VITISHO KWA UHURU WA HABARI
Chenge anavyotishia waandishi
Na Ndimara Tegambwage
SITAKI mwanasiasa Andrew Chenge achoke kusemwa. Sitaki achoke kuandikwa. Hii ni kwa sababu, asipoandikwa atakufa kisiasa.
Kijijini kwa Chenge kuna watu wengi wa umri wake. Wanafahamika kwake na wanakijiji wenzake. Hawajaandikwa na huenda muda utafika watatoweka bila kuandikwa.
Vivyo hivyo kwa wananchi wengine wengi katika makabila na koo zao; katika nyadhifa mbalimbali; katika biashara na uchuuzi; na katika mahusiano ainaaina.
Chenge anaandikwa; lakini siyo kwa kuwa ni Chenge. Hapana. Ni kwa kuwa ni Mbunge. Kwa kuwa alikuwa Waziri wa Miundombinu. Kwa kuwa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimepanga ikulu.
Chenge anaandikwa kwa kuwa ni mjumbe wa Kamati ya Madili ya CCM; alikuwa mserikali muhimu wakati akiwa Mwanasheria Mkuu. Lakini zaidi ya yote, Chenge anaandikwa kwa kuwa ni mwanasiasa.
Kuandikwa ni matokeo ya kuwa na nafasi maalum katika jamii. Mara hii, Chenge amepata nafasi maalum kwa kuwa yote yaliyotajwa hapo juu na hasa kwa kuwa mwanasiasa – kazi ambayo inamuhusisha moja kwa moja na maslahi ya nchi na watu wake.
Mjadala uliopo sasa ni juu ya Chenge kuwa mjumbe katika kamati ya CCM ya “kupitia upya” mkataba wa Umoja wa Vijana wa CCM na mwekezaji katika kuendeleza kitegauchumi cha umoja huo.
Mkataba huo ambao sasa inafahamika kuwa ulishughulikiwa na watu binafsi, na siyo vikao husika, na hivyo kuwepo harufu ya ufisadi, “unaangaliwa” na timu ya viongozi watatu akiwemo Chenge.
Kinachofanywa na vyombo vya habari hivi sasa ni kunukuu na kuchapisha maoni ya wananchi juu ya Chenge kuwa katika kamati ya CCM wakati yeye ni mtuhumiwa katika kashfa ya rada; kashfa iliyosababisha ajiuzulu uwaziri.
Utaona basi, kwamba kushika nafasi ya utumishi wa ngazi alizopitia Chenge, ni kukaa uchi mbele ya kamera na kalamu za waandishi; na kupitia kwa waandishi, ni kukaa utupu mbele ya umma uliomtuma kazi.
Hili ndilo somo kuu juu ya sababu za kuandika wanasiasa – kuanzia yule wa kijijini hadi mpangaji mkuu wa ikulu. Anayelalamika kwa kuandikwa, ama hajui nafasi yake katika jamii au anataka kuendeshea gizani shughuli za umma.
Vyombo vya habari haviundi habari. Habari inakuwepo au vinaichokonoa na vinaiandika, kuichapisha au kuitangaza. Chombo cha habari kinachobuni habari kinajitia kitanzi.
Chombo cha habari kikijiua kinakuwa kimewanyang’anya wasomaji, wasikilizaji au watazamaji wake, nafasi adimu ya kupata taarifa na habari za kuwasaidia kufurahia na kukamilisha uhuru wao wa maoni.
Na taarifa ambazo wananchi wanataka ni juu ya wanavyotawaliwa: haki zao, misingi na taratibu. Ni juu ya tabia na mwenendo wa wanaowatawala wakiwa katika ofisi za umma.
Wananchi wanataka, na vyombo vya habari vinawajibika kuwapa, taarifa juu ya mipango, uadilifu wa serikali, utawala wa sheria au utawala wa mwituni; umakini, uwazi, weledi au upendeleo, ukabila au ufisadi.
Katika kuripoti na kujadili, vyombo vya habari vinagusa wanasiasa na watawala kwa ujumla, siyo kwa majina yao, bali kwa nafasi zao katika kuvunja kiu ya wananchi ya kujua. Hapa, jina kama Chenge ni utambulisho tu wa mwajiriwa wa umma.
Kauli iliyoripotiwa kutolewa wiki iliyopita na utambulisho unaoitwa Chenge, kwamba waandishi wa habari wanamwandika sana na hawamweshimu; na kwamba atawafunza adabu, ni ya kusikitisha.
Kwa mujibu wa ufafanuzi juu ya kwa nini wanasiasa na viongozi wengine waandikwe, iwapo Chenge hataki kuchokonolewa na kuandikwa, sharti aachie ofisi zote za umma zinazomweka wazi kwa kila raia kumjadili na kumtathmini.
Vilevile akitaka kutoandikwa, basi asiingie katika biashara kubwa au ndogo. Kwani, wakati biashara kubwa inahusu maslahi ya nchi na umma kwa msingi wa mapato na kodi, biashara ndogo, hata ya kuuza vocha za simu, inamrejesha kwenye ulingo kuwa ameporomoka zaidi.
Hapa ataandikwa tu. Njia pekee ya kuandikwa na usiyumbe, usikasirike na kughadhabika, ni kutenda kazi yako bila uficho; kutenda haki na kuwa mwadilifu. Ukiwa hivyo na ukaandikwa, utachekelea maisha yako yote.
Kutishia “kufunza adabu” waandishi wa habari, ni kwenda mbali. Ni kukata tamaa. Ni kuloloma kusikoweza kuitikiwa kwa huruma. Ni kutishia kunyamazisha waandishi wa habari.
Aidha, vitisho hivyo vinaashiria kuvunja haki ya msingi ya binadamu – uhuru wa maoni; lakini pia vinaashiria kuvunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayolinda uhuru wa kutafuta na kutawanya habari.
Kama kweli Chenge amesema aliyoripotiwa kusema, basi anashauriwa bure kufanya yafuatayo: Asifute usemi bali asitende alichokusudia kutenda. Hakina tija.
(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili 14 Septemba 2008. Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0713-614872; imeili: ndimara@yahoo.com)
No comments
Post a Comment