Header Ads

LightBlog

WOGA WA WATAWALA

Vitisho kwa waandishi wa habari Iringa


Na Ndimara Tegambwage

SITAKI vitisho vya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Mrisho Said alivyomwaga mbele ya waandishi wa habari mjini Iringa, Jumanne ya 29 Julai mwaka huu.

Amina alikuwa akifungua mafunzo ya wiki moja ya Uandishi wa Habari za Uchunguzi katika Rushwa, Utawala Bora na Matumizi ya Sheria ya Ununuzi Serikalini ya mwaka 2004.

Ilikuwa baada ya mkuu huyo wa mkoa kuwapaka mafuta kidogo waandishi wa habari kwa kusema wao ni mhimili wa nne wa dola, ndipo aliwageukia na kumwaga nyongo.

Kwanza, Amina alilalamika kuwa mkoani mwake kuna waandishi wa habari ambao wanamkera sana kwa kuandika wanavyotaka na kudai kuwa hayo waliyoandika yamesemwa na yeye.

Pili, alisema baadhi ya waandishi wa habari wa mkoani Iringa, bila kutaja majina yao, wanajipachika ‘majina bandia’ na kutawanya habari zao katika vyombo vingi vya habari.

Tatu, Amina aliapa kupambana na waandishi wa aina hiyo kwa kusema, ‘serikali ina mkono mrefu. Mimi nawafahamu tu. Nikisoma habari hii na hii na ile, najua ameandika mtu mmoja kwa kubadili majina tu, lakini nasema, serikali ina mkono mrefu. Nikiwahitaji nitawapata.’

Kauli hii, mbele ya waandishi wa habari waliokusanyika kujifunza jinsi ya kuandika habari za uchunguzi; ukiwemo uchunguzi katika matumzi ya madaraka na dhamana za uongozi, ilikuwa kama kutangaza msiba katikati ya sherehe.

Kwa kuzingatia kauli aliyotoa, mahali alipoitolea, madhumuni ya kusanyiko hilo la waandishi wa habari na ujio wa ziara ya Rais Jakaya Kikwete – siku nne mbele – utaona kuwa mkuu wa mkoa alilenga kupanda mbegu ya woga.

Tukubali basi kwamba hakuna anayepinga mtu kuwa na haki ya kuwa na maoni. Kila mtu pia, ikiwa ni pamoja na mkuu wa mkoa, ana haki ya kusikitika, kukasirika, kulia, kucheka au kulalamika. Hizo pia ni baadhi ya njia za kujieleza.

Lakini kwa mkuu wa mkoa kusubiri darasa la kufundisha wachokonozi katika matumizi ya serikali, rushwa na utawala bora ndimo amwage malamiko na vitisho vya kutumia mkono mrefu wa serikali, hakika ni kwenda mbali.

Haishangazi basi kwamba waandishi wa habari aliotishia walisikika wakikejeli kuwa, ‘Mama huyu ni mwoga; ana mchecheto,” wakihusisha vitisho vyake na hali iliyomkumba siku moja kabla Rais Kikwete kuanza ziara mkoani Iringa.

Usiku wa manane wa mkesha wa siku ya kwanza ya ziara ya rais, Amina alilazwa hospitali kuu ya mkoa mjini Iringa akisumbuliwa na kile madaktari wawili walisema ni ‘matatizo katika kifua.’

‘Nadhani ni mchoko na vumbi,’ alieleza daktari mmoja bila kutaka kufafanua hasa kilichokuwa kinamsumbua mkuu wa mkoa.

Yawezekana ulikuwa mchanganyiko wa mambo mengi: Mchoko uliotokana na mzunguko mrefu kwenye sehemu ambazo rais angetembelea, vumbi, wasiwasi wa ujio wa rais katika mazingira ambayo hayajawekwa sawa, misuguano na malumbano miongoni mwa viongozi mkoani ambavyo vingeonekana wakati wa ziara ya rais.

Mambo mengine ambayo bila shaka yaliongeza mchecheto na huenda kuathiri afya ya Amina ni ‘jeshi’ la waandishi wa habari walioandamana na rais kutoka Dar es Salaam na mkoani wakidhamiria kuanika kila kitu katika ziara hii.

Lakini jingine muhimu ni kuwepo mkoani kwa waandishi wa habari aliowatishia kwa kusema serikali yake ina mkono mrefu wa kuwasaka kwa kuandika kinyume na kile alichosisitiza kuwa ‘maadili ya uandishi wa habari.’

Kwamba tayari Amina amepata afueni na alifanikiwa kuhudhuria angalau kikao cha majumuisho ya ziara ya Rais Kikwete, mengi ambayo yalimfanya awe na mchecheto yaweza kuendelea kuibuiliwa.

Kwa mfano, tayari taarifa zinazohitaji kuthibitishwa zinasema kuna maeneo ambayo hayakuwa katika ratiba ya awali ya ziara ya rais, lakini yaliingizwa baadaye. Haya ni pamoja na Shule ya Sekondari ya Anna Makinda iliyoko kijiji cha Ihanga, Njombe.

Makinda ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Eneo jingine ambalo limetajwa kuwa halikuwa katika ratiba lakini liliingizwa, ni ASAS Dairy Farm – shamba la mifugo linalomilikiwa na mfanyabiashara Salim Abri. Hili nalo Kikwete alilitembelea.

Lakini katika majumuisho yake, baada ya ziara ya karibu wiki nzima, Kikwete aliwataka viongozi wa mkoa, kwenye kikao pekee alichohudhuria Amina, ‘kuongeza ushirikiano’ na kuepuka malumbano ambayo alisema hayasaidii kuleta maendeleo.

Ukiweka pamoja yote yaliyotokea mkoani kabla na wakati wa ziara ya rais; na ukizingatia kile ambacho rais amebaini – kuwepo kwa malumbano na ukosefu wa ushirikiano – mchecheto wa mkuu wa mkoa mbele ya waandishi wa habari ni hali iliyotarajiwa.

Bali hakuna sababu yoyote kwa mkuu wa mkoa yeyote kuwa na mchecheto na hata kutishia waandishi wa habari kwa mkono mrefu wa serikali. Mkono mrefu wa serikali ukamate mafisadi ambao wapo pia mkoani Iringa.

Anachohitaji Amina ni kuweka wazi utendaji wake, kwa kila moja kuona na hata kutathmini na kutarajia waandishi wa habari kuheshimika kwa kuandika ukweli au kuumbuka kwa kuandika uwongo.

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, 10 Agosti 2008.Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)

No comments

Powered by Blogger.