Header Ads

LightBlog

UJINGA UNAPOKUWA NGOME

Fasheni ya kukiri ujinga Tanzania

Na Ndimara Tegambwage

KATIKA siasa za Tanzania, kukiri ujinga imekuwa fasheni. Lakini siyo fasheni peke yake. Kukiri ujinga hadharani imekuwa njia ya kueneza ghiliba, kujikosha na kutaka kuhurumiwa.

Waziri Mkuu Edward Lowassa amenukuliwa akisema mjini Morogoro mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba serikali haiwajui mafisadi na “vigogo” wauza dawa za kulevya nchini.

Gazeti moja, katika toleo la juzi Jumatatu lilimnukuu Lowassa akisema, “Nasema watajeni na ninaahidi tutawashughulikia bila kujali cheo cha mtu au nafasi aliyonayo katika taifa hili…”

Lowassa amefuata nyayo za Rais Jakaya Kikwete ambaye miezi miwili iliyopita aliwaambia waandishi wa habari akiwa Ufarasa kwamba hajui sababu za Tanzania kuwa masikini wakati ina maliasili na raslimali nyingi.

Hata Kikwete alikuwa akirudia yaliyosemwa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ambaye alinukuliwa akisema, Juni mwaka huu, kwamba kabla ya kupata elimu katika Chuo Kikuu cha Harvard, Marekani, alikuwa hajui kwa nini Tanzania ni nchi masikini.

Katika hili, ujinga wa Kikwete unaweza kulinganishwa na ule wa Sumaye. Kwamba viongozi hawa, pamoja na kuwa serikalini kwa miaka mingi, hawakuweza kupata nyenzo za kuwasaidia kufikiri na kuchambua.

Wamekuwa wakitazama lakini hawaoni. Kuona ni kutambua. Kutambua kunahitaji elimu iliyolenga muhusika kujenga tabia ya kufikiri, kuuliza maswali na kujenga mashaka. Kupita madarasani kwa kukariri bila kufikiri, hakuzai elimu; kunazaa kasuku na makasha.

Sumaye anakiri kuwa elimu imemwondoa katika kiza nene. Hakuweza kujua kwa kuwa alikuwa hajapata elimu ya kumwezesha kufikiri, kuuliza maswali na kudai majibu sahihi na kupembua.

Kikwete bado anashangaa kwa nini nchi bado ni masikini wakati ina utajiri wa maliasili na raslimali nyingi. Bila shaka anahitaji kufumbuliwa macho kwa kuambiwa au kufunzwa kufikiri na kung’ang’aniziwa tabia ya kufikiri kwa kuzingatia mazingira na nyakati.

Lakini hili la Lowassa la kuwataka wananchi wataje mafisadi na vigogo wauza dawa za kulevya, linahitaji zaidi ya darasa la kufikiri.

Lowassa ni mmoja wa wale waliotajwa kwenye orodha ya mafisadi 11. Jina lake linaonekana bila wingu lolote. Naye, kwa miezi mitatu sasa tangu orodha iwekwe hadharani, hajakana kuwa fisadi. Hata serikali haijajitokeza na orodha yake ya mafisadi.

Kilichosikika sana kutoka kwa baadhi ya viongozi serikalini na katika na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni kauli kwamba wanaotaja “mafisadi” sharti wawe na “ushahidi.”

Hii siyo mara ya kwanza kusikia kauli hizo ambazo, bila shaka yoyote, zimelenga kunyamazisha watoa fununu juu ya ufisadi.

Lakini Lowassa anayo orodha. Kila kiongozi wa ngazi ya juu katika serikali ana orodha hiyo. Tatizo ni kwamba karibu wote wanasema, “madai hayo siyo mapya.” Wanaongeza kuwa hayo ni malalamo ya wapinzani.

Hii ina maana gani? Kwamba tuhuma za ufisadi zinazowahusu wao siyo mpya. Kwa hiyo hazipaswi kushughulikiwa. Kwa hiyo wanataka tuhuma mpya dhidi ya watu tofauti na siyo wao!

Mazingira ambamo Lowassa alitolea kauli yake yalikuwa mazuri kwake kukana au kukiri kuwa ni mmoja wa mafisadi. Lolote kati ya hayo, ama lingekuwa ungamo au kanusho ambalo lingepata nguvu ya askofu mpya, Jacob ole Mameo aliyekuwa anatiwa wakfu kuwa Askofu wa Dayosisi ya Morogoro.

