Header Ads

LightBlog

WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA ATAYAWEZA HAYA?

Na Ndimara Tegambwage

HAKUNA anayetaka kumfundisha kazi waziri mkuu mpya, Mizengo Pinda. Ninachojua ni kwamba amekubali uteuzi na anajua anachotakiwa kufanya. Akiboronga, tunaye!

Bali kuna mambo kadhaa ya kumkumbusha ili ayaweke karibu na orodha ya majukumu yake ya kila siku na hasa baada ya kuthibitika kwa ufisadi katika mkataba kati ya serikali na kampuni ya "kubuni" ya Richmond Development Corporation.

Kwamba waziri mkuu, pamoja na mambo mengine, ahakikishe serikali yake inatambua, inaheshimu na kulinda uhuru wa mtu mmojammoja au vikundi, wa kuwa na maoni tofauti na watawala. Asijiingize katika kutaka tuwe na sare ya fikra.

Kwamba serikali yake itambue na kulinda uhuru wa watu wa kutoa maoni yao bila woga wala aibu, na kwamba serikali ijifunze kuheshimu mawazo ya wananchi, mmojammoja au vikundi, hata kama haina nia ya kuyafanyia kazi.

Kwamba waziri mkuu mpya atambue uhuru wa habari; na katika eneo hili, tusisitize uhuru wa wananchi kupata taarifa na uhuru wa vyombo vya habari kukusanya na kutawanya habari/taarifa bila kushinikizwa kwa njia ya vitisho au hongo za fedha au ahadi za vyeo.

Katika hili, ule mtindo wa kukusanya waandishi wa habari, kuwauliza wataandikaje habari za waziri mkuu na hata kufikia hatua ya kuwaelekeza jinsi ya kumpamba, utokomezwe kabisa na katika nafasi yake ijengeke tabia ya Mizengo Pinda kujiamini na kuacha waandishi na wananchi wamwone Pinda kama anavyoonekana.

Kwamba serikali ina wajibu wa kuchangia elimu pana ya waandishi wa habari. Hii ni elimu katika nyanja mbalimbali na katika taaluma ya habari ambayo itajenga jeuri ya waandishi, kuwaondolea woga na kuwashikisha zana za vita dhidi ya ufisadi.

Kwamba Mizengo Pinda atasimamia, pamoja na mambo mengine, kupatikana kwa jamii inayoongea bila woga wala aibu; inayotunga kidole jichoni mwa viongozi na watawala na kusema, “Hili siyo sahihi.”

Umuhimu wa mazingira huru ya aina hii umedhihirika wakati wa mapambano ya kuthibitisha kuwa mkataba kati ya serikali na Richmond ulighubikwa na upendeleo na vitendo kadhaa vya kifisadi; na kwamba hata waliotarajiwa kulinda maslahi ya umma walizama katika kutafuta maslahi binafsi na kuzamisha zaidi wananchi katika dimbwi la ufukara.

Kwamba waziri mkuu mpya atapokea, kama alivyokwishakiri, mchango maridhawa wa vyombo vya habari katika kupigania haki, uwazi na ukweli; na kushiriki kwa njia ya uwezeshaji – hasa kielimu – wa waliomo katika taaluma ili kulinda ujasiri huo usimomonyoke.

Kwamba, kwa waziri mkuu mpya kutambua umuhimu wa uhuru wa habari na waandishi wa habari, atahakikisha kwamba serikali inaweka mazingira ambamo waandishi wazalendo, wanaopigania ukweli, haki na maslahi ya taifa, hawamwagiwi "tindikali" wala kukatwa mapanga wakiwa katika vyumba vya habari au popote pale kutokana na habari wanazoandika au staili ya uandishi wao.

Kwamba Mizengo Pinda ataheshimu uhuru wa wananchi wa “kujenga mashaka” juu ya mwenendo wa watawala wao; na kwamba ni mashaka hayo yaliyowezesha ufuatiliaji hadi ikagundulika kuwa mkataba kati ya Richmond na serikali ulikuwa kaburi jingine la jasho na damu ya walipakodi wa nchi hii.

Kwamba serikali itaanza kufikiria upya utoaji wa matangazo yake kwa magazeti na vyombo vingine vya habari vya watu binafsi.

Matangazo ni chanzo muhimu cha mapato katika kuendesha vyombo vya habari. Kwa serikali kuvinyima matangazo vyombo binafsi; imekuwa ikivijengea mazingira ya kufa wakati fedha hizo za serikali zinatokana na kodi ya wananchi ambayo ulipaji wake haubagui wananchi kwa misingi ya vyama vya siasa, itikadi wala jinsia.

Kifo cha vyombo vya habari, viwe vya serikali au vya watu na mashirika binafsi, ni kifo cha uhuru wa maoni na uhuru wa kutoa mawazo. Kwani uhuru wa habari na uhuru wa kutoa mawazo hukamilika pale mawazo yanapochapishwa au kutangazwa na kutawanywa.

