DK. NGASONGWA NA MACHOZI YA PAPA
SITAKI Na Ndimara Tegambwage
SITAKI Dk. Juma Ngasongwa, yule Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji astuke leo hii kwamba uchumi wa nchi umeshikwa na wawekezaji kutoka nje.
Kwani ushikwe na nani? Kwa miaka kumi sasa
Watanzania wameshuhudia kasi isiyomithilika ya watawala kuuza kila kitu kilichoitwa “mali ya umma” kana kwamba wametumwa kufuta msamiati huo na chochote kile kilichosimamia dhana hiyo.
Damu ya walipakodi na jasho la wananchi wote kwa ujumla, vimechuruzikia katika mabenki, maofisi, mifuko na midomo ya watu binafsi kutoka nje ya nchi.
Hili halikufanyika kwa misingi linganifu ya kibiashara, bali kwa taratibu zinazoonyesha kana kwamba watawala walikuwa wanajiondolea kero. Uuzaji damu na jasho la wananchi uliwekewa kalenda kana kwamba usipofanyika katika kipindi maalum, basi watawala wataadhibiwa.
Ubinafsishaji nchini ulifanyika mithili ya uuzaji nguo kuukuu sokoni au mitaani. Kwa mtindo huo, mashirika na makampuni ya umma – yale mazao ya damu na jasho la wananchi – yakawa kama matambara yawezayo kununuliwa kwa bei yoyote ile iliyotamkwa na mnunuzi, hata kama ni ndogo kukaribia kuwa bure.
Leo hii, Waziri Ngasongwa anasema, “Tulibinafsisha kwa nia njema,” na kuharakisha kuongeza kuwa ubinafsishaji huohuo umefanya watu wa nje, siyo tu kushika bali hata kutawala “uchumi wa nchi.”
Kuuza mali ya umma kwa watu kutoka nje ya nchi, ni kuuza damu na jasho la wananchi. Ni kuuza mali iliyochumwa na wananchi; na mara hii bila kuwashirikisha katika maamuzi.
Kuuza mali ya umma hadi hatua ya kutambua kuwa sasa uchumi wa nchi, kupitia nyanja ya uwekezaji, uko mikononi mwa wageni, ni kuuza nchi na kufanya watawala wetu kubakia na kazi ya kuchunga mali ya wawekezaji.
Ubinafsishaji wa aina ya Tanzania umekuwa wa aina ya kusaidia uporaji wa mali ya umma na raslimali za nchi, kwa kasi ambayo ilikuwa haijawahi kuonekana nchini. Ni ubinafsishaji unaopaswa kujengewa mashaka; kama kweli wahusika walilenga kuneemesha taifa au walitaka kuchuma kwa mkondo huo.
Leo hii Dk. Ngasongwa ndio anakumbuka “wazawa.” Alisema Alhamisi wiki hii kwamba serikali inaandaa mipango ya kuwezesha wananchi wawekezaji ili waweze kushika uchumi wa nchi yao. Alisema hiyo inafanywa kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC).
Kauli ya Ngasongwa ina maana gani katika mazingira ya sasa? Kwamba serikali ndiyo imezinduka? Kwamba serikali ya sasa inasikitishwa na hatua ya serikali iliyopita ambayo iliuza nchi kwa kasi ya moto wa kiangazi?
Ngasongwa anamsemea nani? Mipango hiyo ipo kweli au anatangaza hisia zake? Je, yawezekana kuna aina ya kujirudi serikalini na kwamba mawaziri sasa waweza kukiri, kutubu na kuomba msamaha?
Katika suala la ubinafsishaji, ilitazamiwa kwamba serikali ingekaa chini na kuangalia jinsi ya kukuza uwezo wa uwekezaji wa ndani kabla ya kuita wawekezaji kutoka nje.
Wawekezaji kutoka nje, wanaokuja kwa kasi tuliyoshuhudia nchini na ambayo waziri anaanza kustukia, wana uwezo wa kuchochea au kuendeleza rushwa, kufinyaza ajira, kulaghai juu ya mapato na hivyo kutolipa kodi kamili au kutolipa kabisa; au kuishia kwenye kulipa mirabaha.
Baya zaidi, wawekezaji wengi wa aina ya wale walioingia Tanzania, na kwa kasi na mfumo walioingilia, waweza kushirikiana na waliowawezesha kuingia, kudumaza na hata kufuta kabisa uwezekano wa kuibuka na kukua kwa uwekezaji wa ndani ambao ungekuwa endelevu na mkombozi wa taifa.
Ni baada ya serikali kuuza makampuni na mashirika ya umma yaliyochangiwa na kila raia kwa njia mbalimbali, ndipo inastuka na kusema kwamba ilisahau wazawa. Ni leo inasema kuwa inataka kuwaandalia mpango chini ya NDC.
Hii ni aibu. Lakini pia ni jinai. Wazawa wamenyang’anywa chao; hicho walichopata kwa damu na jasho lao na kwa pamoja kama taifa. Wameachwa kwenye mwamba wa ufukara na matarajio haba.
Siyo rahisi kuamini kwamba NDC itafanya maajabu. Shirika hili limekuwepo kwa miaka mingi. Ubinafsishaji wa kasi umelikuta na kasi imeisha na kuliacha palepale.
Kama ni kujenga nguvu na uwezo wa Shirika la Taifa la Maendeleo, kwa maana halisi ya jina hilo, uimarishaji wake ndio ungetangulia ubinafsishaji ambao umeweka uchumi mikononi mwa wageni.
Nguvu za uwezeshaji NDC zinatoka wapi wakati mashirika na makampuni ambayo lingesimamia ili yajenge nguvu ya ndani ya nchi ama ni mizoga au yako mikononi mwa wageni?
Sitaki kusema serikali haiwezi kubadili mkondo wake. Nasema imechelewa. Sitaki kusema anayosema waziri hayawezekani. Nasema mazingira ya sasa ni magumu mno kuliko ilivyokuwa na leo hii hakuna cha kusalimisha.
Sitaki kusema wazawa hawawezi kuinuka na kuchukua nafasi yao. Nasema utawala wa sasa hauonekani kuwa na lengo, shabaha na sera hiyo. Uzawa unakuwa mtamu kuimba majukwaani lakini wakati ukiwadia mwekezaji wa nje anakumbatiwa.
Mashirika, makampuni na raslimali nyingine za taifa vimeuzwa kwa watu wa nje. Serikali imekataa au imeshindwa kusaidia wazawa hadi maziwa na asali vyote vimekombwa na wageni.
Tunachoshuhudia ni mamilioni ya Watanzania na watawala wao kuwa katika nyarubanja: wanalima, wanapalilia, wanavuna na kuhifadhi. Wanasubiri mwenye shamba aje kuchukua mazao; labda na kuwaachia bakshishi.
Huo ndio utumwa tuliomo. Ngasongwa anajua hili vema. Je, NDC iliyopuuzwa kwa miaka mingi itaweza?
(Makala hii itachapoishgwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, 03 Februari 2008. Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)

No comments
Post a Comment