Header Ads

LightBlog

AINA NYINGINE YA UFISADI

'MACHINGA COMPLEX' NA LONGOLONGO YA KISIASA

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI Machinga Complex kwa kuwa itazaa mgogoro utakaozaa migogoro itakayozaa migogoro isiyoisha na kuwa mfano mbaya kwa nchi nzima.

Machinga Complex ni kitu kikubwa kinachoitwa Jengo la Wafanyabiashara Wadogo lililoko Dar es Salaam ambalo Rais Jakaya Kikwete aliweka jiwe lake la msingi Ijumaa wiki hii.

Tunaambiwa ni machinga watakaokuwa katika jengo hilo la thamani ya Sh. 10 bilioni kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na linalotarajiwa kukamilika Novemba mwaka huu.

Wazo la kujenga Machinga Complex lilitokana na mawazo ya watawala kwamba ‘Jiji la Dar es Salaam limechafuka.’ Limejaa takataka lakini pia limejaa uchafu unaotembea; maduka yanayotembea (machinga).

Wakati wageni wa kitaifa wanapotangaza kutembelea nchi, maganda ya mihogo na miwa, machinga, plastiki zilizotumiwa, ombaomba na mikokoteni, vyote hufagiwa kwa shabaha ya kusafisha jiji kabla wageni hawajawasili.

Swali likazaliwa. Uchafu ulioko sehemu moja unaweza kukusanywa haraka. Uchafu unaotembea je? Wazo likazaliwa: Ukusanyiwe kwenye jengo moja litakaloitwa Machinga Complex. Hapa ndipo tumefikishwa.

Takwimu zinasema jengo lina uwezo wa kuchukua wafanyabiashara wadogo wapatao 10,000. Hapo ndipo hoja zinapoanzia.

Wafanyabiashara ndogo ni akina nani? Biashara ndogo inaanzia shilingi ngapi? Nani anajua thamani ya biashara ya wafanyabiashara ndogo? Nani anajua idadi ya wafanyabiashara ndogo jijini Dar es Salaam na idadi imepatikana kwa vigezo vipi vya biashara ndogo?

Tunaambiwa Machinga Complex inajengwa kwa fedha za NSSF. Bila shaka hiki ni kitega uchumi. Kama hivyo ndivyo, hii ni biashara ya aina yake. Ni nipe nikupe.

Katika hali hii wafanyabiashara ndogo tunaowajua, wale wasaga lami kuanzia alfajiri ya saa 11 hadi usiku wa manane, watapata wapi fedha za kulipia pango kwenye jengo la ghorofa sita?

Hata kabla hawajafikiria suala la pango, nani atafikiria wasaga lami kuwa sehemu ya jengo la kisasa: wao na marapurapu yao; wao na jasho lao; wao na makatambuga yao au pekupeku – bila kiatu wala ndala?

Kuna mifano michache hapa ya kuangalia. Nenda soko la Kjitonyama, wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam. Hakuna ghorofa. Hakuna mmeremeto. Ni jengo na vituti vya kuuzia bidhaa. Nani hakumbuki kilichotokea pale lilipofunguliwa?

Wenye fedha walichukua karibu nafasi zote katika soko; wakilipa kiasi kilekile kinachohitajika kulipwa. Wakahodhi soko. Ndipo wakaanza biashara ya kuuza nafasi hizo kwa bei isiyoshikika.

Asitokee mtu akadai kuwa hajui kilichotendeka Soko la Sterio Temeke. Ni yaleyale ambayo yalitokea Kijitonyama. Hodhi ya karibu nafasi zote au zilizoko maeneo mazuri na baadaye kuziuza kwa bei ya juu.

Hayo ni madai hai hadi sasa. Waliokumbwa na mkasa huo bado wana la kusimulia. Na bado kuna wanaodai kuwa mabanda yaliyojengwa kuzunguka shule nyingi Dar es Salaam yamehodhiwa na wenye fedha na kuuzwa baadaye kwa kiwango cha kufuru.

Ndiyo maana maneno ya Machinga Complex hayawatui hata machinga wenyewe. Kama walikuwa sehemu ya takataka, na ‘dampo’ linalojengwa ni la dhahabu, wao watatupwaje katikati ya utajiri?

Kama wenzao, wauza mihogo na mboga, walishindwa kupata nafasi katika masoko ya pembezoni, kutokana na wenye fedha kuhodhi maeneo mengi na nyeti kibiashara, wao wataingiaje ghorofani hata kabla mtoto wa mkuu wa wilaya au mkoa hajapewa nafasi?

Ni maswali yanayotokana na mazingira na mazoea jijini na nchini kwa ujumla. Chukua mfano wa Benki ya Makabwela (NMB). Hakuna mkurugenzi au hata mfanyakazi wa benki hiyo anaweza akasema ile benki ni ya makabwela. Hayupo!

Sababu ni kwamba siyo ya makabwela. Basi. Ni benki ya biashara isiyokuwa na ukabwela wowote. Wenye akaunti humo ni wafanyabiashara, maofisa serikalini na makapuni mbalimbali binafsi.

Wengine wenye akaunti ni na wale ambao waajiri wao wamewaambia wafungue akaunti zao kule au wanaolazimika kuchukua mikopo kupitia benki hiyo. Ukabwela uko wapi?

Kabwela hana shati. Anaazima la rafikiye. Kabwela hana kitanda. Analala chini au kwa kugawana na mwenzie. Kabwela hana akaunti benki wala ajira. Kabwela gani anamiliki benki kama siyo dhihaka?

Machinga Complex itakuwa kama Benki ya Makabwela. Ni longolongo ya kisiasa ya kukidhi haja iliyopo tena kwa wakati uleule tu. Machinga – ule uchafu unaoleta kinyaa mitaani wakati wageni wanapotembelea jiji – utakaaje ghorofani?

Lakini tusiishie hapo. Ni machinga wangapi walioko jijini hivi sasa? Wanaingia wangapi jijini ambao watakuwa machinga kesho? Kiwango cha uingiaji mijini vijana wa kuwa machinga katika miaka mitano ni kipi?

Kuna wasioanza moja kwa moja na umachinga. Dereva na karani aliyefukuzwa kazi. Mfanyakazi wa nyumbani aliyepewa ujauzito na mwajiri na kutupwa mitaani. Ni wengi. Ni wengi.

Mradi wa machinga utasimama kwa miguu yote? Abbas Kandoro atakuwa shahidi.

(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la MwanaHALISI la Alhamisi 20 Agosti 2008. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872 na imeili: ndimara@yahoo.com)

No comments

Powered by Blogger.