Kwamba Mizengo Pinda, baada ya kutambua mchango wa kauli za wananchi, waandishi na vyombo vya habari, atakwenda mbele zaidi na kufaya yafuatayo, hasa kuhusu kampuni ya Richmond:

Kwanza, kuhakikisha kuwa serikali inaanzisha mchakato wa kusimamisha mkataba kati yake na kampuni ya Richmond kwa msingi mkuu kwamba wahusika katika kampuni hiyo walisema uwongo na waliingia katika ubia na wananchi ili kukamua uchumi wa nchi hii.

Madai kwamba mkataba ukisitishwa serikali itafikishwa mahakamani, ni kama kumtishia mtu mzima kwa nyau. Woga wa kushitakiwa ni sehemu kubwa ya mkakati wa ufisadi; na serikali haina budi kukataa kutishiwa.

Pili, wananchi wanatarajia kuona waliohusika na ujambazi huu wa kiuchumi wakichukuliwa hatua za kisheria. Hatua hizi ni pamoja na kuwakamata, kuwahoji na kuwafikisha mahakamani kujibu mashitaka ambayo mpaka sasa ni wazi kabisa.

Kinachohitajika hapa pia ni kutaka kurejesha serikalini, fedha zote ambazo serikali iliishaweka kwenye mradi huu unaoendelea kueleweka, kila kukicha, kuwa wa kitapeli.

Hatua nyingine ni kutathmini mali za wote waliohusika katika uchafu huu wa kuangamiza taifa, zinazoshukiwa na, au zilizothibitika kutokana na mradi wa Richmond Development Corporation na kuzitaifisha.

Tatu, kuhakikisha kwamba mapendekezo yote ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu kampuni ya Richmond yanatekelezwa. Hili litampa waziri mkuu, heshima mbele ya wananchi, serikali yake na jumuia ya kimataifa.

Nne, waziri mkuu mpya ajifunze kuwa “kikulacho kinguoni mwako.” Kwamba waliobuni au walioshinikiza au waliopendelea kile kinachoitwa kampuni ya Richmond kupata mkataba na serikali ni baadhi ya viongozi serikalini.

Vilevile wanaoongoza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), iliyosema “hakuna hasara iliyopatikana kwa upande wa serikali” kutokana na kutoa mkataba kwa kampuni ya Richmond, nao ni wateule wa rais.

Hilo la uteule lisiwape kinga. Wananchi wanasubiri kuona, kwamba katika mapambano dhidi ya rushwa, angalau kwa mara ya kwanza, anakamtwa sangara na kukaangwa kwa mafuta yake mwenyewe. Kazi hii Pinda anaiweza.

Kwa msingi huo, kitu muhimu hapa, mbali na sheria za udhibiti, ni kuweka mazingira yatakayohakikisha kwamba mambo yote yanayohusu serikali yanafanywa kwa uwazi na, au yanapohitajiwa na wananchi, yanawekwa wazi.

Sitarajii kuwa haya ni mengi ya kumchosha Mizengo Pinda. Bali wananchi wanaangalia serikali itafanya nini leo kuwadhihirishia kuwa iko makini na inastahili kuendelea kuwatawala.

(Makala hii imeandaliwa kwa ajili ya gazeti la MwanaHALISI toleo la 13 Februari 2008. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)

4 comments

zemarcopolo said...

Ndimara hii makala safi sana. sasa nakuomba kwa dhati utufanyie utafiti wa kutosha kuhusu kinga aliyokuwa nayo Rostam Aziz nchini Tanzania mpaka anaachiwa bila kuguswa pamoja na tabia yake ya kukataa kuhojiwa na kamati teule na kuonekana ni kiini cha dhuruma hii kwa watanzania...zemarcopolo

N N said...

Hawa ni wa kuangalia;
http://video.google.com/videoplay?docid=-1583154561904832383,
http://video.google.com/videoplay?docid=-7336845760512239683.
Sasa angalia jinsi makaburu wa kiyahudi wa natawala ulimwengu, sasa wanainvest Tza kwa nguvu zote. Watatatulia pesa zote huku tukifa kwa njaa.
Wananunua ardhi, wannaunua makampuni yetu wanatumalizia nchi hawa.
http://khanverse.blogspot.com/2008/02/diamonds-are-4eva.html

N N said...

unajua kwa nini kuna ujeuri ulimwenguni?? Ona hii:
http://iamthewitness.com/books/Protocols.in.Modern.English.htm

ndimara tegambwage said...

Nawashukuruni nyote kwa maoni na maelekezo. Nimeeleweka zaidi kwa mails mlizonielekeza kusoma.

Asante tena.

Powered by Blogger.