Header Ads

LightBlog

SERIKALI IOMBE ASKARI WAKAE KIMYA


Mawe yakisema, serikali itaumbuka

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI waziri Jeremiah Sumari achokoze Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kwa kutumwa au kwa sababu zake binafsi.

Majeshi ni mawe makubwa. Majabali. Miamba. Majeshi ni wagumba. Majeshi yakitaka kuzaa sharti yakubali kufa polepole; kwa maana kwamba atokee wa kuyapasua ili yatoke mengi kwenye mawe makubwa au miamba. Hapo hayabaki mojamoja na imara tena.

Na kawaida majeshi ya nchi hayachokozwi na mtu wa ndani wala wa nje. Wachokozi huchokoza nchi na watawala wa nchi zilizochokozwa huagiza majeshi yake kwenda mstari wa mbele na kukunja uchokozi kama jamvi la wageni.

Lakini uchokozi uliofanywa na waziri Sumari ni wa ndani na unaweza kufanya mawe makubwa, miamba kutamani kutoa sauti na kusema hayataki kupasuliwa; yaachwe kama yalivyo.

Akijibu swali la Dk. Willibrod Slaa juu ya ufisadi ndani ya mradi wa Meremeta, Sumari alitoa majibu ya vitisho. Alimwambia mwakilishi wa Karatu (CHADEMA) aachane na hoja ya ufisadi ndani ya Meremeta.

Kiasi kinachodaiwa kupitia Meremeta kwenda mifuko isiyojulikana si haba. Ni zaidi ya Sh. 155 bilioni. Waziri anamwambia mbunge aachane na hoja ya Meremeta kwa madai kuwa mradi huo ulikuwa wa jeshi; kwamba ni suala nyeti na labda ni kuingilia suala la usalama wa taifa.

Waziri anataka kulazimisha mawe kusema. Mawe yatabaki kimya juu ya ahadi zao; juu ya mipango yao na silaha zao; juu ya mikakati ya sasa na baadaye; juu ya mbinu mpya walizopata katika medani ya vita; juu ya wanachopanga kufanya hivi sasa.

Ukimya huu ni kama jua, mvua na upepo vipigapo kwenye mwamba na mwamba ukavumilia. Zaidi ya hapo, miamba husema. Miamba mingi imeota juu ya mizimu ya kale iongeayo wakati wa jua kali.

Inawezekana, siku moja unapita karibu na miamba hiyo, wakati wa jua kali, ukasikia mtu akikuita kwa sauti ya juu sana – mara mbili au mara tatu – na usimwone.

Wale dhaifu wa moyo huweza kuanguka chini na kuzimia; wengine humudu kukimbia hadi nyumbani kwao, wakitweta na kulowa jasho mwili mzima huku wakiishiwa na kauli. Mawe, majabali, miamba imeamua kusema!

Wakati huo hujawahi kuichokoza. Hujailalamikia wala kuituhumu. Hujaisingizia wala kuihusisha katika miradi bubu ya watawala. Inasema tu. Inabubujika. Sembuse utakapoihusisha na wizi, uporaji, ukwapuaji, au kwa ujumla – ufisadi!

Ikae kimya? Sitaki waziri Sumari achokoze miamba na yenyewe iseme kwamba haijui Meremeta ni nini na ya nani. Kwamba haijawahi kunufaika na kampuni hiyo. Kwamba mafao yaliyotokana na Meremeta hayafahamiki jeshini. Kwamba hayakuingia jeshini.

Sitaki waziri achokoze miamba ianze kukohoa na kunong’ona na hatimaye kulipuka. Miamba hii inajua kuwa fedha za kuendesha jeshi hutoka kwenye bajeti ya serikali inayosomwa na kupitishwa bungeni.

Miamba hii inaelewa vema kwamba wakati Meremeta wanaanzisha mradi walihamisha wananchi kutoka makazi yao. Walihamisha hata kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa na kutawanya askari katika vijiji kwa kutumia mikokoteni.

Si wananchi – raia, wala askari walionufaika na mafao ya Maremeta baada ya kuanza kuvuna kutokana na mgodi. Shule na zahanati vilivyong’olewa havijarudishwa. Bwawa kubwa la maji lililokuwa sehemu ya uhai wa watu na viumbe anuwai, halijarejeshewa hadhi yake.

