Header Ads

LightBlog

ULAFI NA TATIZO LA USAFIRI WA WATOTO TANZANIA

SITAKI Na Ndimara Tegambwage

SITAKI kuandika kwa kujirudia lakini ninaolenga kuelimisha wakionyesha kuwa hawajaelimika, nitarudia, kurudia na kurudia. Hivi ndivyo nifanyavyo sasa.

Somo lenyewe ni dogo: Ni usafiri wa wanafunzi katika jiji la Dar es Salaam na miji na majiji mengine. Ni somo lililochukua saa nzima ya kipindi cha Kipima Joto cha Independent Televisheni (ITV), juzi Ijumaa usiku.

Kipindi hiki kilitawaliwa na maswali: Nani anawajibika kusafirisha wanafunzi kwenda na kutoka shuleni na hatua gani zinachukuliwa kumaliza tatizo hilo.

Kipindi kilimalizika kwa msiba mkubwa. Hakuna jibu lililotolewa. Hata Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ludovick Mwananzela hakuwa na maelezo muwafaka.

Washiriki wote waliogelea katika nauli ya Sh. 50 kwa mwanafunzi kuwa ni kiasi kidogo kisicholeta faida; na umuhimu wa kuwa na kampuni za kusomba wanafunzi peke yao. Huu ni mkasa.

Katika nchi zenye mipango mizuri ya uchumi, na ambamo huduma au biashara ya usafiri na usafirishaji inaitwa “usafiri wa umma,” hakuna msamiati uitwao “mwanafunzi.” Msamiati pekee unaotumika na kuheshimika, ni “abiria.”

Katika mazingira hayo, mwanafunzi ni abiria. Mwanamke ni abiria. Mwanaume ni abiria. Mnene ni abiria. Mwembamba ni abiria. Mfupi ni abiria. Mstaafu ni abiria. Mfanyakazi ni abiria. Mwenye ulemavu wa aina yoyote ile ni abiria.

Lakini katika Tanzania, mwanafunzi siyo abiria. Ni mwanafunzi tu; kitoto cha kusumuka huku na kule; kupiga, kufukuza, kuchania vitabu au ikiwezekana, kuacha vituoni ili kuepuka “hasara.”

Hiyo ndiyo dini ya madereva na makondakta wa mabasi ya daladala na huenda baadhi ya wamiliki wake. Ni: Achana na watoto wa shule, wanaleta hasara kwa kulipa nauli ya shilingi 50.

Na hii ni kutokana na mfumo wa sasa wa umuliki wa mabasi. Kila mwenye fedha ya kununulia basi, kubwa au dogo, ananunua na kuliweka barabarani. Huyu aweza kuwa tajiri mwenye mtaji mkubwa, askari, mfanyakazi, mstaafu, mporaji “aliyetajirika jana,” mjane, yatima au hata aliyeokota fedha jana au aliyeshinda bahati nasibu.

Kila mwenye gari anatafuta kondakta na dereva anayemfahamu na kumkabidhi chombo. Kilichobaki ni kukinga mkono na kupokea mavuno ya barabarani. Basi.

Katika ushindani huu, wafanyakazi wa gari la “tajiri” wanataka nauli kubwa inayokamilisha haraka kiwango walichowekewa na tajiri. Kwa hiyo mwanafunzi anayelipa Sh. 50, ni balaa, ni kero. Kondakta anataka nauli ya mtu mzima.

Kwa kuwa mabasi ya daladala yanaongozwa na kusimamiwa na tabia binafsi ya mmiliki, dereva na kondakta, lazima mwanafunzi atakuwa ukoma au uchuro au kero ya kudumu.

Ni hivi: Kama mabasi ya daladala, au vyovyote vile yatakavyoitwa mabasi yanayotoa huduma ya umma, yangekuwa chini ya usimamizi mmoja, msamiati wa “mwanafunzi” ungekuwa umekufa na kuzikwa zamani.

Mabasi yote yangechomekwa chini ya mamlaka moja; kwa mikataba maalum inayozingatia ubora wa gari, muda wa kutoa huduma chini ya mamlaka na viwango vya mapato kila mwezi, suala la “mwanafunzi” lisingekuwepo.

Kungekuwa na masuala ya kisera na utekelezaji tu, kwamba watoto wa umri fulani hulipa nauli kiasi gani na wakubwa hulipa kiasi gani. Basi. Kwa msingi huo, kusingekuwepo msamiati wa wanafunzi na unyanyasaji tuuonao leo, kwani kuna hata watoto wasioenda shule ambao wanastahili kusafiri.

Kwa maana hiyo, gari likibeba wanafunzi wengi au wachache, haitakuwa ajabu wala hasara; ni basi la mamlaka ya usafirishaji. Aliyebeba watu wazima watupu na aliyebeba watoto kwa bei iliyowekwa kisera, wote wameingiza mapato katika mamlaka hiyohiyo.

Umiliki wa aina hii, wa kampuni moja au mbili; wa ushirika au utawala wa jiji au mji, ndio pekee uwezao kurejesha hadhi na kulinda haki ya watoto wanaokwenda na kutola shuleni au wanaokwenda sehemu yoyote ile.

Katika kipindi cha Kipima Joto, Naibu Waziri alisema kuna mwekezaji mmoja ambaye ameanzisha kampuni ya kusafirisha watoto peke yao kwenda shule na kurudi makwao na kwamba wizara yake imemsaidia katika maeneo kadhaa.

Kampuni hii au mengine yenye lengo kama hilo, hayataondoa tatizo la unyanyapaa wa wanafunzi kwa misingi ya viwango vya nauli.

Kampuni hizo zitakuwa zimelenga kuchuma mahali penye ushindani mdogo lakini zitakuwa zimewatenga wanafunzi na watoto wengine. Je, wasiosoma lakini ni watoto watasafiri vipi?

Niliwahi kuandika kwamba mabasi ya daladala “hayana mwenyewe,” kwa maana ya kutokuwa na utawala wa pamoja. Kila mwenye shughuli huweza kuchomoa gari lake na kwenda zake, huku abiria wakitaabika.

Magari ya daladala yaweza kunufaika na mpango wa kuwa chini ya mamlaka moja; kubeba abiria na siyo “wanafunzi,” na kwa njia hiyo kusitisha unyanyasaji wa watoto. Hii ni iwapo yatakuwa chini ya mamlaka kwa njia ya mikataba.

Faida nyingine ya kuwa chini ya mamlaka ni kwamba magari yakiharibika, mamlaka inayatengeneza; yanapangiwa madereva stadi na makondakta wenye ujuzi; yanalazimika kufuata kanuni na sheria na hivyo kujenga utamaduni bora wa matumizi ya barabara.

Leo hii ni vurugu mechi. Kuendelea na utaratibu huu au ule wa “kusomba wanafunzi peke yao,” ni kuendeleza unyanyapaa wa watoto na wanafunzi. Ni kuvunja haki za binadamu.

(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, 28 Januari 2008. Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)

No comments

Powered by Blogger.