA BAJETI ULIOJAA VISINGIZIO

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI mjadala juu ya bajeti ya mwaka 2009/10 kwa kuwa tayari umezaa visingizio. Kwani iwapo bajeti itashindwa kukidhi matarajio, serikali itajitetea kwa kusema, “kulikuwa na hali mbaya ya uchumi duniani.”

Lakini bajeti hii ina somo kuu kwa walioko serikalini na maeneo mengine yanayohusiana na utawala kisiasa na kifedha. Kuna kila sababu kwa wahusika kuanza twisheni.

Siku moja kabla waziri wa Fedha na Uchumi kusoma bajeti bungeni, Rais Jakaya Kikwete alihutubia taifa. Alisema hali ya taifa si nzuri kiuchumi kutokana na msukosuko wa kiuchumi duniani. Akasema serikali imetenga Sh. 1.7 trilioni katika bajeti ya sasa kukabiliana na hali hiyo.

Lakini wananchi wanakumbuka kuwa, wakati taarifa zimeenea dunia nzima kuhusu kuanguka kwa uchumi wa mabepari-viongozi duniani, Gavana wa Benki Kuu (BoT) na mawaziri katika serikali ya Kikwete walinukuliwa wakisema “Tanzania haitaathirika” kutokana na hali hiyo.

Leo tunaambiwa Tanzania imeathirika na rais analazimika kuandika dibaji ya bajeti ya taifa, ikiwa njia ya kujenga hoja ya kuweka kibano katika kukusanya kodi ili kupata fedha za kujinusuru.

Je, gavana na mawaziri walipata wapi kauli hizo? Je, wana uelewa wa aina gani kuhusu mifumo ya fedha duniani? Je, wanajua mahusiano ya fedha za madola makubwa duniani na fedha za nchi hii? Maswali ni mengi.

Inawezekana watawala wa siasa na fedha hawakujifunza hili shuleni na vyuoni? Inawezekana walisoma zamani na sasa wamesahau na hivyo wanahitaji kukumbushwa kwa njia ya twisheni?

Labda watawala wa siasa na fedha walitaka kuficha kinachobisha hodi. Wahaya husema katika methali, “Ekyaizile mabele” – huwezi kuficha matiti ya msichana yaliyoanza kuchomoza. Yataonekana tu.”

Kuficha kumekuwa tabia ya viongozi. Hakuna mvua. Kuna ukame mkubwa na mazao yamekauka. Viongozi watasema, “Hakuna njaa na hakuna atakayekufa kwa njaa.”

Watu wanakabwa na kunyang’anywa walichonacho. Nyumba zinabomolewa usiku na mchana na vitu mbalimbali vinaibwa. Watoto wa kike wanabakwa, albino wanakatwa viungo vya mwili na wengine kuuawa. Wengi wanashinda na kulala njaa. Viongozi watasema nchi ni shwari na kuna amani na utulivu.

Sasa huu ni ugonjwa; na ukificha ugonjwa kifo kitakuumbua. Kile ambacho gavana wa BoT na mawaziri walikuwa wakidai hakipo, ndicho kinaingizwa kwenye bajeti.

Rais ambaye hakuwakemea wateule wake wakati wanatoa kauli zisizoweza kuthaminika katika medani ya uchumi wala siasa, leo analazimika kuwaambia wananchi kuwa na “uvumilivu” wakati wa utekelezaji wa bajeti ya kujikwamua.

Uchumi wa Tanzania utakosaje kuathirika kwa mafua ya uchumi wa nchi za kibeberu wakati ni sehemu yake? Uchumi tegemezi utakosaje kuathirika wakati anayetegemewa kayumba?

Uchumi usiokuwa na viwanda wala kilimo – zile injini kubwa; na ambao hata umeshindwa kunadi vivutio vya asili kwa njia ya utalii – tunajua nchi zinaoishi kwa utalii tu – utakosaje kuyumba na hata kuanguka?

Gavana na waziri wanaweza kushindwa vipi kuona kuwa kushuka kwa mapato katika nchi za kibeberu; kufilisika kwa viwanda, kuongezeka kwa idadi ya wasio na kazi na kupungua au kukosekana kwa huduma za jamii kwa wasio na kazi, vinaweza kuathiri uchumi wa Tanzania?

Kwani walipa kodi wakubwa katika serikali zinazotoa mikopo na misaada wakiishiwa, wakafilisika au hata wakilegalega, kwa nini serikali zao ziendelee kufikiria Tanzania? Watapunguza au watasitisha mikopo au misaada. Lazima nchi itaathirika.

Kama kauli za kutoathirika zilikuwa zinatolewa na wahusika ili kuficha janga na ili kuepusha “kuogopesha wananchi,” basi huu ni utoto wa ukubwani katika siasa na uchumi.

Watanzania wengi sasa wanajua kuwa wanaishi kwa mashaka kutokana na sababu nyingi. Watawala wake wameshindwa hata kukusanya na kuweka akiba ya chakula. Likitokea janga pana la miezi mitatu, tayari serikali itaanza kuhaha kutafuta chakula kutoka nje ya nchi.

Hapa twende kwa mfano mmoja tu wa pamba. Serikali ilikuwa inaendesha karibu viwanda 20 vya nguo. Ikashindwa kuviendesha. Vikafa. Sasa tunauza pamba nchi za nje. Viwanda vya nje vinavyotumia pamba vikikwama, basi pamba haitanunuliwa na iliyokusanywa itaozea ilipo.

Mkulima wa pamba asipouza pamba, hatalima tena. Asilipolima pamba na hana zao jingine, atafukarika zaidi, yeye na familia yake. Atakufa polepole. Kifo ndiyo hatima ya mahusiano kati ya Mtanzania na ubeberu.

Hili linaweza kuonekana vema zaidi katika mazingira ya sasa; na hii ndiyo hali halisi katika nchi zote zinazojiita “changa” hata baada ya nusu karne ya kutoka kwenye ukoloni.

Nchi zote ambazo zimebaki kuwa shamba la bibi, ambamo wenye viwanda wanachota malighafi – mazao na madini – kama wanavyotaka, lazima zikose usingizi hivi sasa.

Kwa hiyo, kwa jinsi mfumo wa sasa wa uchumi wa nchi hii ulivyoshonwa kwenye mfumo wa uchumi wa kibeberu, siyo rahisi kukwepa mstuko, msukosuko na hata kuanguka kabisa kwa uchumi na kuangamia kwa watu wake.

Labda baada ya hili kutakuwa na funzo.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
(Makala hii ilichapishwa katika toleo la Jumapili, 14 Juni 2007 la gazeti la Tanzania Daima Jumapili chini ya safu ya SITAKI)

No comments

Powered by Blogger.