Header Ads

LightBlog

MAMILIONI ZAIDI WATAKUFA KWA MALARIA




Ubeberu wanona kwa mgongo wa malaria

Na Ndimara Tegambwage

UHAI wa wananchi katika nchi za joto (tropiki), Tanzania ikiwemo, uko hatarini kutokana na ugonjwa wa malaria unaoua kwa wingi na kwa kasi kuliko ukimwi.

Nchi hizi, hasa watawala wake, wamejisahau. Badala ya kuchochea matumizi ya tiba asilia zilizoko kwenye makazi ya watu; na kuweka mazingira ya kujenga viwanda vyake, wameendelea kutegemea dawa kutoka viwanda vikubwa vya nje.

Matokeo ya uzembe huu wa kujisahau ni makubwa na mabaya. Watafiti wanaotoka nchi zenye viwanda vya dawa, wataendelea kupendekeza ni dawa ipi “bora” wamegundua itumike kutibu malaria.

Wakati huo wenye viwanda vya kutengeneza dawa na wafanyabiashara katika tasnia hii, wataendelea kutoa na kusimamia bei ya bidhaa hiyo bila kujali nani tajiri na nani masikini.

Kwa hiyo, kutokuwepo matumizi mapana ya dawa asilia; kutokuwepo utafiti na ujenzi wa viwanda vya ndani vya kutengeneza dawa; na kutokuwepo ruzuku kwenye dawa zinazotoka nje ili zipatikane bure au kwa bei inayowezekana, basi watu wengi watakufa kwa malaria.

Sasa serikali ya Tanzania imekiri kuwa bei ya dawa ya kutibu ugonjwa wa malaria, ambayo imeiidhinisha itumike, ni kubwa mno na wananchi hawawezi kuimudu.

Katika kipindi cha karibu miaka kumi, serikali imesema klorokwini (CQ) haifai, iachwe. Ikaachwa. Ikaleta SP (Sulphadoxine-pyrimethamine). Baadaye ikasema hata hiyo haifai, iachwe. Ikaachwa.

Serikali imekuja na dawa inayoitwa “mseto,” kwa ufupi wa ALU. Kabla hii haijaenea nchini, sasa inakiri kwamba imeleta kinyamkera. Dawa hii ni ghali sana. Dozi moja ni kati ya Sh. 13,000 na Sh. 15,000.

Hii maana yake ni nini? Ni kwamba Tanzania inashirikishwa, kwa kujua au kutojua, katika mchezo unaoangamiza maisha ya mamilioni ya wananchi na wakazi wengine katika nchi za tropiki, ambako ugonjwa wa malaria unaua bila simile.

Uchunguzi unaonyesha kuwa karibu watu milioni tatu hufa kwa malaria kila mwaka katika nchi za tropiki. Kati ya idadi hiyo, milioni moja ni watoto; ambayo maana yake ni kuwa mtoto mmoja hufa duniani kila baada ya sekunde 30.

Haya ni maafa makubwa na mbu aina ya Anofelesi, ambaye hueneza malaria, tayari amepewa na watafiti na walio katika mapambano dhidi ya malaria, jina la “gaidi mkubwa kuliko wote duniani.”

Gaidi huyu amenufaisha wenye viwanda vya kutengeneza dawa za kupambana na malaria na wote walio katika mkondo wa biashara ya dawa hizi, kiasi kwamba wagonjwa katika nchi masikini watakosa tiba. Watakufa.

Mkurugenzi wa Roche, kampuni kubwa ya kutengeneza dawa aliyeko Korea Kusini amenukuliwa akisema, “…Hatuko katika biashara ya kuokoa maisha ya watu, bali kupata fedha; uokoaji maisha siyo jukumu letu…”

Alikuwa akijibu ombi kwa kampuni yake kupunguza bei ya dawa za kukabiliana na ukimwi. Inatarajiwa atakuwa na kauli ileile au kali zaidi akiombwa kupunguza bei ya dawa za malaria kwa watu wanaoishi kwenye tropiki.

