Header Ads

LightBlog

CHAMA TAWALA KINAPOKIRI KUZIDIWA NGUVU TARIME

CCM YATAKA MSAADA WA ASKARI

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kibaki katika jimbo la uchaguzi la Tarime wakati tayari kimekiri kushindwa. Tujenge mashaka: Kinabaki uwanjani hadi uchaguzi ili kifanye nini?

Mapema wiki hii, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Mekwa alikaririwa na vyombo vya habari akikiri kuzidiwa nguvu; akisema vurugu zimezidi na wafuasi wa chama chake wanamwagiwa pilipili.

Katika hali inayoonyesha kuwa ingekuwa kazi yake binafsi angebwaga manyanga na kuacha jimbo, Msekwa amekaririwa akisema kuwa atamweleza Rais Jakaya Kikwete apeleke askari wengi zaidi kukabiliana na kile alichoita “vurugu.”

Hapo ndipo CCM imefikia. Siyo siasa tena. Ni askari. Ni silaha. Ni vita. Rejea kauli za watawala wakati wa vuguvugu la kurejesha mfumo wa vyama vingi: Kuanzia kiongozi wa ngazi ya chini kabisa hadi mkuu wa nchi, wote walieneza hofu kuwa “vyama vingi vikija, vita vitakuja pia.”

Leo, tunajua nani angeleta vita. Watawala wakishindwa, au wakionekana kushindwa, au wakitikiswa; wanaweka siasa chini. Wanachukua kauli na vitendo vya ubabe. Wanakimbilia kwa rais kuomba askari na silaha. Wanatangaza vita. Wanaanzisha vita. Wanaingiza vita Tarime na nchini.

Hivyo ndivyo vita ambavyo wanasiasa waliokuwa madarakani kati ya 1985 na 1992 walikuwa wakitishia wananchi. Kwamba wao, watawala wakishindwa, au wakiona wanaanza kutetereka, hawatakubali. Wataanzisha vita.

Naomba kutoa hoja, kwamba kwa kushikilia utawala kwa karibu miaka 50; kwa mbwembwe za utukufu wa kisiasa na majigambo; kwa woga wa kushindwa na hisia tu kwamba watadhalilika iwapo watashindwa; hakika baadhi ya viongozi wa CCM wanaweza kuingiza nchi vitani.

Lakini hiyo ndiyo hali iliyoko jimboni Tarime. Kama makamu mwenyekiti wa chama kinachopanga ikulu anatamani matumizi ya “askari zaidi” na hivyo silaha zaidi, basi mambo ni magumu kwa chama hicho.

Na haya mapenzi ya CCM kwa askari na silaha ni mapenzi hatari. Silaha badala ya siasa? Askari badala ya raia wanaoimba nyimbo na ngonjera? Milio ya bunduki badala ya hotuba zilizosheheni ahadi zinazotekelezeka na kuambizana ukweli uwanjani? Hapana.

Naomba kutoa hoja, kwamba ikifikia hapo, askari wanaoitwa katika siasa wataanza kujiuliza: Hivi kumbe watu hawa (watawala) ni chui wa karatasi?

Mwandishi mmoja wa vitabu wa Afrika Magharibi aliwahi kusema kuwa, “Kama wanasiasa wanatumia mabavu, kwa nini basi wasiwaanchie nafasi hiyo askari ambao kutumia mabavu ndio kazi waliyosomea?”

Hatari! Askari wameweza kusema, katika nchi mbalimbali, tena kwa jeuri ya uhakika: Kama siasa zimeshindwa, si basi ziwekwe chini; tutawale sisi kuliko kuwa na mseto wa siasa na silaha? Uuuuhwi! Mungu apishe mbali. Lakini ndiko CCM inataka kuelekeza.

Kwa CCM kutaka askari zaidi uwajani Tarime wakati wa uchaguzi mdogo wa kutafuta diwani na mbunge, ni kujitia kitanzi mbele ya wapiga kura.

Ni wilayani Tarime ambako kumekuwa na ugomvi kati na baina ya koo; tena kwa muda mrefu. Serikali imeshindwa au imekataa au imedharau kuingilia kati kwa busara na kishindo ili kumaliza migogoro.

Iweje basi, serikali iombwe kupeleka kishindo cha askari na silaha wakati wa uchaguzi? Je, si atakayetangazwa kuwa mshindi kupitia askari na silaha atakuwa amewekwa kwa mabavu, badala ya ridhaa ya wananchi kwa kauli za kisiasa tu?

Je, atakayeshindwa au hata akishinda, baada ya kutumia askari wa taifa, silaha za nchi, muda na fedha nyingi za umma; atafidia vipi gharama hizo, tena kwa riba gani? Lakini kabla ya hapo, nani anaruhusu matumizi hayo?

Ushauri mzuri ungekuwa, kwamba anayeona ameemewa, ajiondoe taratibu na kimyakimya. Wachezaji katika uwanja wa Tarime ni vyama vya siasa na wanasiasa. Chama ambacho kinaona siasa zake zimeyeyuka, kisiite askari. Kijiondoe.

Kutumia nguvu ya nyongeza ya askari katika uchaguzi kutadhoofisha siasa za utashi. Kutajenga woga miongoni mwa wananchi. Kutafanya baadhi ya wananchi kupoteza fursa ya kupiga kura.

Matumizi ya askari kujaribu kuleta ushindi kwa chama kilichoko madarakani, kuna uwezekano wa kuleta mbunge legelege; aliyechoka kabla ya kuanza kazi na ambaye amezibwa mdomo kabla ya uchaguzi kufanyika. Huyu siye wanayemtaka wananchi wa Tarime.

Kutafuta mbunge kwa kusaidiwa na askari, ni kukana kanuni za kidemokrasia; ni kufuta utawala wa kiraia hatua kwa hatua na kuasisi kinyemera utawala wa kiaskari.

Hii ni njia ya kuonjesha askari asali. Wakinogewa asali wafanyeje? Bila shaka watachonga mzinga. Huko ndiko wanatupeleka Pius Msekwa na Yusuf Makamba.

Mkoa wa Mara una historia ya upinzani tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi nchini. Kwa Msekwa ambaye hana uzoefu wa kukurukakara za kutafuta kura katika mazingira ya mshikemshike, bila shaka ataogopa.

Woga wa Msekwa unatokana na ukweli kwamba CCM inaweza kushindwa vibaya pale wananchi wa Tarime watakapoamua kuiadhibu kwa kutumia vitisho; ikiwa ni pamoja na kauli kwamba wasipochagua CCM “hawatapata maendeleo.”

Hivi sasa Halmashauri ya Tarime inaongozwa na upinzani. Ina mipango kabakaba ikiwa ni pamoja na kuwalipia karo baadhi ya wanafunzi. Hili ni moja ya mambo ambayo mgombea wa Chadema, Charles Mwera Nyanguru, ambaye pia ni Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, anajivunia sana.

Kutishiwa kunyimwa “maendeleo” ambako CCM imeshikia bango, kunaweza kuwa kichocheo kikubwa cha wananchi wa Tarime kufanya maamuzi ya busara ambayo ni kuchagua Chadema au chama kingine na siyo chama tawala.

Vyovyote itakavyokuwa, askari hawahitajiki katika uwanja wa siasa jimboni Tarime.

(Makala hii imeandikwa kwa ajili ya gazeti la Tanzania Daima Jumapili, 28 September 2008. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)

1 comment

Anastácio Soberbo said...

Hello, I like this blog.
Sorry not write more, but my English is not good.
A hug from Portugal

Powered by Blogger.