Sitaki watawala jeshini wajitokeze na kuiumbua serikali juu ya matumizi haya. Sitaki wapatikane watumishi wa Wizara ya Ulinzi na kuthibitisha kuwa hawajawahi kupanga fedha za Meremeta au sehemu yake katika matumizi ya wizara.

Sitaki maofisa wa ngazi za kati jeshi waanze kufurukuta na kusema hawataki kusingiziwa katika suala la ukwapuaji na hivyo kujitokeza na ukweli utakaoangamniza hadhi ndogo ya watawala iliyosalia.

Sitaki askari wa vyeo vya chini ambao wanajua vema kilichokuwa kinaendelea waanze kujitokeza na kusema walichoona na nani hasa walikuwa wavunaji wakuu wa Meremeta na siyo jeshi.

Wala sitaki askari wakumbushe serikali kwamba Tume ya Jaji Bomani iliishasema kuwa Meremeta si mali ya serikali bali ni ya binafsi. Labda likisemwa na wao ndipo serikali itasikia na waziri Sumari ataelewa.

Nani anataka azibuliwe masikio kuliko alivyofanya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Aliiambia Kamati ya Bunge kuwa Meremeta haimo katika orodha ya mashirika ya umma na kwamba ofisi yake haijawahi kuikagua.

Mei mwaka jana tulipeleka baruapepe kwa benki ya Nedcor Trade Services ya Afrika Kusini kuhusiana na suala hili. Hatukujibiwa. Tuliwaandikia Deutsche Bank AG ya Uingereza. Hawakujibu.

Lakini kwa kufuatilia kinachoendelea ni kwamba serikali haifanyi lolote. Imetafuta mahali pa kuegesha na kusahau hoja za wananchi wanaotaka kujua huyu Meremeta ni nani na fedha alizochota alizitumia wapi.

Matumizi ya visingizio vya jeshi, kama anavyosema Sumari, hayana uzito tena. Hayamtishi yeyote. Wananchi, wachunguzi na wengine wanaotafuta ukweli wangestuka na hata kuogopa kama wangekuwa wameingilia undani wa shughuli za jeshi.

Lakini hili la kikampuni cha Meremeta halimtishi mtu. Badala yake linaweza kuiweka serikali pabaya, kwani inaendelea kujichanganya; kuficha ukweli na hatimaye kusema uwongo.

Hatari kubwa inaweza kuzuka pale mawe, majabali na miamba itakaoamua kuvunja kimya; siyo lazima kwa mikutano ya hadhara bali kwa mn’ong’ono tu ambao hatimaye utavuma kama upepo wa kimbunga.

Na askari – hiyo miamba – ni watoto wa watu masikini na wao ni masikini pia. Hawana cha kupoteza kwa kusema ukweli wanaoujua. Hapo ndipo serikali itaumbuka zaidi.

Nani anaweza kuiondolea aibu serikali kwa kusema ukweli na kuijengea heshima na uhalali? Kama siyo mawaziri wake, nani hasa? Tusubiri majabali yaite wakati wa jua kali na kwa mzizimo wahusika wazimie?

Uwezekano wa aliyezimia kupitiliza hadi dunia nyingine ni mkubwa kuliko aliyesimama. Kwa nini serikali ijiingize kwenye majaribu tata? Ukimya unaidhalilisha serikali na kuiondolewa uhalali. Itoboe kilichomo ndani ya Meremeta.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
(Makala hi ilichapishwa katika toleo la Jumapili, 28 Juni 2009 la
Tanzania Daima Jumapili)

1 comment

godwin said...

