TAKUKURU YAWEZA KUWA CHUO BADALA YA KOROKORONI
CHUO KITATOA ELIMU KWA WENGI
Na Ndimara Tegambwage
SITAKI jengo kubwa la thamani ya Sh. 4.1 bilioni lililosimikwa jijini Dar es Salaam na kufunguliwa rasmi na Rais Jakaya Kikwete wiki iliyopita, litumike kufuatilia tu wala rushwa.
Wala sitaki rais aagize tu uchunguzi wa rushwa na kuchukuliwa kwa hatua dhidiya wala rushwa katika vyama vya siasa na wakati wa uchaguzi wa Oktoba (serikali za mitaa) na uchaguzi mkuu 2010.
Kwani jengo hili lingefanya makubwa zaidi. Hii ni kwa kuwa sitaki Taasisi ya Kuzia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) iwe taasisi ya kudumu (Samahani sana Dk. Edward Hoseah!).
Kwa vyovyote vile TAKUKURU itakavyokuwa imeshonwa kisheria, taasisi hii haipaswi kuwa chombo cha kudumu. Yawezekana walioiunda ili idumu kadri rushwa inavyodumu, walikuwa na nia ya kuongeza ajira. Kwa maana hiyo, hawanabudi kuchunguzwa.
Hapa usijali iwapo waliopendekeza “kuzuia na kupambana na rushwa” walikuwa rais, baraza la mawaziri au kwamba sheria ilitungwa na bunge. Kila mtu ana nafasi ya kupitiwa, kupotoka na kupotoshwa, kutojua, kusahau au kudharau; na daima kuna fursa ya kufanya mabadiliko.
Hakuna awezaye kutabiri lini rushwa itaisha. Wala lugha ya kijeshi ya “kupambana” haina uwezo wa kumaliza rushwa. Rushwa yaweza kukua na kushamiri kutegemea mazingira ya utawala na watawala walioko madarakani.
Bali rushwa huendana na vishawishi. Mahali ambako taratibu, kanuni na sheria vimeacha mwanya wa kutoa na kupokea rushwa, lazima rushwa itashamiri, bila kujali iwapo kuna taasisi tano 10 au 20 za “kuzuia na kupambana” na rushwa.
Kama madhara ya kutoa au kupokea rushwa ni madogo kuliko mafao ambayo mtoaji au mpokeaji atapata, basi rushwa itatolewa na itapokelewa. Kule kutokuwepo kizibo madhubuti ndiko kunatoa fursa na ndiko kishawishi na motisha.
Kuunda taasisi ambayo inafanya uchunguzi kwa “miaka yote,” inakamata, inasweka mahakamani watuhumiwa, tena kwa miaka yote, kuna uwezekano wa kufanya taasisi hiyo kuwa sehemu ya “porojo” za rushwa na hata kufanya baadhi ya viongozi wake kulenga na kulengwa na rushwa.
Kazi za taasisi ya kuzua rushwa zinaweza kupimwa kwa tuhuma zilizoibuliwa na wafuatiliaji wake, zilizopokelewa kutoka kwa wananchi au kuelekezwa na viongozi, zilizochunguzwa, zilizothibitishwa, zilizofikishwa mahakamani na zilizoisha, kwa maana ya matokeo ya kesi mahakamani.
Kazi nyingine za taasisi zinapimwa kwa kuangalia upanuzi wa uelewa wa wananchi juu ya kazi zake na nafasi yao katika kusaidia kuibua wala rushwa. Hii ni eneo la elimu kwa umma.
Eneo hilo la pili linalenga kufanya kazi ya kueleza na kufafanua maana ya rushwa, aina za rushwa, madhara ya rushwa na jinsi kila mwananchi anavyoweza kukabiliana na rushwa au kusaidia kutoa taarifa zenye lengo la kukabiliana nayo.
Chukua mifano hiyo miwili kama kazi kuu za taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa. Ukiziagalia kwa mtizamo wa ukiritimba utaona taasisi ina jukumu kubwa, nene, zito lisiloisha na wakati mwingine, ambalo haiwezi kulikamilisha.
Bali ukiziangalia kazi hizo kuwa zinafanywa na taasisi, asasi na maeneo mengine katika jamii, utaona kuwa jengo kubwa lililofunguliwa Dar es Salaam halitakuwa na kazi ya kutosha.
Karibu kila ofisi ya serikali inashughulikia suala la “kuzuia na kupambana na rushwa.” Asasi mbalimbali za kijamii zimelenga, hata bila kutamka, kuondoa rushwa ili shughuli zake ziende sawasawa na kwa mujibu wa matakwa ya jamii.
Katika hatua hii, kuna haja ya kuwa na TAKUKURU inayofanya kazi za kupeleleza – kazi ambazo zinafanywa na polisi? Hivi polisi hawana uwezo wa kupelekewa vitonyo wakafanya uchunguzi wa jinai ya rushwa?
Inalazimu kufanya mgeuko hata kama sheria ya TAKUKURU bado mbichi. Kwa jina tofauti lakini lenye maana ileile, taasisi hii iwe chuo maalum cha utawala kinachogusa nyanja zote za menejimenti – ndani ya serikali na sekta binafsi.
Chuo hiki kinaweza kushirikisha taasisi nyingine, kama Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na kutoa elimu juu ya utawala, taratibu, kanuni na sheria zinazohusika.
Wanafunzi wa chuo hiki ni wote waliomo serikalini, makampuni na mashirika yake, ofisi za makampuni na mashirika binafsi, wakufunzi kutoka vyuo mbalimbali ambao wanafundisha masomo katika eneo hili; asasi za kijamii zilizomo katika mapambano dhidi ya rushwa, wamiliki na waandishi wa vyombo vya habari; watumishi katika vyama vya siasa; wabunge na wanasiasa wengine.
Hii ina maana kwamba kazi ya kuelimisha jamii juu ya rushwa, madhara yake, kuchochea wananchi kuchukia na kupambana na vitendo vya rushwa, inaachwa mikononi mwa asasi zisizokuwa za kiserikali.
Ni asasi hizi, zilizo karibu zaidi na wananchi; zenye jukumu la kushawishi wananchi kukataa kutoa, kupokea rushwa na hata kuripoti vitendo vya rushwa; zisizo na maslahi katika rushwa kubwa au ndogo, ambazo zinaweza kukabiliana na rushwa maisha yote.
Mfumo huu waweza kuondoa mashaka ya wengi kwamba taasisi kubwa ya kupambana na rushwa, iliyoundwa na serikali, inalipwa na serikali na kiongozi wake mkuu anateuliwa na rais, inaweza kuhongwa pia au kunyamazishwa.
Hii ina maana kwamba majengo yaliyofunguliwa jijini Dar es Salaam sasa yanakuwa chuo maalum kwa masomo ya utawala, huku rushwa likiwa moja ya masomo hayo.
Maana kuu ni kwamba “TAKUKURU” kama taasisi kinakuwa chuo cha kutoa elimu ya kudumu na siyo taasisi ya kudumu. Elimu hii inadumu katika jamii kupitia asasi zake na vita vinaoenekana kupiganwa, majeruhi kuonekana na wafu kuhesabika, badala ya kusikika tu kupitia chombo cha serikali.
Hapa basi wafanyakazi wa kudumu wa TAKUKURU ama wanatafuta kazi mahali pengine; hasa katika asasi za kijamii au wanaomba kuajiriwa na chuo. Inawezekana.
0713 614872
ndimara@yahoo.com
(Makala hii itachapishwa katika toleo la Tanzania Daima Jumapili, 12 Julai 2009 katika safu ya SITAKI)

No comments
Post a Comment