Header Ads

LightBlog

RAIS KIKWETE NA 'WAFANYABIASIASA'

Na Ndimara Tegambwage
RAIS Jakaya Kikwete ametangaza nia ya kuwa na sheria ya “Wafanyabiasiasa.” Hii ni sheria kizibo. Inalenga kuzuia tabia ya “mshika mbili.”

Kama unataka uongozi wa kisiasa, basi ukabidhi biashara yako kwa wadhamini hadi mwisho wa kipindi cha uongozi wako. Kama unataka biashara, usubiri ukomo wa kipindi chako cha uongozi kisiasa ndipo uanze kufukuzia shilingi.

Leo hii serikali yake imejaa hao tunaowaita “wafanyabiasiasa” – wale wanaochanganya biashara na madaraka ya kisiasa kwa wakati mmoja.

Ni hoja nzuri. Lengo ni muafaka, bali uwezekano wa kuziba udenda wa siasa kuvujia kwenye biashara; na kuzuia mtononoko wa tamaa ya biashara kuvujia kwenye siasa, ni mdogo sana.

Katika mazingira ya sasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho Kikwete anaongoza, wafanyabiashara ndio “tajiri wa chama.” Tuseme “wenye fedha” ndio roho ya chama kiuchumi.

Mieleka iliyoendeshwa kwa mabilioni ya shilingi katika chaguzi tatu kuu zilizopita na majigambo ya “ushindi wa kishindo,” vimeingiza taifa katika mashindano ya fedha na siyo siasa kwa misingi ya itikadi, sera na ajenda za maendeleo.

Katika mazingira hayo, mwenye fedha, awe mfanyabiashara wa kweli au “mwizi” aliyethibitika machoni mwa wengi, anaweza kushika uongozi. Kaidi wa kuelewa hili aulize mwananchi mmojammoja.

Nasema wenye fedha kwa kuwa hakuna anayetaka kujua fedha zimetoka wapi. Popote zilikotoka, halali au haramu, zikitawanywa kama njugu, mtawanyaji anashinda uchaguzi na huweza kuambulia madaraka zaidi, kwa mfano uwaziri.

Aliyekuwa na biashara akipata uongozi serikalini anakuza biashara yake; aliyekuwa na fedha akipata uongozi, anaanzisha biashara, kwani chanzo chake cha fedha za awali kinaweza kukauka. Hapa ndipo kuna ugumu wa kazi anayojipa Kikwete.

Rais anasema anataka afanyie marekebisho ile sheria ya maadili ya viongozi ili kuzuia walioko katika uongozi kuendelea kufanya biashara na wanaoingia kwenye uongozi kuanza kufanya biashara.

Kwanza, hadi sasa kauli ya rais ni kauli tu. Inaweza kutumika kwenye mijadala mirefu na isiyoisha. Baadhi ya wanasiasa wanaweza kupendekeza kuwa kuwepo utaratibu wa kutafuta maoni ya wananchi juu ya suala hilo. Miaka inaweza kuja na kupita.

Pili, kauli tu ya rais tayari imezaa “roho mbaya.” Wenzake ambao walikuwa naye katika mbio za kutafuta urais wake, wameanza kusema, “Rais anataka kutusaliti.” Wengine wanasema tayari amewatelekeza.

Miongoni mwa wale ambao aliwateua kushika uongozi serikalini na walioko bungeni, Rais Kikwete anajua nani ana biashara ipi. Anajua nani ana mali au fedha kiwango gani. Zaidi ya yote, anaweza kuwa anajua nani alimchangia kiasi gani.

Aidha, rais anajua ni akina nani wenye kilio kikubwa kuhusiana na biashara, mali au fedha zao. Akiona huruma au akiogopa kuchukua hatua, kwa misingi ya kutotaka kusaliti au kutelekeza “wenzake,” basi atavuta miguu.

Hapo ndipo tutashuhudia mchakato wa kuleta mabadiliko ya sheria ukikawia kuanza; au hata kama utaanza, siyo leo wala kesho; au hata kama utaanza kesho, utakwenda goigoi au vitazaliwa visingizio; hatimaye hoja itazeeka na kufa kabla ya wakati wake.

Hapa Kikwete atalazimika kuamua kati ya mawili: “Kusaliti” agano na wafayabiashara ambao sasa ni wafanyabiasiasa wenye nafasi za utawala au kusaliti umma wa nchi hii unaotarajia utawala usio na doa.

