CCM YAENEZA UJINGA TARIME
PIGA NIKUPIGE NYUMBANI KWA WANGWE
Na Ndimara Tegambwage
MSIMU wa ujinga umewadia. Ujinga huu unaimarishwa na vitisho kwa njia ya kauli na silaha. Ukitaka uthibitisho nenda Tarime, mkoani Mara ambako unafanyika uchaguzi mdogo wa diwani na mbunge.
Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakiongozwa na Katibu Mkuu Yusuf Makamba, tayari wamefungulia mabomba ya kauli na vitisho kwa shabaha ya kupata ushindi katika uchaguzi huu.
Wanawaambia wakazi wa Tarime kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambacho ni mshindani mkuu, siyo chama bali “kampuni binafsi ya mtu mmoja.”
Wanataka wapiga kura wa Tarime waamini kuwa mbunge wao aliyefariki, Chacha Wangwe, alikuwa kwenye kampuni. Wanataka kupendekeza kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, ama amehongwa au ana ubia katika kampuni hiyo kwa kuwa hajafuta Chadema kwenye orodha ya vyama.
Msimu wa ujinga huu hapa. Waziri Stephen Wasira anaripotiwa akisema, hukohuko Tarime kuwa Chadema ni chama cha mtu mmoja; anamtaja Edwin Mtei.
Huyu anataka kusema kwamba Msajili wa Vyama vya Siasa, ama alihongwa kukiandikisha chama cha mtu mmoja, kwani kinapingana na sheria ya vyama; au ana maslahi nacho ndiyo maana hajakifuta.
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa ananukuliwa akisema Chadema ni chama cha wafanyabiashara wawili. Wanatajwa Mtei na Philemon Ndesamburo.
Msekwa anataka wananchi waamini kuwa mara hii, katika uchaguzi wa Tarime, kila mmoja anaingia tu – mwenye chama, kampuni au duka. Kwa maana kwamba sheria ya uchaguzi haitumiki! Msimu wa ujinga.
Ni Msekwa anayenukuliwa akisema “vyama vingi” vilikuja ili kutoa haki kwa watu wachache (asilimia 20) wakati wengi (asilimia 80) hawakutaka mfumo wa vyama vingi. Hapa anazungumzia Tume ya Nyalali juu ya vyama vingi.
Elimu ya Msekwa na uzoefu ndani ya chama kimoja havimuongozi kuelewa kuwa hodhi ya kisiasa ingeendelea, nchi ingeshindikana kutawalika.
Bali hatushangai. Ni Msekwa aliyetunga kitabu cha kushindilia ukiritimba wa kisiasa kiitwacho “Chama kushika hatamu.”
Haoni kuwa hata hadidu za rejea za Tume ya Nyalali zilikuwa na kasoro kubwa. Kuuliza wananchi kama wanataka chama kimoja au vingi ulikuwa msiba wa kihistoria; hata kama mkuu wa tume alikuwa jaji mkuu.
Tayari wananchi waliishaporwa haki ya kuunda vyama na asasi zao huru. Iweje wananchi waulizwe iwapo wanataka haki yao badala ya mwizi kujisalimisha kwao, akilamba mchanga na kuomba msamaha? Kilichohitajika ni kurejesha mfumo wa vyama bila kupoteza fedha za wananchi na kutubu.
Ni Wassira pia anayenukuliwa akisema Chacha Wangwe, aliyekuwa mbunge wa Tarime (sasa marehemu), alichaguliwa kwa kura nyingi, lakini chama chake cha Chadema hakikuteua mbunge wa viti maalum kutoka Tarime.
Huyu anataka wananchi waamini kuwa kila jimbo ambako CCM inapata mbunge kwa kura nyingi, inateua pia mbunge wa viti maalum. Huu siyo tu uwongo, bali pia uzushi mpevu.
Na huyo Peter Keba, ndugu yake Wangwe, anasema ndugu yake “aliuawa kutokana na kudai kujua matumizi ya ruzuku” ya chama chake.
Naye huyu anataka wananchi, wakazi wa Tarime, waamini kuwa mtu yeyote atakayetaka kujua matumizi ya ruzuku ya Chadema, atauawa au hata Msajili wa Vyama akitaka kujua matumizi ya chama hicho, naye atauawa.
