Header Ads

LightBlog

UFISADI ULIOKUBUHU

EPA na watuhumiwa wasioonekana

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI kubishana na Rais Jakaya Kikwete kuhusiana na hatua aliyochukua kuhusu watuhumiwa wa ufisadi wasioonekana.Kwani mjadala ndio umeanza.

Pamoja na mambo mengine, Kikwete amesema amedaka watuhumiwa. Wamerudisha sehemu ya fedha walizokwapua. Amewanyang’anya pasipoti na kukamata nyumba na magari yao.

Aliliambia taifa na dunia, kupitia hotuba yake bungeni, Alhamisi wiki iliyopita, kuwa watuhumiwa wawe wamerejesha kiasi chote cha fedha walizokwapua kabla ya Oktoba 31, vinginevyo watapelekwa mahakamani.

Mpaka hapo nani hataki kumsikiliza rais? Masikio ya wengi yalikuwa yamejiandaa kusikia atasema nini juu ya wizi katika akaunti ya EPA ndani ya Benki Kuu (BoT).

Katika kupambana na rushwa na ufisadi, kile alichotangaza rais ni hatua ndogo sana, tena ya kutamanisha tu. Kuna hatua kubwa na shirikishi ambazo ni msingi wa mapambano haya.

Tujadili hatua moja ya msingi. Hii ni ile ya kutangaza majina ya watuhumiwa, makampuni yao, mahali wanakoishi, zilipo nyumba zao zinazoshikiliwa na serikali, biashara zao, magari yao yaliyokamatwa na mahali yalipoegeshwa.

Hatua hii ni muhimu kwa kuwa vita vyovyote dhidi ya rushwa na ufisadi ni vita vya umma; vinavyohusu jamii nzima. Hii ni kutokana na ukweli kwamba matokeo ya rushwa na ufisadi yanaathiri jamii nzima.

Jamii ingependa kuwajua watuhumiwa, tena kwa majina yao; lakini kubwa zaidi, jamii ingependa kuona “mapapa wa ufisadi” wakiburuzwa mahakamani na hatimaye kuona wanapewa adhabu kubwa ikiwa ni pamoja na kifungo.

Jamii ingependa kuona watuhumiwa hawakingiwi kifua kwa sababu zozote zile, hata visingizio vya “haki za binadamu.” Hakuna popote ambako haki za binadamu zinaruhusu wizi au aina yoyote ya ufisadi.

Mambo haya mawili, kutajwa hadharani kwa majina ya watuhumiwa na kufikishwa mbele ya sheria, huwapa imani wananchi kuwa serikali yao ipo, ni makini, inafanya kazi yake na haitavumilia ufisadi.

Hatua hii hufanya wananchi kuwa na hamu na nia ya kushiriki katika kutoa taarifa za kufichua mafisadi. Huamini kuwa wanaowahujumu wao na taifa lao, wakikamatwa watachukuliwa hatua.

Wananchi ni pamoja na asasi za kijamii. Asasi hizi zina nafasi kubwa katika kuangaza njia ya jamii na kuiongoza katika kufikiri na kutenda.

Asasi ambazo zinahusika na mapambano dhidi ya rushwa; zinazoshughulikia elimu na malezi; zinazojitambulisha na masuala ya demokrasi na utawala bora, ni sehemu nyingine ya jamii iliyoko vitani dhidi ya rushwa na ufisadi.

Kuongezeka kwa hamu ya kushirikiana na serikali katika mapambano haya; kukua na kupanuka kwa shughuli zao katika eneo hili; na kufumuka kwa fikra mpya juu ya mbinu na mikakati dhidi ya ufisadi, hutegemea wanavyoona serikali inawajibika.

Hakuna mahali popote duniani ambako serikali imefaulu kupambana na rushwa na ufisadi bila kushirikisha wananchi – mmojammoja na katika makundi na asasi za kijamii. Hakuna!

Vilevile hakuna popote pale ambako wananchi peke yao au na asasi zao, wamepambana na rushwa na ufisadi na kushinda bila kushirikisha serikali.

Utashi na mamlaka ya serikali ni muhimu katika mapambano haya na utashi utajidhihirisha kwenye hatua ambazo serikali inachukua.

Hatua hizo ni pamoja na kuweka wazi kila kitu: Nani mtuhumiwa wa ufisadi, yuko wapi, kachukua nini na wapi, kapelekwa mahakamani na kachukuliwa hatua gani.

Hakuna mahali ambako rais amewahi kushinda ufisadi kwa kutumia wapelelezi wake wa siri; kupata taarifa ya siri, kukamata watuhumiwa wa siri, kukusanya fedha za siri na kuzihifadhi kwenye akaunti ya siri. Hakuna.

Hakuna kokote duniani ambako rais amefaulu kupambana na ufisadi kwa yeye kuwa mkamataji watuhumiwa, mwendesha mahojiano, mkusanyaji fedha, mtoaji misamaha; tena kwa watuhumiwa wasioonekana. Hakuna.

Hatua kama hiyo haisaidii kukuza mapambano dhidi ya rushwa; haisaidii kujenga msingi wa mapambano, wala haionyeshi kuwa serikali ina nia nzuri.

Badala yake, hatua hiyo inachafua sura ya serikali katika mapambano haya. Inasaidia kujenga mazingira ya kuishuku serikali na watawala, kwamba huenda hata wao wanahusika katika ukwapuaji.

Vita vyovyote dhidi ya rushwa na ufisadi sharti vifanywe kwa uwazi na katika uwazi. Pasipo uwazi ni kukomaza rushwa, ufisadi na uhalifu. Kwa ufupi, ni kushiriki ufisadi. Mjadala ndio umeanza.

(Makala hii itachapishwa katika Tanzania Jumapili, 24 Agosti 2008. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872 ma imeili: ndimara@yahoo.com)

No comments

Powered by Blogger.