Tatu, Kikwete ameanza kusikia sauti, aghalabu za chinichini, ndani ya chama chake, zinazosuta na kukemea mwenendo wa jeuri ya wafanyabiasiasa, hasa mawaziri na watumishi wengine serikalini. Kutosikiliza sauti hizo kunaweza kumnyang’anya kete muhimu kisiasa.

Nne, rais hajapata shinikizo la kutosha kutoka nje ya chama chake kuhusu umuhimu wa kuondokana na wafanyabiasiasa. Shinikizo hilo linatarajiwa kutoka kwa wafanyabiashara waaminifu, asasi za kijamii na vyama siasa.

Iwapo rais atasubiri kushinikizwa na sehemu hizo za jamii, atakuwa amepoteza fursa mwanana kwa kiongozi wa nchi kuchukua hatua bila kushinikizwa kwa migomo, kauli kali na hata maandamano.

Kwa mfano, mgomo wa aina yake ulioendeshwa na wabunge wa Bunge la Jamhuri mjini Dodoma, wa kukataa kumsikiliza waziri na kukataa kujadili hoja kuhusu umeme, ni moja ya majanga ya kisiasa yawezayo kumpata rais anayeogopa kuasi wafanyabiasiasa.

Tano, inawezekana kabisa rais alikuwa na malengo maalum katika kuwateua wafanyabiashara kuingia serikalini na alikuwa akijua kuwa nafasi zao zitaleta mgongano wa maslahi. Je, sasa malengo hayo yametimizwa?

Lakini rais anaweza kuwa ameemewa na katika hilo anataka kuonyesha kuwa ana mamlaka ya kutenda kile ambacho wananchi wanatarajia kutoka kwake.

Kwa hiyo, shinikizo ndani ya chama chake, malalamiko ya wananchi, mgomo bungeni, utendaji wa mashaka wa watuhumiwa na woga wa kimbunga cha upinzani, vinaweza kumsukuma rais kuchukua hatua.

Bali katika mazingira ya sasa, siyo rahisi marekebisho ya sheria ya maadili peke yake kuwa dawa ya kukabililiana na ufisadi, mgongano wa maslahi na rushwa vitokanavyo na wafanyabiasiasa.

Kwani hata kabla rais hajafanya marekebisho ya sheria, wafanyabiasiasa wanafahamika kuwa na makampuni mengi, biashara nyingi na mali nyingi chini ya majina ya watoto wao, wake/waume zao, ndugu zao na marafiki zao.

Tayari kuna uhusiano wa aina ya kipekee miongoni mwa wafanyabiasiasa. Aliyeko wizara ya nishati aweza kusaidiwa na aliyeko Kilimo, wakati wa Elimu aweza kumwinua aliyeko Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa. Ni nikune hapa nitakukuna pale.

Marekebisho ya Kikwete hayawezi kuona hili. Anayeng’olewa kwa ufanyabiasiasa, tayari amejenga mkondo – kuanzia kwa rais, hadi waziri mwenzake, hadi katibu mkuu wa wizara, hadi mbunge ambaye ni mjumbe wa bodi ya wakurugenzi, hadi mtendaji wa kata ambako anataka kipande kikubwa cha ardhi.

Tuchukulie kwamba sheria imeyataja maeneo yote. Hoja mpya inakuja: Nani anafuatilia kuona haya yanatendeka? Mbona hata sheria inayotakiwa kurekebishwa imeshindikana kusimamiwa na imekaa kama kolokoloni mwenye rungu na ambaye pia amelala usingizi wa pono?

Ni kweli Kikwete ameogopesha wengi kwa kauli yake, lakini waliokaribu naye wanajua la kufanya, wakati waliombali naye wanatafuta pa kuanzia.

Sheria ya Kikwete haitafanikiwa hadi watawala wametambua, kuhesimu, kuthamini na kulinda uhuru wa jamii wa kufikiri na kutoa maoni. Huko ndiko chimbuko la taarifa na mamlaka ya kukabiliana na ufisadi.

Ninazungumzia jamii huru inayozungumza bila woga wala aibu. Asasi huru za kijamii zenye uwezo wa kuibua hoja na taarifa. Vyombo huru vya habari vyenye macho, masikio na midomo ya nyongeza; na vyama vya siasa vinavyojua wajibu wake kwa jamii katika maandalizi ya kuleta mabadiliko.

Hapa sharti pia uwe na serikali sikivu. Inayopokea taarifa na kuchukua hatua. Iliyo tayari kukosolewa na kulinda watoa habari. Inayokiri mamlaka ya wananchi.

(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la MwanaHALISI toleo la 6 Februari 2008. Mwanndishi anapatikana kwa simu: 0713 614872 na imeili: ndimara@yahoo.com)

No comments

Powered by Blogger.