Header Ads

LightBlog

UFISADI SOKONI NA MITAANI

Wanafunzi, mabasi na mafisadi

Na Ndimara Tegambwage

ANGALIA watoto hawa. Ni wanafunzi. Wasichana kwa wavulana. Umri wao ni mdogo. Baadhi yao wana matongotongo. Kuna waliobeba mikoba, madaftari mikononi na nyuso zisizotabirika. Lakini wana lengo moja.

Kuna waliobeba mabango na moja linalosomeka haraka linasema, “…maisha bora kwa kila fisadi.” Wamo katika maandamano jijini Dar es Salaam.

Vichanga hivi vya shule za msingi na sekondari vimevuka mstari. Vimeona wazazi wao wamebaki kimya. Vimeamua kusimama na kupaza sauti kutetea wazazi na kujitetea. Vinasema nauli ya Sh. 100 kwa safari moja kwa mtoto, katika mazingira ya sasa, ni mzigo usiobebeka.

Kama kawaida sauti zinagonga kwenye mwamba na kutoa mwangwi unaoendelea kwa muda mrefu: Nauli! Nauliii! Nnaul…! Nnnau…Nnnna…nnnnn…

Sauti za wanafunzi hao, zikiwakilisha maelfu ya vijana wa rika lao, zinapotelea katika mwangwi kama madai yao yanavyoyeyukia kwenye ahadi za watawala na ujanja wa wafanyabiashara.

Kwa vijana hawa, makali ya ufisadi yanaanzia pale wanaposhindwa kwenda shule au wanapochelewa; wanaposhindwa kutumwa sokoni au kwa ndugu; wanaposhindwa kutembeleana.

Sasa ujumbe wao kuwa maisha bora kwa kila Mtanzania yamechukuliwa na “maisha bora kwa kila fisadi,” hakika umepelekwa na umefika.

Walioandamana ni wanafunzi walewale wadogo, ambao wamekuwa wakishirikishwa katika magwaride, kusoma risala na kukimbiza mwenge. Kauli za maisha bora wamezidaka kwenye mdomo wa watawala na maisha yao ya kila siku.

Kwa nini tusikubali kuwa sasa wanafunzi wameanza kufundishwa kufikiri na kuoanisha maisha na matukio na kuacha kuwa kasuku wa vibandani?

Sasa jambo moja ni wazi: Kwamba tayari watoto wa shule, katika umri wao mdogo, wameanza kujifunza kwa kufikiri na siyo kuwa kama kasuku wa vibandani.

Mabango yao yanaonyesha jinsi ya kuunganisha matukio. Kwa mfano, uhusiano kati ya rushwa na kufifia au kukosekana kabisa kwa huduma za kijamii.

Wanajua ukosefu wa utawala bora unavyoweza kusababisha hata njaa kwa nchi nzima kwa kuwa wananchi hawana fursa za kutenda kwa uhuru.

Wanaelewa kuwa chakula ni suala la ulinzi wa nchi na kwamba kupungua au kukosekana kwa chakula, kama ilivyo kwa kukosekana kwa utawala bora, kunaweza kuzaa maafa ya vita vya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe au kupinduliwa kwa serikali.

Leo hii wanafunzi wanajua kuwa kuwepo kwa mafisadi, wanaojipakulia mabilioni ya shilingi kutoka kwenye chungu cha taifa, kunadhoofisha uchumi na kuua fursa za elimu, tiba na miundombinu.

Wanaelewa kuwa ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi, unaofanywa na wachache katika jamii, unachochea kukua kwa akili butu, zisizo na uwezo wa kufikiri isipokuwa kuiba, kula, kunenepa na kufa kwa magonjwa ya ulafi.

Aidha, wanafunzi wanajua sasa kwamba ukwapuaji huo pia ndiyo njia ya kuchimba makaburi ya mamilioni ya wananchi waliokamuliwa (sio wasionacho kwani wanaporwa kila kukicha); ambao lazima wafe kutokana na ujinga, maradhi na umasikini.