Huo ndio uwanja wa ujinga. Si hayo tu. Viongozi na wapiga chapuo wa CCM wanadai kuwa vyama vya upinzani havina fedha za kuleta maendeleo; kwa hiyo kama wananchi wanataka maendeleo sharti wachague mgombea wa CCM.
Mbegu ya ujinga iko mikononi mwa Katibu Mkuu wa CCM, ambaye tayari amejipa jina la “Yohana Mbatizaji” ambaye anatengeneza “njia ya bwana” – Makamu Mwenyekiti, Pius Msekwa!
Yote haya ni kutafuta kiti cha ubunge na kiti cha udiwani katika jimbo la Tarime. Kila uwongo utasemwa; wakiwapakia wananchi kila sura ya kishawishi ili wapate “ushindi.”
Katika hali ya kawaida, kwa umri na huenda ukomavu uendao na uzoefu, CCM ingekuwa na hoja za maana na kuwa mfano kwa vyama vingine.
Haya yote yanayomwagwa usoni na vichwani mwa wananchi yanatokana na uelewa na imani, kwamba wananchi hawajui; hivyo wataamini tu chochote kile wanachoambiwa na hatimaye kuchagua CCM.
Uwongo na ujinga vinafinyangwa na kusokomezwa katika akili ya wananchi wenye kiu ya kujua. Kumbe ndio wananchi wanapotoshwa. Wanapigwa kafuti ya ujinga na ghiliba ili watawala waweze kuondoka na kiti cha ubunge na kile cha udiwani.
Wakati kuna kilio cha kutoa na kusambaza elimu muwafaka, watawala wanasambaza uwongo, uzushi na ujinga usiomithilika kwa madai ya kutafuta ushindi. Huu ni msiba.
Hakika, wanaoishi kwa tamaa ya kutawala kwa kutumia ujinga wa wananchi, hawawezi kuondoa ujinga. Kwao, ujinga ni mtaji wa kuchukulia madaraka. Ni silaha ya kuulia wapinzani na daraja la kuwapeleka kwenye utukufu wa kisiasa.
Kwa watawala wa aina hii, shule ni adui mkubwa. Elimu ya watu wazima ni kinyamkera ndani ya nyumba. Mijadala ya kutaka kushiriki katika uongozi wa nchi ni adui mtukutu.
Kwa umri huu, CCM wasingekuwa bado wanatamani ujinga. Wasingekuwa wanapenda umma ulioganda kwa propaganda na vitisho. Wasingekuwa wanataka kondoo au umma uliopigwa kafuti za uwongo, uliotishwa kwa silaha au unaogeuzwageuzwa mithili ya chapati.
Chama kikubwa, chenye uzoefu, sharti kiingie uwanjani kwa hoja ili kiwe mfano. Kisipofanya hivyo, basi kisubiri hatma: Nyumba iliyojengwa kwa uwongo, ujinga na vitisho, ni tofali la barafu. Itayeyuka.
(Makala hii imechapishwa katika gazeti la MwanaHALISI, toleo la Jumatano,24 Septemba 2008. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)
1 comment
Kweli mzee wangu nimekubali kuna ujinga hasa ndani ya CCM. Tatizo baadhi ya wazee hawajui zama zimebadilika na wanafikiri enzi za ukomunisti wa Chama kushika hatamu bado tunazo. Wamesahau nyakati lakini mie kama kijana najua tu kilichobakia ni Maulana "Mungu" ataamua kuwazeesha na wataondoka kwenye siasa tu, si mbali sana kutoka leo.
Manake bila kizazi cha baadhi ya wazee wa chama kuondoka madarakani nadhani si rahisi hata nguvu ya umma kuwashinda manake wako tayari kutumia nguvu ya dola.
Mwisho, nadhani wanapaswa kujifunza maana ya siasa za kisasa, hebu waige mfano wa kwa Bwana Mbeki alijiondokea kistaaarabu.
Mwisho nikupongeze sana mzee kwa mchango wako kwa wanajamii.
Usiache kutembelea blog yangu pia, karibu sana.
Post a Comment