tanzania ni miongoni ya mataifa yenye utulivu utulivu huu usiwafanye watawala kufanya ndio misingi ya kukandamiza jamii fulani tumeshuhudia polisi wakitwa wazembe na waheshimiwa sipingi kwani hata walimu na wanajeshi nao utendaji kazi wao umeshushwa na upungufu wa maslahi duni na ukosefu wa vitendea kazi watawala wameamua kuwaingiza katika mtego utaowatofautisha na wananchi kwa kuwahusisha na ufisadi wa meremeta watawala wanatumia misingi ya nidhamu ya jeshi kutowajibika kujibu hoja yeyote iliyotolewa na mkubwa wako, napenda kusisitiza kwa watawala wasijaribu kutibua misingi mizuri ya jeshi na kulitwisha mzigo wa ufisadi, ningependa kuwafahamisha ya kuwa mzigo wa ufisadi ni vema wachague ni fisadi gani atayeubeba na si jeshi kwani utakua ni uonevu usiostahiri na utaoleta madhara makubwa kwa watawala wenyewe ni nani asiyefahamu kutoa kafara wapiganaji wetu kuna madhara gani? sipendi kuona watanzania tunapoteza misingi ya amani na utulivu ila nasita kuona ni wapi jahazi la tanzania linaelekea , vijana wapo tayari kulikomboa taifa lao kutoka katika dimbwi la umasikini hata kwa dhana duni ila watawala wawahakishie sera bora tunaweza kushiriki katika kilimo lakini taifa ni lazima litunze ardhi kwani sasa taifa linabinafsisha kwa wageni ningependa tusiliingize jeshi katika ufisadi ila ikibidi lishirikishwe kwenye uzalishaji na miradi kama nyumbu inaweza kuleta tija na heshima kwa jeshi letu sishangai kuona viongozi wakijisahau kwani ni kawaida kwa binadamu wasio na uwezo wa kukumbuka ni wapi walipotoka ni nani asiyejua ni askari wangapi wanalala njaa na kushindwa kusomesha watoto wao vyuo vikuu kutokana na sera za watawala wanaojari maslai yao na kutaka kujinufahisha kupitia wanyonge,natambua tanzania ni tajiri kwani mimi kama mwanachuo ninayesomea account and finance natambua nini kinaendelea, kikubwa kinachonisikitisha ni kitendo cha watawala kutaka kuliunganisha jeshi na wakoloni sijui wamelala na kusahau wanakata tawi waliokalia kwani ni nani atayemtoa mkoloni wanayempa ardhi yetu kutokana na ukuhadi wa viongozi wetu tazama watawala wanavyotumiwa kuteketeza maisha ya watanzania north mara (NYAMONGO) je inahitaji elimu ya chuo kutambua taifa lipo katika ukoloni mamboleo na ni upungufu wa afikiri unaosababisha umasikini wetu na kutumiwa kama mabwege na wakoloni na sasa mkoloni anasababisha kitendo cha kulipotezea imani jeshi letu ili iwe raisi kuja tena kwa kadri ninavyowafahamu watu wa kanda ya ziwa nachelea kusema serikari inaliingiza jeshi la polisi katika mgogoro usio na tija jeshi la polisi na wananchi nafahamu ya kuwa watawala wameamua kutumia jeshi vibaya kwa malengo ya kisiasa ili kuvunja sakata la ufisadi na kuendeleza ukuhadi wa wakoloni kama hawatambui ni kosa linaloweza kusababisha mabadiliko ya historia ya nchi na wao wasipate watu wa kuwatawala kwani ni nani mwenye furaha huko somalia..? kama si magaidi pekee najiuliza watawala wetu wanataka kuwa magaidi ..? wiishi kama somalia au wanapenda wawe kama MOBUTU SESESEKO....? ni kitu cha kushangaza kwa watawala wetu kutopenda kuwatumia wataalamu wetu sasa imefika wakati wanafikiri wanastahiri kujiheshimu wao tu na kutupia mzigo wa lawama kwa kila wanayemuona napenda kusisitiza ya kuwa wanajeshi si walimu kwani watawala wamewakandamiza kwa kipindi kirefu bila ya wao kujinasuo na kuongozwa na vibaraka wanaouza haki za walimu kwa SUZUKI NA RAV 4 , naipenda tanzania na nisingependa 2020 niwe mkimbizi katika ardhi ya wazungu kama wasomi wetu wwalivyozoea kudhani ya kuwa ulaya ndio kipimo cha mafanikio yao, najiuliza je watawala wanajaribu kuamsha mawe ili wao wanufaike au wawe wakibizi katika ardhi za wanaowafanya makuhadi wao na kutorosha rasilimali za taifa lao
nisingependa kuelezea kwa undani zaidi kwani hata baba yangu aliwai kusema "WATAWALA NI JAMII YA WATU WASIO NA UCHUNGU NA RASILIMALI ZA NCHI ZAO NA NI WATU WASIOTESEKA NA VITA NA UMASIKINI WA TAIFA" nawatakia watanzania mafanikio na ushindi katika maisha ya kila siku na kushauri watawala wasiangamize kizazi kisicho na hatia
MUNGU IBARIKI TANZANIA
MUNGU IBARIKI AFRIKA
GODWINI CHACHA
0718122081

Powered by Blogger.