Header Ads

LightBlog

MAHAKAMA YA KAZI YENYE MIGOGORO NA WAFANYAKAZI

JAJI MKUU NA AJIRA YA VIBARUA

Na Ndimara Tegambwage

JAJI Mkuu Agustino Ramadhani ametonesha vidonda. Kitendo chake cha kukutana na madereva na kusikiliza dhiki zao, kimezua adha kwa baadhi ya walioongea sana kikaoni.

Vidonda vilivyomwagiwa chumvi nyingi ni vya madereva Hoseah Mahenge na Godlove Ngilangwa; wote watumishi wa Mahakama ya Kazi jijini Dar es Salaam. Mahusiano yao na waajiri wao yametajwa kuwa “yanatota.”

Madereva hawa wamo katika ajira ya mahakama kwa takriban miaka mitano sasa. Wanalipwa mshahara wa Sh. 48,000 kwa mwezi na kwa muda wote huo, wamebaki vibarua. Hawajaajiriwa (!?).

Kinacholeta uzito katika suala la vibarua hawa ni kwamba mahakama inayowaajiri ndiyo imeundwa maalum kwa kazi kuu ya kushughulikia mashauri ya waajiriwa na waajiri – Mahakama ya Kazi.

Swali linaloulizwa na wengi ni, vipi Mahakama ya Kazi, inayopaswa kusimamia haki miongoni mwa waajiri na waajiriwa, inaweza kuwa katika kinachoonekana kuwa mgogoro wa kazi?

Swali jingine ni, Mahakama ya Kazi itakuwaje mfano bora kwa waajiri wengine na watumishi inaopatanisha, iwapo yenyewe, kama mwajiri, nyendo zake zinagongana na misingi ya ajira?

Labda tuulize swali jingine hapa: Kama Mahakama ya Kazi inaweza kumweka mtumishi kwa miaka mitano akiwa kibarua, jambo ambalo halikutarajiwa, nani awe msuluhishi, au hata mwamuzi?

Kumbe Jaji Mkuu ameanzisha utaratibu wa kukutana na kada mbalimbali katika utumishi wa mahakama. Mara hii alitaka kukutana na madereva ili kujua mazingira ya kazi zao na matatizo yanayowakabili.
Ni hapo, mbele yake, vilipomwagwa vilio vya madereva.

Hiyo ni miezi minne iliyopita. Madereva wa mahakama walikaa chumba kimoja na jaji mkuu. Kila mmoja aliyejisikia kutoa dukuduku lake alifanya hivyo.

Turudi kwa Hoseah Mahenge na Godlove Ngilangwa. Ninayoandika ndiyo yanafahamika ofisini kwa madereva-vibarua hawa. Hoseah ameoa. Ana watoto wawili. Godlove ameoa. Ana watoto watatu. Sikujua jinsia ya watoto hao.

Wanalipwa mshahara wa Sh. 48,000 kila mmoja kila mwezi kutunza familia zao. Jinsi gani kiasi hicho kinaweza kukidhi mahitaji, ni swali la kujibiwa na wahusika hao.

Taarifa za kiofisi zinaonyesha Hoseah amemaliza Kidato cha Nne. Amepata mafunzo ya udereva. Ana leseni. Amehitimu mafunzo ya nyongeza Chuo cha Usafirishaji cha Ubungo, Dar es Salaam.

Aidha, amepata mafunzo mengine katika Mamlaka ya VETA na chuo kingine cha Kihonda, Morogoro ambacho kimeelezwa kuwa moja ya vyuo muhimu kwa madereva.

Naye Godlove Ngilangwa anaonyeshwa kuwa amemaliza shule ya msingi, lakini amehudhuria mafunzo ya udereva katika vyuo mbalimbali na anaimudu kazi yake vema kama afanyavyo Hoseah.

Madereva hawa wanaelezwa kuwa miongoni mwa walionyoosha kidole wakiomba kujieleza na walipopewa nafasi, walimwaga vilio vyao kwa Jaji Mkuu Ramadhani.

Kilio chao kikuu kilikuwa kutopewa ajira ya kudumu kwa takriban miaka mitano sasa; malalamiko yao kutosikilizwa kwa kipindi kirefu; kupewa uhamisho bila kulipwa gharama za usumbufu; na kutopewa hadhi wanayostahili kama madereva wenye ujuzi kamili.

Imefahamika kwamba baada ya kikao na jaji mkuu, kiongozi huyo wa mahakama aliwaambia madereva wote kuwa ameelewa. Walipotaka kujua lini waliyomweleza yatafanyiwa kazi, imeelezwa kuwa jaji aliwaambia kuwa atafuatilia.