Katika hatua nyingine, mkondo mwingine wa viwanda, katika kasi isiyo ya kawaida, umetengeneza dawa bandia. Kwa hiyo, wakati dawa halisi haikamatiki kwa bei, dawa bandia haitibu au ni sumu.

Waziri wa Afya, Profesa David Mwakyusa alikiri jijini Dar es Salaam wiki iliyopita kuwa dawa ya malaria ambayo imependekezwa na wataalam, hainunuliki. Ni ghali sana.

Alirejea kilio cha mataifa masikini na wanaowaunga mkono, kuwa uundwe mfuko wa kimataifa (Global Fund) ambamo wenye fedha watachangia, ili fedha hizo zipelekwe kwa wenye viwanda vya dawa kupunguza gharama za uzalishaji na hivyo kupunguza bei ya dawa husika kwa watumiaji.

Hii ina maana “watu wema” wamchangie fedha tajiri mwenye viwanda vya kutengeneza dawa, ili apunguze gharama za uzalishaji na ili bei ya dawa ipungue.

Nchi masikini za tropiki zimeshindwa kupata mwelekeo katika kuzuia na kutibu malaria. Kwanza, zimeshindwa kuua mbu Anofelesi anayeeneza ugonjwa huu. Pili, zimeshindwa kupata tiba inayopatikana kwa gharama nafuu, kwa wepesi na karibu na makazi yao.

Kinachofanyika hivi sasa ni watawala kubabaika; kutapatapa na kuburuzwa na makampuni yanayotengeneza dawa za kutibu malaria.

Inawezekana hakuna kuburuzwa, bali watawala na makampuni kadhaa katika nchi hizi, wanashiriki biashara haramu ya “kuzalisha fedha” na siyo “kuokoa maisha” ya watu.

Kwa hiyo, likija pendekezo kuwa baada ya miaka 50 sasa “klorokwini” haimudu tena kutibu malaria, basi watawala na wataalam wa nchi hizi masikini, ama huchekea kiganjani kwa mtindo wa “kufa kufaana;” au huanza kuweweseka.

Rafiki yangu, Leonard Mutakyahwa, aishiye Dar es Salaam na Morogoro, hukumbwa na malaria kila baada ya miaka mitatu na nusu au minne. Lakini hadi hivi karibuni alikuwa akiendelea kutumia vidonge vya klorokwini kutibu malaria. Ilikuwa haijamkataa.

Mutakyahwa anaishi mjini. Lakini Mzee Flaviani Byeyombo wa kijiji cha Bushumba, Muleba ambako nilizaliwa na kukulia, hajawahi kumeza kidonge cha klorokwini au chochote kile cha kutibu malaria.

Mzee huyu hutumia mitishamba. “Kila nipatwapo na homa – mwili kukanyanyaa na kulegea, nikaumwa kichwa na wakati mwingine kuanza kuona kizunguzungu, macho kutoona vizuri na wakati mwingine kuwa na kichefuchefu, basi najua ndiyo hiyo mnayoita malaria imenitembelea,” anaeleza.

Maelezo ya Byeyombo hayaonyeshi dalili ya malaria peke yake. Dalili hizo zaweza kuwa za magonjwa mengine mengi.

Kwa hiyo dawa anayotumia mzee huyu, familia yake na wenzake kijijini, ni mseto wa majani ya miti mingi unaoitwa omubazi g’womushana kwa kutibu malaria na magonjwa mengi mengine na hata kuwa kirutubisho.

Hata Wahaya na wakazi wa muda mrefu wa Bukoba (Buhaya) ambao sasa wanaishi Dar es Salaam na miji mingine, na ambao wameendeleza mila na desturi za vyakula vyao na tiba, bado wanatumia mseto huu kwa tiba nyingi.

Unaweza kupendekeza bila woga, kwamba bila mitishamba, watu waishio katika nchi za tropiki wangekuwa wameteketea wote; kwani wanaofikiwa na vidonge vya kuzuia au kutibu malaria ni idadi ndogo – hasa Afrika.

Haya ndiyo maisha ya mamilioni ya watu waishio mijini. Kidonge au kijiko cha dawa ya kunywa kutuliza kikohozi, kuondoa mwasho mwilini, kuongeza damu; kukomesha kuhara au kutibu malaria, hakifiki mbali. Mitishamba ndiyo imekuwa ngao na tiba kuu.