Hakufanya hivyo. Hakupata ushauri wa kufanya hivyo. Aliwaambia wananchi, wengi wa madhehebu yake ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kwamba wampe orodha ya mafisadi na vigogo wa dawa za kulevya.

Kumbe waumini hao na wananchi wengine waliohudhuria ni sehemu ya jamii ambayo tangu Septemba 15 mwaka huu imehubiriwa orodha ya mafisadi ambamo jina la Lowassa linasomeka bila utata.

Tendo la waziri mkuu kujiunga na “klabu” ya viongozi wenye fasheni ya kukana kujua hili au lile kutokana na ama kutokuwa na elimu au kwa ghiliba tu na kutaka kuonewa huruma, halijamshangaza yeyote mjini Morogoro na katika taifa zima.

Kikwete na Lowassa wamekuwa serikalini kwa zaidi ya miaka 20 sasa. Hakuna awezaye kusema hajui kilio cha wananchi juu ya watu wanaofanya ufisadi na kuuza dawa za kulevya, lakini hawakamatwi na kama wakikamatwa hawafikishwi mahakamani.

Na hili halihitaji kuhubiriwa kanisani wala misikitini. Serikali iliyo makini huandaa utaratibu wa kuondoa kero za ufisadi na dawa la kulevya. Huomba wananchi watoe taarifa bila kuwatishia kwa kudai ushahidi.

Baada ya hapo serikali huchukua fursa hiyo, kwa kutumia vyombo vyake, kuchunguza na kupata ushahidi na hatimaye kuwaswaga wahusika mahakamani.

Lakini sivyo ilivyo. Kila anayeingia madarakani anaanza kusema “nipe majina ya mafisadi na wauza dawa za kulevya.” Rais Kikwete amewahi kukiri kupewa orodha ya wauza dawa za kulevya. Kwa nini Lowassa anakataa kutumia orodha hiyo?

Leo hii pia kuna orodha ya mafisadi iliyotolewa hadharani na kuhubiriwa nchi nzima. Rais anayo. Waziri Mkuu na viongozi wengine serikalini wanayo. Kwa nini Lowassa hataki kutumia orodha hiyo na badala yake anadai mpya?

Tayari wananchi wameanza kuelewa kinachoendelea. Kuna kukiri ujinga ambao hakika ni wazi; kwamba muhusika alikuwa hana nyenzo za kutumia kufikiri, kuchambua na kupambanua.

Lakini hata katika hilo, ghiliba ni wazi. Je, muhusika hakuwa na wasaidizi; wataalam wenye uwezo wa kufikiri? Je, kama kweli alikuwa hajui, kwa nini aliendelea au anaendelea kukaa madarakani bila kwanza kujifunza anachopaswa kufanya?

Hapa pia kuna chembe ya rushwa. Kung’ang’ania kuchukua nafasi ya utawala ya ngazi ya juu, kwa kishindo na mbwembwe, wakati hujui unachopaswa kufanya ili kulinda watu na maliasili na raslimali zao, ni rushwa ya aina yake.

Hata hivyo, kuna kukiri ujinga kulikolenga kulegeza mishipa ya fahamu ya wananchi; ili waseme kwa sauti ya unyenyekevu, “Jamani, kumbe hata rais wetu na waziri mkuu nao hawajui hili?

Hili nalo ni sehemu ya ufisadi. Ni njia ya udanganyifu usiomithilika wa kuchota mawazo ya wananchi na kuwafanya wakubaliane na hoja dhaifu, lakini zilizolenga kuwatakasa watawala ili wadumu madarakani.

Hebu soma hili: “Jamani kwa muda mrefu nimekuwa nasikia wanaokamatwa kwa dawa za kulevya na rushwa eti ni watu wadogowadogo huku vigogo wakitazamwa, tatizo ni kuwa mnasema tu vigogo, vigogo, hamuwataji.”

Hivyo ndivyo alivyonukuliwa Lowassa akisema mjini Morogoro. Anasema hawajui mafisadi wala vigogo wa dawa za kulevya na amesikia malamiko “kwa muda mrefu.” Na kwa muda mrefu, yeye na serikali yake
wamechukua hatua gani?

Kuna kila haja ya kuondoa uwezekano wa wananchi kuamua kwamba watawala wote nao ni mafisadi. Kwa kuwa watakuwa wameamini kuwa mafisadi hawawezi kukamata mafisadi, basi watafanya watakavyofanya kwani kukiri ujinga sasa hakuwaondolei adha.

(Makala hii imechapishwa katika gazeti la MwanaHALISI, 28 Novemba 2007)
ndimara@yahoo.com
Simu: 0713 614872

No comments

Powered by Blogger.