WAKO WAPI WALIO WAKALI SANA?
VIJANA WA TANZANIA WASIOKUA
Na Ndimara Tegambwage
WAKO wapi walio wakali sana, sisi twawataka…Huu ni wimbo. Tuliuimba tukiwa madarasa ya awali. Wakati unaimba, unapiga chini, tena kwa kishindo, mguu wako wa kulia na kuonyesha uso wa ukakamavu.
Ni enzi za ujana. Katika ubichi wa umri na kujituma; na kutumwa na wazazi. Acha siasa ziingie. Wanasiasa wa umri mkubwa wakaanza kutuma vijana.
Fanya hili, fanya lile. Ninyi ni taifa la kesho. Leo ni taifa letu – sisi kwa sisi. Na vijana wakakubali. Mgongoni wakapandwa mithili ya farasi; na vikongwe kuwavusha.
Lakini vijana hawa hawakui. Akibahatika mmoja akaona mwezi, anaudaka uwaziri au unaibu waziri. Mwingine anakuwa katibu ndani ya chama; lakini sharti wakubali kuendelea kunyonya na kuwekewa kiporo mafigani.
Vijana wakitaka kula sharti waombe ruksa. Sharti waombe ruksa kwenda matembezi. Sharti waombe ruksa kuimba nyimbo za vijana; na sharti wacheze ngoma za kale; za leo zina maasi.
Chini, ardhi haipenyeki. Ardhi imegandana. Juu, wamekaa vigogo kwa maana halisi ya vigogo. Vizito kwa umri. Kwa madaraka. Vizito kwa mamlaka. Kwa kauli nzito na kali. Kwa kutotaka kubishiwa au kujadiliwa hadharani. Vigogo.
Wako wapi walio wakali sana wa kuvunja ardhi; kutokomea na kutokezea kwingine? Kama hilo ni aghali, wako wapi basi walio wakali sana wa kupasua ufa katikati ya vigogo?
Wale wa kulenga na kunasa. Wale wa kutamani kupenyeza sauti na utashi wa vijana kwenye mwamba wa vigogo na ardhi ya ugumu wa kigumu.
Wako wapi walio wakali sana wa kujadili hoja kuu za vijana wanaokua; na siyo waliolemaa na wanaolamba nyonyo hata katika umri mkubwa?
Wako wapi wanaoona mbali na wasioteta? Wale wenye damu moto ya ujasiri wa kweli. Wako wapi waliojaa hekima lakini wakali kwa mali ya vijana na umma, pale inapogugunwa na fungo? Wako wapi?
Wako wapi wenye uwezo wa kuwaambia wale waliowakalia vichwani: Asante kwa malezi, lakini kwa hili baba, tuheshimiane? Wale waliotayari kuweka mitima yao wazi kwa kila mmoja kuona.
Wako wapi walio wakali sana wa kuona mbali; wale wa kukiri kukua na kukomaa na wasiotaka nyonyo tena? Wako wapi wenye bisibisi, tindo na sululu za kuvunja mwamba uliowakandamiza?
Wako wapi walio wakali sana – wasio na mapenzi ya minong’ono na kuumana sikio? Wale wasioteta bali wanaoweka wazi hoja zao; hoja za vijana na wa makamo; hoja za taifa na nchi. Wako wapi wasiojimung’unya kwa aibu na unafiki?
Wako wapi wa kuwaambia vikongwe kwamba sasa watulie wahudumiwe? Kwamba ni kweli, wamewatoa mbali, lakini leo hii wakubali kuwa wamechoka na wanahitaji kusaidiwa.
Wako wapi walio wakali sana; wale wa kuwaambia vigogo: Ahsante kwa malezi lakini kuendelea kuwa “kamanda wa dogodogo,” tena kwa umri huu, ni kejeli kama siyo matusi?
Wako wapi wa kuhoji ukamanda wa vijana kushikwa na vikongwe? Wale wa kuhoji utitiri wa nondo umwagwao vichwani mwa vijana kwa madai ya kuadabisha, kutiisha na kunidhamisha?
Wako wapi walio wakali sana – wa kuweza kunyoosha kidole na kusema, baba hapa umekosea? Kwamba baba hapa uko uchi? Wasionyenyekea ukali wa sauti bali hoja mwanana yenye tija kwao na kwa taifa?
Asije mtu na kusema hawapo. Asitokee wa kuamini kuwa wote bado ni vifaranga. Asiwepo wa kuamini kuwa vijana ni watoto wasiokua; wasioweza kufikiri na kutenda.
Nani anataka kuwa mtoto ukubwani? Isije kuwa hadithi ya Kabuyanga. Alinyonya. Miaka miwili. Akanyonya. Miaka minne. Akanyonya. Miaka mitano.
Kabuyanga akawa anamwambia mama yake: Mama ee, naona umevaa vizuri na unataka kuondoka. Naomba urudi mapema mama; nataka kunyonya!
Umri mkubwa. Nyonyo mdomoni. Mama analiendekeza lakini pia analinyima haki na uhuru wa kufikiri na hivyo linashindwa kujitegemea.
Kumbe ni mabavu ya Kabuyanga tangu udogo. Waliona mwili wake ule ungewaletea kasheshe kama angepewa mbawa. Akabakizwa kwenye mapakato ya mama. Akanyonya na kulewa maziwa. Akalelemaa.
Bali huyo ni mmoja. Ni mmoja peke yake. Hukaa na walomlemaza na kuteta vijana wenye nguvu, ukakamavu na nia ya kupasua ardhi na mbingu ya vigogo vikongwe.
Fumbua macho. Inua kichwa. Angalia juu na usiogope. Ni utando wa mwamba tikitiki. Kwa haraka, mwamba hauvunjiki. Haupasuki.
Bali kwa walio makini, ni ukungu mtupu. Panahitajika ujasiri mdogo kupenya hasira, chuki na gadhabu za baba na mama Kabuyanga.
Wako wapi walio wakali sana – wenye uwezo wa kuhimili vishindo vya matusi, kebehi na kejeli; ukali wa macho mekundu na mibubujiko ya midomo na mashavu yanayoanguka mithili ya embe la vuli?
Wako wapi walio wakali sana wa kuandaa mahusiano mapya na kukata mikatale iwawekao vijana utumwani? Wako wapi wa kuzima migegemo ya Kabuyanga ya kuendelea kuuma nyonyo ukubwani?
(Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0713-614872 na imeili: ndimara@yahoo.com)

No comments
Post a Comment