Ukitaka waweza kusema kuwa wakazi wa nchi za tropiki waishio nje ya miji, wamejilinda, kujikinga na kujitibu kuliko tawala ambazo zinaweza kuwa zinakimbilia hongo ya asilimia 10 kwenye gharama ya dawa za viwandani; na nyingine zikiwa feki.

Hata kule ambako kidonge kama klorokwini kilipenya, matumizi yake hayakuwa sahihi. Kutokuwepo elimu ya kutosha juu ya matumizi, ama kulisababisha vifo au usugu wa malaria.

Nakumbuka Mama Zulfa, kijijini Bushumba, Muleba aliyenieleza mwaka 1996, “Nimechukua hivyo hapo (vidonge vya klorokwini); juzi nilimeza viwili, hivyo vingine viwili nitameza tena huko mbele iwapo nitajisikia homa tena.”

Katika kijiji cha Mwamihanza, Shinyanga, mwaka 1985, tukiwa kwenye ziara ya Mwalimu Julius Nyerere, mama mmoja aliniambia alivyonunua vidonge vinne vya klorokwini na kuwagawia watoto wake wanne – kila mmoja kidonge kimoja. “Naona sasa wanaendelea vizuri,” alieleza.

Kwa hiyo, klorokwini, SP na hata ALU, ni baadhi ya dawa ambazo zimekuwa zikibambikizwa kwa jamii hata bila maelezo ya kutosha kuhusu matumizi bora.

Kupungua kwa kinga dhidi ya malaria na usugu wa ugonjwa huo, haviwezi kamwe kuwa kwa viwango sawa kwa sehemu zote katika nchi moja au katika nchi zote za tropiki.

Bali hakuna anayetaka kujua ni sehemu gani ya nchi ilikuwa haijafikiwa na dawa za viwandani; mwingiliano wake na wenye malaria uko vipi; idadi gani ya watu wanatumia dawa zipi na waliokuwa hawatumii dawa hizo walikuwa wanatumia nini.

Kwa njia hiyo, king’ora kikilia Ulaya, kwamba sampuli ya mji mdogo kama Kongwa (Dodoma), na siyo vijijini, inaonyesha usugu wa malaria – na sehemu nyingine kama hizo katika nchi nyingine – basi inatosha kuharamisha dawa na kuingiza mpya.

Hoja ya mtanuko wa eneo la maambukizi, inakubalika; lakini kuna hoja kinzani kwamba walioambukizwa malaria ambako vidonge havikufika wamepona.

Kwa hiyo kuna njia nyingine isiyo rasmi ya kutibu ugonjwa huo na nchi za tropiki hazistahili kuendelea kuwa “panya wa maabara” – wa kufanyia majaribio ya dawa.

Hadi hapa tunaona ni kwa kiasi gani nchi za tropiki zilivyoendelea kucheza na mauti ndani ya nyumba wakati mkombozi yuko mlangoni.

Tafiti za dawa za asili za kutibu malaria zimekwenda goigoi sana katika Tanzania na nchi za tropiki, hasa Afrika wakati watafiti walikuwa na mahali pa kuanzia.

Waliougua malaria wapo. Dawa zilizotumika kuwatibu zipo. Waliotibiwa kwa mitishamba hadi wakapona wapo – ni mamilioni. Ugumu umekuwa wapi?

Hata wakati nchi za tropiki zikiendelea na utafiti na “ombaomba,” uko wapi mkakati wa kuhimiza wananchi kutumia dawa za asili?

Misitu na vichaka vya nchi za tropiki ni mali, ni dawa, ni baraka. Majani na mizizi kutoka nchi hizi, na hasa Afrika, vimetumika kutengeneza dawa ambazo zinaletwa nchini na kuuzwa aghali.

Mchungaji Emmanuel Mwakalinga wa Tukuyu, mkoani Mbeya pamoja na kazi zake za kuhubiri neno la Mungu, anatoa dawa aina mbalimbali kwa magonjwa kadha wa kadhaa.