Wakati Hoseah na Godlove wanapokea Sh. 48,000 kwa mwezi, madereva wengine wanapokea zaidi ya Sh. 85,000; wanapangiwa safari zenye marupurupu ya alawansi na wanapata mafao mengine kama waajiriwa wa kudumu.

Kinachouma zaidi kwa upande wa madereva hawa wawili ni kwamba, kuna wenzao ambao hawana ujuzi wala uzoefu wa kiwango chao, ambao wana mshahara mkubwa na marupurupu kedekede.

“Mimi siwezi kujitapa, kwa mfano, kwa Hoseah. Ni kama mwalimu wetu; anajua mengi. Lakini kwa nini wanamweka kibarua kwa miaka yote hii, ni jambo ambalo haliwezi kupata jibu la hekima,” ameeleza mmoja wa madereva wa Mahakama ya Kazi.

Dereva mwingine wa Mahakama Kuu alimwambia mwandishi huyu kwamba miaka minne na zaidi ni kipindi kirefu cha kumweka mtu akisubiri ajira ya kudumu, hasa katika taasisi inayoamua mashauri yanayohusu waajiri na waajiriwa.

“Sisi wengine hatuna hata viwango vya kuwazidi hawa, lakini tuna fursa ya kupata mikopo na marupurupu mengine ya kiofisi, wakati wao wanakodoa macho kama watoto wa mama wa kambo,” ameeleza.

Hapa ndipo Jaji Mkuu anapopata kazi ya nyongeza. Kwanza ameanzisha utaratibu mzuri wa kuongea na kada mbalimbali. Utamu wa utaratibu huu umejichimbia kwenye nia yake ya kujua kulikoni katika maisha ya wafanyakazi wa ngazi ya chini.

Leo hii, Mkuu wa Mahakama anagundua kuwa tawi jingine la ofisi yake, limeweka madereva vibarua kwa takriban miaka mitano. Bila shaka hili linamsononesha.

Anagundua kuwa vibarua hao wamelia kwa muda mrefu lakini hakuna aliyewasikiliza. Bila shaka atajiuliza, iwapo suala la ajira ya dereva linaweza kupuuzwa, kutelekezwa, kudharauliwa au kunyamaziwa tu, kuna mangapi katika safu za juu ambayo hayaendi sawa?

Katika kudadisi suala hili, zimepatikana taarifa kwamba miezi kadhaa iliyopita, hasa baada ya madereva kukutana na jaji, kulikuwa na uvumi kuwa Hoseah na Godlove wangeachishwa kazi

Pendekezo hilo liligonga ukuta pale wahusika walipong’amua kuwa watalazimika kulipa kiasi kikubwa cha fedha kwa madereva hao. Kilichofuatia hapo ni madai kwamba madereva hawana elimu inayostahili.

Lakini ukweli ni tofauti na madai hayo. Hoseah ana elimu ya sekondari; amehudhuria mafunzo; ana vyeti na ujuzi mkubwa. Naye Godlove, pale alipoajiriwa kama kibarua, hakukuwa na masharti ya elimu ya sekondari.

Bali ukweli unabaki palepale kwamba watumishi wote ambao hawajafikia viwango vya elimu hupewa muda wa kusoma, na kwamba muda huo ukiisha wanakuwa ama wamepata elimu hiyo au hujiondosha kwenye ajira.

Godlove hajapewa sharti hilo wala muda wa kufanya hivyo. Sababu pekee ni kwamba hakuwa kwenye ajira ya kudumu kwa zaidi ya miaka minne; akitumikia chombo ambacho kinashughulikia mashauri ya aina hiyo kuwa ni ukiukaji sheria na haki!

Hivi sasa ni Jaji Mkuu Agustino Ramadhani ambaye anaweza kumaliza tatizo la ajira la vibarua hawa na wengine waliomwaga vilio vyao mbele yake.

Inaweza kuonekana kuwa “aibu” kwa watendaji katika Mahakama ya Kazi, kuona Jaji Mkuu akiteremka hadi ngazi hiyo, kushughulikia ajira ya vibarua. Bali kwa shabaha ya kuonyesha mfano, itabidi afanye hivyo.

(Imeandikwa rasmi kwa ajili ya gazeti la MwanaHALISI, 2 - 9 Januari 2008)

Simu: 0713 614872
ndimara@yahoo.com

No comments

Powered by Blogger.