Siyo siri tena kwamba wakati kuna wanaokufa kwa magonjwa yatokanayo na ulafi; ulafi ambao ni uzao wa wizi mkubwa, unyanganyi na ufisadi; kuna wanaokufa kutokana na maradhi yaletwayo na ufisadi.

Wanafunzi pamoja na umri wao mdogo, sasa wanaweza kubaini kuwa mikataba ya kinyonyaji, kwa mfano ile ya nishati ya umeme, inaongeza ugumu wa maisha kwa baba au mama zao.

Wanaona hatua ya serikali ya kukimbia wajibu kwa visingizio vya “serikali haifanyi biashara,” imeacha soko la nishati ya mafuta mikononi mwa walafi – ambao huenda ni pamoja na maofisa wa serikali – na kusababisha mzazi kushindwa kununua hata fungu la mchicha ambalo bei yake imepaa.

Watoto wanasikitika sana. Wakilia wanaona na serikali inalia. Maana yake ni nini? Wanaona kwamba hawana ulinzi tena. Kwamba usalama wao umeyeyuka. Kwamba serikali waliyotarajia kuwa ngao yao nayo imetota.

Tena afadhali kilio cha wengi, wakiwemo wanafunzi, kinachoweza kuleta kisirani au simanzi kuliko kilio cha wachache serikalini ambao wamebainika kuwa miongoni mwa wakwapuaji wakubwa wa fedha za umma na raslimali za taifa.

Wanafunzi katika shule za msingi na sekondari, wanayaona yote haya. Wamezaliwa katika mazingira haya. Wanakulia humo. Hawahitaji kusimuliwa uchungu wake. Wanaujua vema. Wanahitaji nadharia tu ya mapambano ya kuondokana na hali hiyo.

Siku ya Ijumaa, tarehe 1 Agosti mwaka huu, wanafunzi wa Dar es Salaam, kwa niaba ya wenzao mkoani na nchi nzima, walitumia kauli na miguu hadi ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kusisitiza kuwa wao na wazazi wao hawana uwezo wa kulipa nauli mpya.

Nauli haikupunguzwa. Lakini kesho wanaweza kujitokeza kutoa maoni kwa jambo jingine muhimu katika jamii. Ni ishara ya vijana hai; jamii hai inayotolea maoni kila jambo linaloihusu.

Bali duniani kote hakuna mahali ambako kuna mabasi pekee ya wanafunzi isipokuwa katika shule chache sana ambazo huwa na mabasi ambayo gharama yake huingizwa kwenye karo. Wengine wote hutumia usafiri wa umma.

Hapa kwetu kelele za “wanafunzi” zinaletwa na wenye shabaha ya kutaka kupendelewa ili wanunue magari na kuendesha miradi ya kubeba wanafunzi pekee au wanaofikiri serikali itanunua mabasi wapate mahali pa kufanyia ufisadi.

Leo tutafute jibu kwa swali moja: Nauli ya Sh. 100 siyo kwa wanafunzi peke yao. Ni kwa watoto wote. Yakinunuliwa mabasi kwa wanafunzi peke yao, na kufanya kazi siku za shule, watoto wengine watasafiri vipi? Wakati wa likizo wanafunzi watasafirije?

Halafu angalia uchovu huu wa aina yake. Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam anasema kwa kuwa wanafunzi watalipa Sh. 100, basi waketi kwenye viti!

Kwa wenye mipango mizuri ya usafiri mijini, viti vichache – kama 15 hivi katika basi kubwa – huwa vya wajawazito, wenye ulemavu, wagonjwa na vikongwe. Wengine hupanda, husimama na kushuka. Mwanafunzi atakaa vipi?


(Makala hii imechapishwa katika gazeti la MwanaHALISI la 13 Agosti 2008. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)

No comments

Powered by Blogger.