Kwa Mwakalinga ndiko chimbuko jingine la dawa za kutibu malaria, homa ya matumbo na magonjwa mengine yaliyoshindikana. Ni dawa za mitishamba. Wako wengi wa aina hii nchi nzima na katika nchi za tropiki.

Swali kuu ni wataalam wa nchi hizi wamefanya nini, kwa miaka 50, kutumia ujuzi wa waendesha tiba kwa kutumia dawa asilia?

Serikali za nchi hizi zimefanya nini katika kujenga mazingira na kuchochea elimu katika medani hii ili kukabiliana na mbu na malaria?

Hata pale serikali ziliposhindwa kufanya haya, zimechukua hatua gani kuhimiza wananchi kutumia mitishamba iliyoko karibu nao, kwa maelekezo madogo tu ya wenye ujuzi, ili kukabili malaria?

Ninafahamu nyumba moja jijini Dar es Salaam ambayo mazingira yake yamepandwa miti shamba kwa ajili ya matibabu ya malaria.

Mjini Morogoro, kuna eneo moja karibu na viwanda, Kihonda ambako mtu mmoja amepanda miche ya mitishamba aina ya Artemisia annua. Mmea huu wenye asili ya China umekuwa ukitumiwa kwa kutibu malaria na magonjwa mengine kwa zaidi ya miaka 2000.

Pamoja na uchunguzi unaoendelea kwa ngazi ya maabara mbalimbali duniani, baadhi ya nchi za tropiki zimeanza kupanda, kuvuna na kutumia mmea huu, wenye aina zaidi ya 50, kwa tiba ya mafanikio.

Majirani wa Tanzania – Kenya na Uganda, wana bustani za mmea huu. Kenya inakadiriwa kuwa na wakulima zaidi ya 4,000 ambao wameanza kuvuna fedha kutokana na kuuza majani ya artimesia.

Asasi ya kijamii ya Natural Uwemba System for Health (NUSAG) kaskazini mwa Tanzania imekuwa ikishirikiana na asasi nyingine katika Afrika Mashariki kutafuta tiba ya malaria kwa bei nafuu na mmea huu umekuwa moja ya vyanzo vya tiba ya uhakika na isiyokuwa na athari mbaya.

Mazingira ya dawa ya sasa ya kutibu malaria ni kwamba kutokana na ughali wake, wanaofikiwa na dawa hiyo watakufa wakiitazama.

Kuna ubaya gani kwa wataalam nchini, hata kama hawajakamilisha uchunguzi wa dawa nyingi nchini zinazotibu malaria, kupiga mbiu ya matumizi ya mitishamba ambayo imelinda uhai wa mamilioni ya wananchi kwa miaka yote?

Kuna ubaya gani kufanya hoja ya kuokoa maisha ya wananchi, kwa njia ya tiba za asili, kuwa ajenda muhimu ya wataalam wa tiba na watawala?

Kuna ubaya gani kuhimiza kilimo, kikubwa na kidogo, cha Artemisia annu, hata kama sehemu ya bustani kwa kila kaya, ili watu wajiponye, angalau kwa sasa, huku wakisubiri tiba za kisasa?

Umuhimu wa kufanya haya haraka unatokana na takwimu: Mtoto mmoja hufa duniani kila baada ya sekunde 30; na kwa jumla watu milioni tatu hufa kila mwaka kutokana na malaria.

Kila kabila au jamii ina omubazi g’womushana kwa jina tofauti. Kwenye dawa hizo ongeza Artemisia annu; na nyingine na nyingine za mitishamba. Watu wapone; hata kama ni kuahirisha kifo tu.

Tuogope kutangaza tiba kwa kuwa haijafanyiwa “uchunguzi wa kisasa” au tumihimize matumizi kuokoa maisha ya watu wengi?

Sasa Mutakyahwa anatumia mitishamba kutibu malaria na ana bustani ya Artemisia annu.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
(Makala hii imechapishwa katika toleo la Jumatano, 17 Juni 2009 la gazeti la MwanaHALISI)

No comments

Powered by Blogger.