Header Ads

LightBlog

UHURU WA MAWAZO KATIKA KILA NYANJA

Kisumo asivyopenda uhuru wa kufikiri

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI wanasiasa wachovu wabeze maoni ya baadhi ya wanajamii na kuyaita ya “kitoto” kama alivyonukuliwa Peter Kisumo akisema.

Alikuwa akirejea mjadala uliopo sasa iwapo mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe awemo kwenye Kamati ya Madini ya watu 12 iliyondwa na Rais Kikwete.

Kwa hali yoyote ile, kauli ya Peter Kisumo ina ushawishi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambamo yeye ni mkongwe. Lakini ni kauli chafuzi inayolenga kuziba mifereji ya fikra.

Kwanza, kuziba, kuzuia au kuweka ugumu wowote ili watu wasijadili jambo lolote linalohusu maisha yao kijamii, kisiasa, kiuchumi na hata kiimani, ni kuingilia uhuru wao wa mawazo.

Huko ndiko kuvunja haki na uhuru wao wa kuwa na maoni na kutoa maoni hayo hadharani. Na Kisumo amenukuliwa akisema kwamba mjadala huo ni mabishano ya “kitoto.”

Pili, kwa mtu yeyote mwenye nafasi ya Kisumo katika jamii, kudiriki kuita mjadala hai juu ya maisha ya watu na taifa lao, kuwa ni wa “kitoto” ni kuendesha ugaidi kifikra na kutaka kunyamazisha sauti na hoja zinazogongana na zake au chama chake.

Kisumo anataka kusema kwamba kama rais kasema, basi inatosha. Hakuna haja ya kutafakari. Hakuna sababu ya kutofautiana. Hakuna muda wa kuhoji. Hizo ndizo nyakati za “zidumu fikra za mwenyekiti” ambazo huwezi leo hii, kuzitumia hata katika darasa la chekechea.

Mjadala kuhusu Zitto kuwemo au kutokuwemo katika Kamati ya Kikwete ya Madini (KKM) umeibuka wakati muwafaka. Kilichouibua ni ujasiri wa kuhoji na tabia ya kujenga mashaka.
Haitoshi kugegema na kutokwa udenda juu ya tendo la rais kuunda kamati ya kuchunguza mikataba na sheria zinazotawala uchimbaji madini. Haitoshi.

Rais ameunda kamati wakati gani? Katika mazingira yapi? Kufuatia matendo yapi? Chini ya shinikizo lipi na kutoka kwa nani? Kama ni kwa utashi wake binafsi, lini rais aligundua umuhimu wa kamati kama hiyo? Ina maana rais siyo mwepesi wa kutambua maslahi ya nchi yake?

Hayo ni baadhi ya maswali ambayo mwananchi anatafuta majibu yake kupitia mijadala hai; katika magazeti, redio, televisheni, mikutano na semina. Ni maswali yenye kujenga kiungo thabiti kati ya wazo (fikra) na tendo.

Kuna maswali mengine. Nani mwingine aliyeteuliwa kuingia kamati hii? Anatoka wapi? Amekuwa wapi? Tabia yake ni ipi – katika maeneo ya ukweli, uadilifu na uwajibikaji? Amefanya nini maishani mwake hadi sasa kinachompa sifa za kuingia kamati hii?

Hayo pia ni maswali muhimu. Yanalenga kuibua majibu yenye kutaka kuondoa mashaka juu ya kile ambacho rais anataka kamati ifanye. Hata hivyo, ni majibu kwa maswali haya, ambayo yanaweza kuonyesha mwelekeo na hata hatima ya kazi ya kamati.

Bado kuna maswali mengine. Je, mteuliwa ana uhuru wa kufikiri na kutenda au amefungwa kama boya? Je, ikibidi anaweza kutofautiana hata na aliyemteua? Je, mteuliwa anachukulia uteuzi huu kama ajira, asante, njia ya kumlinda aliyemteua au kujikosha nafsi yake kwa machafu aliyowahi kutenda?

Maswali haya yanalenga kuimarisha hoja kuu iliyosababisha kuundwa kwa kamati. Yanatekenya nafsi za watakaofanya kazi na kupembua hata fikra zao ili kuona iwapo kweli watafanya kazi ambayo wananchi wenyewe wanataka kuamini kuwa ni muhimu kwao na nchi yao.

Ni maswali kama haya ambayo yanaweza kukupa majibu juu ya nia safi ya rais katika kuunda kamati; au ni tendo la kukidhi “utetezi” wa nafasi yake dhidi ya shinikizo kutoka pande zote.

Maswali yote haya na mengine ya aina hii, ndiyo yanaunda hoja za mjadala juu ya nani hasa alipaswa kuingia katika kamati inayopewa jukumu kubwa la kuangalia jinsi raslimali za taifa zinavyopaswa kuvunwa kwa maslahi ya wananchi.

Hapa hoja siyo Zitto awemo au asiwemo katika kamati. Hoja kuu ni je, rais ana dhamira ya kweli ya kujua sheria na mikataba inasemaje kuhusu uchimbaji madini? Ni kweli hakujua hayo kwa karibu miaka 20 aliyokuwemo serikalini na je, utaratibu aliotumia ni sahihi?

Kama rais ana dhamira ya kweli, ni watu wa aina gani wanastahili kuwa katika kamati yake ya kutafuta ukweli? Je, waliokwishanufaika na mikataba hiyo, hata kwa hila, bado wana sifa ya kuwa katika kamati hii?

Mjadala huu ni mzuri na mpana. Unalenga kuwa darasa kwa rais, serikali na wananchi. Unapanua wigo wa mawazo na kuambukiza hamu na sharti kuu la kufikiri.

Kuita mjadala huu kuwa ni wa “kitoto” ni kukiri kuwa mtoto katika utu uzima. Na hiyo ni hatari kwa afya ya taifa na watu wake. Sitaki!

(Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com. Ilichapishwa katika gazeti la Tanzania Daima la 25 Novemba 2007)

No comments

Powered by Blogger.