Header Ads

LightBlog

SERIKALI INAPOKIRI UPUNGUFU KWA UKALI

Wanajeshi, dalalada na manyanyaso

Na Ndimara Tegambwage

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi amekuwa mmoja wa mawaziri wanaosema ukweli.

Katika kipindi cha 1995 hadi 2000, mawaziri waliokuwa wasema ukweli walikuwa wakihesabika na tangu hapo kumekuwa na ukame.

Kazi ya mawaziri imekuwa kuficha ukweli, kunyamaza, kusema nusu uwongo au uwongo mkuu na kutetea serikali hata pale ambapo hapahitaji utetezi.

Miaka hiyo, walioongoza kwa kukiri makosa ya serikali, kutojua, kukubali kukosolewa au kusema ukweli, walikuwa Dk. Aaron Chiduo na Bujiku Sakila.

Dk. Chiduo alikuwa Waziri wa Afya na Sakila alikuwa Naibu Waziri wa Elimu. Hawakusita kutamka kuwa hilo serikali hailijui, haijalitenda na haina mipango ya kulifanya. Walikuwa wakweli.

Naye Dk. Mwinyi kajiunga na wasema ukweli wachache. Sikiliza kauli yake bungeni wiki iliyopita kuhusu askari wa Jeshi la Wananchi (JW) na usafiri wa daladala. Kapasua. Bila woga. Bila shinikizo.

Waziri amekiri kuwa wizara tayari imeandaa bajeti yake; haingewezekana kuirekebisha wakati huo alipokuwa akiwasilisha hoja bungeni ili kuweka fungu la nauli ya askari.

Kauli hiyo inaweza kuchambuliwa kama ifuatavyo: Kwamba serikali haina utaratibu wa kufikiria nauli ya askari. Kwamba si utamuduni wa serikali kupanga bajeti ya usafiri wa askari.

Kwamba wizara/serikali imezoea kusahau kuweka bajeti ya usafiri. Kwamba wizara haijawahi kuona umuhimu wa fungu la usafiri wa askari katika bajeti yake. Kwamba serikali haijui mazingira mabaya yanayowakabili askari.

Lakini inawezekana pia, kama anavyosema Dk. Mwinyi, kuwa wizara haina fedha. Amenukuliwa na vyombo vya habari akisema, wakati huu serikali haina hata uwezo wa “kuwaongezea askari fedha za kujikimu.”

Hili la ukosefu wa fedha ni jibu la kuchonga la serikali ambalo hufukuliwa mvunguni na kutolewa kwa kila anayedai utekelezaji unaohitaji fedha.

Ni hapo ambapo waziri alionekana kuunganisha mawili – ukosefu wa uwezo wa kuongeza fedha za kujikimu na ukosefu wa fungu la nauli – na kusema kuwa kujadili suala la nauli wakati huu ni “kuleta mkanganyiko katika jamii.”

Ni waziri anayeongeza kuwa serikali haina uwezo wa kujenga nyumba za kutosha kwa askari wake katika makambi yao au kutoa usafiri kwa askari kutoka walipo hadi sehemu zao za kazi na kurudi.

Hadi hapa, waziri amekiri upungufu, udhaifu, usahaulifu na pengine kutowajibika, katika mambo makuu yafuatayo:

Kwanza, kushindwa kwa serikali kuona umuhimu wa kupanga fungu maalum kwa ajili ya usafiri wa askari kutoka wanakoishi hadi vituo vya kazi na kurejea makazini kwao.

Pili, kushindwa kwa serikali kujenga nyumba za kutosha kwa askari katika makambi yao nchini.

Tatu, kushindwa kwa serikali kuongeza kiwango cha fedha za kujikimu kwa askari wa JW.


Mambo haya matatu aliyosema Dk. Mwinyi bungeni, mara nyingi huchukuliwa kuwa nyeti na siri. Lakini bunge ni mahali ambako lazima waziri amwage chozi ili kupata alichopanga kupata.

Hii ni fursa adimu kwa wananchi na hasa waandishi wa habari kumegewa taarifa hizi ambazo zinasaidia katika uchambuzi wa tabia na mwenendo wa serikali hata katika mambo yanayohusu ulizi wa nchi.

Ukweli unabaki palepale. Wananchi wanajua baadhi ya matatizo ya askari kwa kuwa askari ni watoto wao, ndugu zao, baba, mama, kaka na dada zao.

Bali katika suala la matumizi ya usafiri wa daladala, hata kama waziri hatataka wananchi waendelee kujadili; kule kuendelea kutumia usafiri huo hakika kunamomonyoa hadhi ya askari, jeshi na serikali yenyewe.

Mara nyingi mimi husafiri kwa mabasi ya daladala. Ndani ya basi kuna viti vitatu au vinne visivyo na abiria. Mnakaribia kituo kingine cha mabasi ambako kuna askari watatu na mwanafunzi mmoja.

Sikiliza kauli za yule wanayemwita kondakta wa basi: “Kuna nuksi hapo. Wanga hao. Simamia mbele kuleee,” anamweleza dereva. Mwanafunzi na askari wanaitwa nuksi. Wanaitwa wanga. Wanaitwa mikosi.

Askari anakimbiwa. Au askari anaonekana kama ombaomba kwa magari madogo, pikapu au malori. Anazomewa na wale ambao wasingeweza kumzomea maishani. Anachelewa kazini. Jumla: ananyanyasika.

Itabakia kuwa kweli kwamba askari ananyanyasika pale anapopanda magari kwa kubahatisha; kwa kuitwa majina machafu; kwa kuitwa “ombaomba wa lifti.”

Majeshi ni vyombo vya ulinzi vya dola. Vyombo vya dola haviwezi kutegemea kufanya kazi zake kwa fadhila za wafanyabiashara wakubwa na wadogo na kwa kubeuliwa na wale ambao wanategemea huduma ya majeshi hayohayo.

Vyombo vya ulinzi vya dola vikiwa na tabia ya kuomba au kutegemea “wema” wa mtu binafsi, vinaweza kupoteza ujasiri wake wa ulinzi na hata kutia hatarini usalama ambao vinatakiwa kuulinda.

Na askari anayesimamisha magari 10 hadi 20 ndipo apate wa kumbeba, huku mabasi madogo yakimpita na kummiminia kejeli nyembamba, atakuwa amechoka sana, kimwili na kisaikolojia, pindi afikapo eneo la kazi.

Hapa kuna mazingira yaliyojitokeza na kuruhusu jamii kujadili hadhi na heshima ya askari. Kuna mazingira pia yaliyosababisha waziri kutoa maelezo ya kweli juu ya kushindwa kwa serikali kukidhi mahitaji ya askari.

Muhimu ni kwamba sasa waziri na serikali wanatambua kuwa askari wananyanyasika. Raia na askari wanasubiri; wanataka kuona hatua zinazochukuliwa kuondoa hali hiyo mara moja.

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la MwanaHALISI toleo la Jumatano, 27 Agosti 2008. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872 na imeili: ndimara@yahoo.com)

0713 614872

No comments

Powered by Blogger.