Header Ads

LightBlog

JESHI LAINGIA BIASHARA YA UTALII?

JWTZ NA BIASHARA YA KITALII

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI serikali ikae kimya kuhusu matumizi ya helikopta ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) iliyoanguka mkoani Arusha siku 11 zilizopita. Sitaki!

Maelezo ya awali ni kwamba helikopta ya jeshi ilikuwa imebeba “watalii” kutoka Canada, Marekani, Uingereza na Australia na kwamba ilianguka na kuwaka moto.

Watalii na helikopta ya jeshi? Watalii kutoka nchi za nje, na siyo watalii wa ndani ya nchi, na helikopta ya jeshi? Watalii wasiokuwa na uwezo kifedha wa kukodisha ndege yao mpaka watumie helikopta ya jeshi?

Watalii kutoka nchi tajiri, Canada, Marekani na Uingereza, nchi washirika wakubwa katika maendeleo ya Tanzania kwa kutoa mikopo na misaada, hawana uwezo wa kukodi ndege kutoka kampuni binafsi? Mpaka watumie helikopta ya jeshi?

Eti watalii walikuwa wanapiga picha za Ziwa Natron na mlima Oldonyo wenye volcano hai! Kwamba ziwa na mlima haviwezi kuonekana vizuri kutoka ndege ya kiraia mpaka mpigapicha awe katika ndege ya jeshi?

Katika hili kwa nini serikali inakaa kimya? Inataka habari hii ife? Inataka wananchi waendelee kujiuliza maswali mengi bila kupata majibu sahihi? Au inataka baadaye, itoke na kauli kwamba mambo ya jeshi hayajadiliwi katika vyombo vya habari?

Hakika, hapa serikali isisubiri kuumbuliwa. Ni jana, Jumamosi, baadhi ya waandishi wa habari walikabidhiwa tuzo za uandishi wa uchunguzi nchini. Ukweli ni kwamba bado wanatambaa, lakini tuzo hizo ni motisha kubwa katika kuandika habari za uchokonozi.

Leo hii, hakuna habari nono kama hii. Rubani wa helikopta ni nani? Helikopta ilianzia wapi safari ya kwenda Natron na Oldonyo. Ilipita wapi na “watalii” walikuwa wakifanya nini kabla ya kukaribia maeneo waliyokuwa wakitaka kupiga picha?

Je, kuna kitengo cha utalii katika JW? Kama kipo, kina ndege na helikopta ngapi? Vifaa vyake vingine kwa shughuli hii ni vipi? Je, utalii ni moja ya miradi ya jeshi ya kuzalisha fedha za matumizi ya nyongeza? Je, jeshi linapungukiwa fedha kiasi cha kuanzisha miradi ya “kubangaiza?”

Je, helikopta iliyobeba watalii iliidhinishwa na nani kufanya kazi hiyo? Ilitoka ngome ipi ya jeshi? Kwa nini iliamuliwa kuwa hiyo ndiyo ilikuwa inafaa? Rubani wa helikopta ya jeshi alijuaje maeneo ya kupita ili watalii wapate picha nzuri waliozotaka?

Kuna maswali mengi. Wanaoitwa watalii walitoka wapi kabla ya kuingia Tanzania? Nani anaweza kuthibitisha kweli kwamba ni watalii? Viwanja vya ndege na, au mipaka ya nchi ina rekodi gani juu ya kuingia nchini kwa watalii hao?

Tayari helikopta imeanguka na kuungua. Watalii wamepona! Nani amethibitisha uraia wa watalii? Balozi za nchi watokako watalii hao, zilizoko Dar es Salaam, zinasemaje juu ya raia wake, kama kweli wanatoka huko?

Balozi ambazo nchi zao huning’iniza serikali za nchi nyingi zikizitaka kuwa adilifu, zinasema nini juu ya raia wake kutumia helikopta ya jeshi la ulinzi kwa raha na mafao ya binafsi?

Kuna uhusiano gani kati ya watalii wa Canada, Marekani, Australia na Uingereza kwa upande mmoja, na balozi na nchi watokako, kwa upande mwingine? Je, inawezekana “watalii” wametumwa kutoa mtihani wa uimara au ulegevu wa jeshi?

Nani alichora mpango wa watalii kutumia helikopta ya jeshi? Huyo lazima awe mtu muhimu katika mahusiano ya jeshi. Kwamba ndege ndogo za kibiashara zinagombea maegesho kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, ni motisha gani watalii walipata kutumia ndege ya jeshi?

Hapa ni muhimu kujua iwapo rubani alikuwa askari wa JW au raia anayejua kuvurumisha kikata hewa hicho Je, rubani wa helikopta alikodishwa kwa kiasi gani au alikuwa wa kujitolea?

Je, helikopta ya jeshi ilichukuliwa kwa mkataba upi? Kuna malipo yoyote yaliyotolewa au ahadi ya kulipa? Kiasi gani cha malipo – fedha taslimu au asante kwa njia mbalimbali? Lini malipo hayo yatatolewa au yalitolewa?

Lakini muhimu pia ni kujua nani hasa anafaidika na malipo hayo – aliyeidhinisha matumizi ya helikopta, rubani na aliyemtuma, baadhi ya maofisa wakuu jeshini, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa au ikulu? Nani anapokea “mshiko?”

Muhimu pia ni kwamba Amiri Jeshi ni rais. Mara hii ni Jakaya Mrisho Kikwete ambaye wakati anaondoka wiki hii kwa ziara ya Marekani aliacha helikopta yake imetumiwa na “watalii” na imeanguka na kuungua.

Amiri Jeshi anasemaje juu ya matumizi ya helikopta “yake?” Helikopta za jeshi, kama zilivyo ndege na magari ya jeshi, ni sehemu ya zana za kazi; waweza kusema, zana za ulinzi wa taifa. Vimeundwa na vinapaswa kutumika na kusimamiwa kwa misingi ya ulizi.

Nafasi ya Amiri Jeshi ni ya kulinda maisha na mali za wananchi ndani ya mipaka ya nchi yao na dhidi ya uchokozi au uvamizi kutoka nje. Kwa maana pana, helikopta ni mali ya wananchi, waliyonunua kwa kodi wanazotozwa na inayopaswa kutumiwa kwa ulinzi wao.

Katika mazingira ambamo serikali imekataa kutoa taarifa juu ya helikopta ya jeshi kutumiwa na watalii kutoka nje kufanya shughuli binafsi, ni uandishi wa wa uchokonozi ambao pekee unaweza kusaidia kuleta nuru juu ya kilichotendeka.

Hadi hapo taarifa zitakapowekwa wazi, acha kila mwananchi awe na mawazo yake: Kwamba sasa jeshi linabangaiza kama machinga; au halina ulinzi kwani kila mmoja aweza kuingia na kujichukulia ndege anavyotaka; au ulinzi wa wananchi sasa mashakani; au wakubwa wameamua kutumia jeshi kufanya biashara ya anga; au amiri jeshi kaenda likizo.


(Makala hii imeandikwa kwa ajli ya safu ya SITAKI, gazeti la Tanzania Daima Jumapili, 16 Desemba 2007. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)

No comments

Powered by Blogger.