Header Ads

LightBlog

MWANDISHI 'ANAYEFICHA' HABARI

SITAKI

Na Ndimara Tegambwage
SITAKI mwandishi wa habari anayeficha habari. Huyu ni rafiki yetu wa siku nyingi, Said Nguba ambaye amekuwa mwandishi wa habari wa Waziri Mkuu kwa miaka miwili sasa.

Katikati ya wiki hii, Nguba alinukuliwa na vyombo vya habari akikiri kutoalikwa waandishi wa habari kwenye makabidhiano ya ofisi kati ya Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa na yule wa sasa, Mizengo Pinda.

Eti hakukuwa na habari katika tukio hilo ndio maana hakuita waandishi, lakaini alipeleka picha ya tukio hilo ikionyesha Lowasss ana Pinda wamekumbatiana; tena kwa kicheko cha “pasua mbavu.”

Katika hili, mwandishi mwenzetu Said Nguba ametuonea. Ametuficha “dhahabu ya habari.” Ametunyima fursa kuu katika maisha ya kisiasa. Ametuweka gizani – waandishi, wasomaji, watazamaji na wasikilizaji wa vyombo vya habari.

Kwa ujumla, Nguba ametupokonya haki yetu ya kuwa mashahidi wa tendo la kihistoria. Lakini lisilokubalika hata kidogo ni kile kitendo cha kufanya shughuli za serikali katika kiza nene.

Mawaziri na naibu mawaziri walikabidhiana kwa uwazi kabisa na hotuba zao kutangazwa. Kwa nini waziri mkuu wa zamani anyimwe au akoseshwe fursa ya kusema lolote alitakalo mbele ya kadamnasi anapokuwa anakabidhi ofisi kwa waziri mku mpya?

Inawezekana wahusika wakuu hawakutaka “kuvamiwa” na waandishi wa habari; hivyo waliamuru wasiitwe. Hapo ndipo penye udhaifu.

Waandishi wa habari wanaoteuliwa au wanaopelekwa kufanya kazi serikalini, wakiwa waandishi wa rais, waziri mkuu, makamu wa rais au idara yoyote ile, kama waandishi wengine, wanapaswa kuwa wataalam.

Utaalam wao hauishii kwenye kuandika tu habari za wakubwa zao, bali hata kuwashauri juu ya jinsi ya kusema wanachotaka kukisema, lini kisemwe ili kipate uzito unaostahili; na kisemwe katika mazingira yapi ili kiwe na uzito uliolengwa.

Muhimu zaidi, waandishi hao wa “wakubwa” huwa na kazi nyingine, na labda muhimu kuliko kuandika habari za wakubwa; nayo ni kuelimisha na kushawishi wakubwa zao kuelewa umuhimu wa vyombo vya habari wakati wote.

Hili ni jukumu la kuwatoa kizani watawala, kwa kuwafundisha na kuwafafanulia polepole na hatua kwa hatua, kwamba ofisi zao ni ofisi za umma na kamwe hazipaswi kutenda kizani.

Kwamba kufanya mambo kwa uficho wakati umo katika ofisi ya umma, ni kujiingiza katika vitendo vya ushirikina ambavyo havipaswi kufanyiwa katika ofisi za umma.

Kuelimisha na kushawishi kwamba kwa kuwa macho ya umma ni vyombo vya habari, na kazi zinazotakiwa kufanywa ni za umma, basi vyombo hivyo viitwe wakati wote; viwepo na kushuhudia kila kinachotendeka.

Natumia neno “viitwe” kutokana na kutokuwepo uhuru wa kutosha wa waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari “kuparamia” ikulu wakati wowote wanapotaka habari.

Tumeona mara kadhaa, ikulu au ofisi ya waziri mkuu, ikibagua waandishi pale kunapokuwa na suala la kueleza wananchi kupitia vyombo vya habari. Ofisi hizi zimeshiriki kujenga “matabaka” ya waandishi kwa matumizi na manufaa ya watawala.


Aidha, hakuna utaratibu wa kuwa na waandishi kutoka vyombo mbalimbali ambao ni wawakilishi wakazi wa ikulu na ambao hudonoa kila kinachodondoka kutoka mdomoni na mikononi mwa watawala.

Inawezekana hatujafikia hatua hiyo kutokana na watawala kuogopa vyombo vya habari au kufanya mambo mengi yaliyo kinyume na yanayotakiwa ofisini; au kutokana na kutojua au uzembe wa washauri kuhusu masuala ya habari pindi wanapoteuliwa.

Lakini, hata baada ya kusema hayo yote, iko wapi nafasi ya mwandishi wa waziri mkuu kusema kwamba “hakukuwa na habari” katika tukio la kukabidhiana ofisi – kati ya Lowassa na Pinda?

Sitaki kumrudisha darasani mwandishi wa waziri mkuu. Kwa hiyo nitasema machache. Kwamba tayari mwandishi wa mkubwa amekuwa mkubwa na anatenda kama “wakubwa” wanavyotenda.

Anaamua na kuwaamulia wengine kwamba hapa kuna habari na pale hakuna habari. Hili ndilo kosa kubwa; ndiyo hujuma kuu ya mwaka huu kwa wananchi, vyombo vya habari na waandishi wa habari.

Kila ninapoingia darasani kufundisha waandishi wa habari wanafunzi, na hata wakongwe, naanza kwa kuwaambia umuhimu wa kuona zaidi ya wengine wanavyoona; kusikia zaidi ya wengine wanavyosikia; na kupaanza sauti kutawanya kilio cha wengi kuliko wengine wanavyofanya.

Hii ina maana moja kuu; nayo ni kwamba siyo kila mmoja ataona jambo lilelile kwa njia ileile na msisitizo uleule. Tuchukue mfano wa makabidhiano ya Lowassa na Pinda.

Wote wataona wawili wakikabidhiana mafaili; wakiwa wamesimama. Wataona wanakumbatiana kama picha ambayo Nguba alituma kwenye vyombo vya habari. Wataona “tabasamu za kisiasa.” Watasikia hotuba za wahusika.

Lakini kuna watakaoona zaidi: Jicho jekundu la mmoja wa wahusika. Kusitasita wakati wa kutoa kauli yake. Chozi lililoning’inia katika jicho la kulia. Mgegemo wa midomo na mashavu. Haraka ya kumaliza tukio.

Si hayo tu. Macho ya huruma ya mmoja wao. Uchangamfu au mdhoofiko. Mashaka. Woga. Aibu. Tabasamu ya kutunga. Ung’avu wa macho na uso kwa ujumla kunakoashiria kupata au kukosa. Mataumaini au kukata tamaa.

Wengine wataona ujasiri usiomithilika machoni mwa wote au mmoja wao. Watatunga yote haya na kuandika habari kwa ujazo unaostahili. Kwa mtazamo wa chombo chao cha habari. Kwa mtindo wa uandishi wautakao. Hiyo ndiyo kazi na utamu wa uandishi.

Kukimbia waandishi wa habari, au kushauriwa kuwaficha tukio kubwa kama la makabidhiano ya ofisi ya waziri mkuu, kwa madai kwamba hakukuwa na habari, ni kuusaliti uandishi wa habari.

Zaidi ya hapo, ni kuendeleza utamaduni wa serikali kufanyia kazi zake gizani. Ukitaka ongeza hili: Ni kukataa kufanya kazi ya kuelimisha watawala juu ya umuhimu wa habari.

(Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com) Makala itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili ya 24Februari 2008)

1 comment

SIMON KITURURU said...

Kufichana habari huku ndio kunakoongezea kuharibu imani ya wananchi kwa serikali yao.

Powered by Blogger.