Header Ads

LightBlog

HELIKOPTA YA JESHI NA UTALII

Likizo ya rais na usalama wa taifa

SITAKI Rais Jakaya Kikwete aende likizo wakati kuna “suala kubwa linaloshusu usalama wa nchi.”

Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyememu aliviambia vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Ijumaa kuwa rais yuko likizo, lakini aweza kufanya kazi iwapo kuna suala kubwa linalohusu usalama wa nchi.

Ukweli ni kwamba rais asingekwenda likizo, kwani suala linalohusu usalama wa nchi lipo mezani kwake. Ni lile linalohusu usalama wa mipaka ya nchi na wananchi wake.

Ni suala la kuingia katika ghala la silaha za Jeshi la Wananchi (JWTZ), kuchukua helikopta ya jeshi na kuruka hadi Arusha, huku waliokuwemo, tena watu kutoka nchi za nje – Uingereza, Canada, Marekani na Australia, wakipiga picha.

Tutake tusitake, hili ni suala la usalama wa nchi. Linahusu usalama wa wananchi na mali zao. Linahusu maisha ya nchi na viumbe wake.

Katika safu hii wiki iliyopita, nililalamikia ukimya wa serikali kuhusu tukio hilo. Niliuliza maswali 42. Nilidhani wahusika wataelewa. Watakuwa wepesi wa kujibu. Wataona wanawajibika kutoa majibu. Wataonyesha uadilifu.

Leo hii, wiki tatu tangu kupatikana kwa taarifa za helikopta ya jeshi kutumiwa na watalii kupiga picha, hakuna taarifa yoyote ya serikali – kutoka kwa Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Juma Kapuya au Amiri Jeshi Mkuu, Jakaya Mrisho Kikwete.

Katika hali hii, sharti watu wenye uchungu na nchi hii; wale wanaojali usalama wa nchi na watu wake, waendelee kuuliza. Hii ni kutokana na uzito wa suala lenyewe; ni kubwa na “linahusu usalama wa nchi.”

Ingawa wanaoiuzia silaha Tanzania wanajua kuna aina gani, kiasi gani, kutoka wapi, kwa bei ipi, zinaweza kutumiwa vipi na zina uwezo gani; kuna mambo kadhaa hawajui. Kwa mfano, hawajui lini silaha hizo zinahitajika kufanyiwa kazi.


Lakini hatua ya watu kutoka nchi za nje, kukodi, au kupewa, au kuiba helikopta ya jeshi na kuitumia kwa kazi binafsi, inaonyesha kuwa: Jeshi limeingiliwa. Kuna wanaojua taratibu za kila siku jeshini, matumizi ya zana; zipi zinahitajika sasa, zipi zikodishwe na zipi zikae “stendibai.”

Hao ndio wanakwenda ama kuchukua, kukodi au kupewa helikopta za jeshi. Au kuna “Idara ya Masoko” jeshini inayotangaza na kufuatilia wateja wa kutumia hekikopta zake.

Aidha, hatua ya kupata helikopta ya jeshi kwa matumizi binafsi, inaonyesha ama ulinzi ndani ya jeshi umepungua au umelegezwa. Nani kapunguza au kalegeza ulinzi na kwa nini; ndilo swali kubwa hivi leo.

Nani amekataa kuweka suala hili mezani kwa Rais Kikwete, mpaka rais anakwenda likizo bila kulishughulikia? Au, nani amemshauri rais kuwa ni “jambo dogo” kwa hiyo alale na kusahau?

Au tafsiri ya “usalama wa nchi” ndiyo inagomba? Na hili linawezekana. Kuna wanaodhani usalama wa nchi ni usalama wa rais kutopinduliwa, kutopingwa au kutoseng’enywa. Huo ni ufinyu na upofu.
Nani anaweza kumuaga rais, na kumtakia likizo njema, wakati katika jeshi lake kuna biashara inayoweza kuzaa mtafaruku mkubwa wa kuweza kumeza amani nchini au kurudisha nyuma maendeleo madogo ya kidemokrasi yaliyopatikana?

Labda rais awe anajua kuwa kinachoendelea “ni kidogo kisicho na athari mbaya na kubwa;” au anaridhika kuwa kinachofanyika ni sahihi; au hana taarifa kamili juu ya kinachotendeka.

Vyovyote itakavyokuwa, hapo ndipo rais anapaswa kujenga mashaka juu ya chochote kinachotendeka; hasa chochote ambacho wananchi wametilia mashaka; na hasa kile ambacho wachambuzi wameonyesha kinaweza kuleta madhara kiulinzi, kisiasa na kiuchumi.

Ukimya wa serikali unaleta tafsiri nyingi. Kwamba wanaokataa kutoa kauli, wanajua kinachoendelea lakini wanashindwa kutoa majibu ambayo wanajua vema kwamba hayatazima kiu ya wananchi na wapenda nchi.

Kwamba wanaokataa kutoa kauli wanajua nani aliidhinisha matumizi ya helikopta nje ya utaratibu; wanajua kama ndio utaratibu na wanajua nani anachuma kutoka mradi huu ambao bila shaka unaingiza fedhi nyingi.

Na katika hili, tukizungumzia viongozi serikalini ambao wanapaswa kutoa kauli, tuna maana ya kwanza na moja kwa moja, Rais Kikwete, Waziri Mkuu Edward Lowassa, Waziri Kapuya, mteule wa rais, Jenerali Mwamunyange na Waziri wa Habari Mohamed Seif Khatib.

Kama wasemaji wanaona suala hili la kuvunja na kuingia kwenye ngome ya jeshi na kuchukua, kuiba au kupewa helikopta ni suala dogo, kwa nini hawatoi majibu yanayolingana na “udogo” huo?

Kama wanaona ni suala kubwa, tena la ulinzi na usalama wa nchi, kwa nini wanakaa kimya na kumwacha rais aende likizo wakati kuna suala kubwa la kumzuia kwenda kulala?

Mkuu wa Mawasiliano ikulu, Salva Rweyemamu, anasema likitokea jambo kubwa la usalama wa nchi, rais anaweza kufanya kazi akiwa likizoni.

Salva, mpelekee rais suala hili. Mfafanulie kwamba, kama ngome ya jeshi imepenywa, na watu kutoka nje wakachukua helikopta ya jeshi kwa raha binafsi, basi yeye na wananchi wake wote, wako uchi!

Mwambie avae na avalishe nchi yake. Lakini muhimu zaidi, mwambie ajibu maswali ya wananchi yaliyowasilishwa kupitia safu hii – wiki iliyopita na leo – ili wajue nafasi yake katika hili na hatua anazochukua.

(Makala hii imeandikwa kwa kuchapishwa katika safu ya SITAKI ya gazeti la Tanzania Daima, Jumapili, 23 Desemba 2007. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)

No comments

Powered by Blogger.