Header Ads

LightBlog

MIAKA 46 YA UHURU WA TANGANYIKA

Kilio kwenye sherehe za uhuru

SITAKI awepo wa kusema kwamba kwa umri wa miaka 46 ya uhuru wa kisiasa wa Tanganyika, “hakuna kilichofanyika.” Sitaki!

Atakuwa anakataa kuona mengi ambayo watawala wamesimamia au wamepuuza kusimamia. Kwani “kufanyika” ni pamoja na kupuuza, kusahau, kuzembea na kukataa kufanya kilichostahili kufanywa.

Acha wenye uwezo na sababu za kuimba nyimbo za wasifu kwa watawala kwa kile walichofanya, wafanye wapendavyo. Wenye dukuduku hapa na pale walitoe; nasi wenye uelewa kuwa kila walichofanya watawala ulikuwa wajibu wao, acha tulenge penye upogo.

Kwamba kwa miaka 46 ya uhuru wa kisiasa wa Tanganyika, Wabarbaig, taifa dogo kaskazini mwa nchi hii, bado wanaswagwa kama wanyama kutoka makazi yao ya miaka nendarudi. Sababu? Watawala wanataka kutoa eneo kwa “wenye fedha” kutoka nchi za nje.

Ni wimbo gani wataimba Wabarbaig hawa katika kuadhimisha miaka 46 ya uhuru? Nani malenga wa “magugu-watu” awezaye kupeperusha midomo yake kusifu kisichosifika. Hapa kuna malenga wa vilio.

Nani kasema ni Wabarbaig peke yao? Kuna kilio kutoka kila pembe ya nchi. Penye rutuba siyo tena mahali pa wananchi kuishi. Rutuba imeleta balaa. Mtanganyika anag’olewa kama gugu na mkoloni mpya anasimikwa kwa lugha ya “mwekezaji.”

Rutuba imekuwa balaa kama madini na vito vya thamani vilivyokuwa balaa. Sikiliza kilio cha wakazi wa Buhemba, mkoani Mara. Waliswagwa kutoka makazi yao ya miaka mingi; wakapoteza mashamba, shule, zahanati na uasili wao.

Waliowang’oa na kuwatupa pembeni, waliwaahidi maziwa na asali, pindi mgodi wa Buhemba, waliodai ni wa serikali, utakapoanza kufanya kazi.

Miaka sita ilipita. Wachimbaji wakachimba. Dhahabu wakabeba. Mgodi sasa umefungwa. Wachimbaji wamekimbia kwa madai ya kufilisika. Wananchi hawajapata chochote. Bado wanalia na kusaga meno.

Yuko wapi malenga wa Buhemba? Ataimba nini ili sauti yake ichanganyike na kurandana na sauti za wanaosifu watawala kwa miaka 46 ya uhuru. Ni madimbwi ya jasho; ni mito ya machozi. Haihitajiki kwenye sherehe.

Nenda kote kwenye machimbo ya dhahabu na almasi katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Kagera na Mara. Ni masimulizo hayohayo ya kutia simanzi.

Waliopaswa kuwa walinzi wa mali na uhai wa Watanganyika “waliopata uhuru” miaka 46 iliyopita, ndio wamewatangulia matajiri; wakiwasha moto wa risasi kufukuza magugu-watu ili “waungwana” waitwao wawekezaji, waweze kuchota dhabu na almasi bila kelele wala mikwaruzo.

Watanganyika hawa, wanaoswagwa kwa moto wa risasi, wanashuhudia hata mchanga wa nchi yao ukipakiwa kwenye ndege ziyeyukiazo angani, huku zikiacha vumbi liletalo maradhi na umasikini wa kutaga mayai.

Ziko wapi ndimi za kusifia watawala? Ziko wapi koo za kupitishia sauti nyororo za kukumbukia kuondoka kwa Twaining, gavana wa mwisho wa Uingereza nchini hapa? Zitoke wapi nderemo na vifijo kwenye mwamba huu wa ufukara, vitisho na michirizi ya damu?

Nani atasimama na kusema watawala hawakufanya chochote katika miaka 46 ya uhuru? Hana macho? Hana masikio? Hafikiri? Anataka aambiwe kwamba anatumia “miwani ya mbao” – ule usemi wa rais mstaafu Benjamin Mkapa? Athubutu.

Waulize vijana waitwao wana-Apolo na wenzao wengine katika machimbo ya tanzanite. Kama ilivyo kwenye dhababu na almasi, uchimbaji wao mdogo, na kwa muda mrefu, ulibadili maisha yao.

Kuna waliojenga nyumba; tena nzuri. Wengi walisomesha watoto wao. Kuna walionunua magari na wengine kuweza kuwa na biashara kubwa baada ya mauzo na biashara hizo kunufaisha wananchi wengi katika mkoa wa Arusha (sasa Manyara) na mikoa ya jirani.

Leo hii, kutokana na tanzanite kuvamiwa na kampuni kubwa za nje, tena kwa muda mfupi, mapato ya mchimbaji mdogo yamepungua, mategemeo yake kwa muda mrefu yametoweka na utajiri kutokana na tanzanite umehamishiwa Afrika Kusini, nchi za Asia Mashariki na Ulaya.

Hizo ndizo hasara za uchimbaji wa kiwango kikubwa kwa kutumia kampuni kubwa za nje zilizoingia kwa mikataba ya kinyonyaji. Utajiri unafyonzwa. Nchi inaachiwa maandaki na ufukara usiomithilika.

Leo hii, wachimbaji wadogo waliodhihirisha utajiri wa nchi yao kwa kuinua maisha yao, sasa wanaendelea kufukarika kila kukicha. Na tayari wenye migodi mikubwa wametangaza kuwa zao hilo, linalopatikana Tanzania peke yake, limepungua sana. Linaisha.

Kwa wale ambao utajiri wao wa asili, tanzanite, umechimbwa mbele ya macho yao na kutokomezwa katika matumbo ya ubeberu na wao kubaki masikini kuliko walivyokuwa miaka 46 iliyopita, wana wimbo gani wa wasifu kwa watawala?

Nenda mikoa ya kanda ya Ziwa Viktoria. Wananchi wanaoishi kuzunguka ziwa hilo, kwa miaka nendarudi, wamenufaika na ziwa hilo. Wamevuna samaki kwa ajili ya chakula na biashara pia.

Uvuvi mdogo umewawezesha kupata kitoweo, kufanya biashara ndogo na kuweza kulinda maisha yao. Leo ni tofauti. Kwa miaka 15 sasa, wavuvi wadogo wameonekana kama wavuvi haramu. Waulize wao. Watakwambia ziwa liliuzwa tangu zamani. Ni kweli.

Wavuvi wakubwa, kwa kutumia ngazi za utawala katika vijiji, kata, tarafa na baadhi ya wilaya, wamedhibiti uvuvi mdogo kiasi kwamba wananchi wanaoishi kuzunguka ziwa wanakuwa na hamu ya kula samaki wa Viktoria kama walioko maili 2000 kutoka ziwa hilo!

Simulizi za kweli za waliopigwa kwa kukutwa na samaki; waliolemazwa kwa kipigo na waliokufa kutokana na hasira za kuazima kutoka kwa wenye makampuni ya uvuvi, zimeenea kanda nzima. Ni majuto.

Matokeo yake ni kwamba wenye biashara kubwa ya samaki ndio wameamua wenye ziwa (wananchi) wale nini. Wanavua kwa wingi. Wanachomoa minofu. Wanaisafirisha nchi za nje. Yale mabaki – mifupa – (mapanki), ndiyo wanawatupia wananchi.

Ni mapanki ambayo wananchi wanapigania na kung’oana meno wakitafuta kupata mnuko wa samaki wa ziwa lao.

Uko wapi mdomo uwezao kuimba wasifu wakati wa miaka 46 ya uhuru wa Tanganyika? Wamwimbie nani? Wamwimbie nini? Kwa lipi? Kwa kuwanyang’anya ziwa na samaki wao? Kwa kuwaunganisha na kunguru kugombea mapanki?

Kilio ni kikubwa. Kipo katika matumizi ya misitu na maliasili na raslimali nyingine za taifa hili. Sitaki kuamini kwamba wananchi waliomo katika mazingira yote haya wana chochote cha kusifia utawala.

Wanachojua wananchi wengi ambao hawako kwenye utawala ni kwamba wao ni tabala la mwisho. Tabaka la kwanza limejijengea mahekalu ambamo mume anaishi na mke wake, mtoto na mbwa mkubwa mweusi! Nani atasema watawala hawakutenda? Walitenda walichotaka.

Walichonacho wananchi wengi ambao hawako kwenye utawala, ni uhai na dhamira kwamba mapambano yanaendelea. Wingi wa miaka (46), wakati wanaendelea kuona kiza, ndio kichocheo kikubwa katika harakati hizo. Soma alama za nyakati.

(Makala hii imeandikwa kwa ajili ya toleo la Tanzania Daima Jumapili, 9 Desemba 2007 safu ya SITAKI. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872, imeili: ndimara@yahoo.com)

No comments

Powered by Blogger.