Header Ads

LightBlog

MATATIZO YA USAFIRI WA WANAFUNZI TANZANIA

Nauli, wanafunzi na serikali bubu

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI wadau wa usafirishaji abiria Dar es Salaam wafikiri kuwa kila Mtanzania au kila mtu, hana uwezo wa kuona, kusikia wala kufikiri.

Siyo siri kwamba wadau wengi katika tasnia hii, ni wenye magari ya usafirishaji abiria. Hata walioko serikalini, mashirika, kampuni na taasisi za mafunzo; wana magari ya kusafirisha abiria.

Kila pendekezo wanalotoa linalenga kuonyesha kwamba wao wana uchungu sana na wanafunzi na wasafiri mijini; kwamba wao hawapati faida au wanapata hasara; kwamba wao wanajitoa muhanga; kwamba wao ni wema sana isipokuwa “hali ya kiuchumi” inauma sana.

Inapotokea mjadala unaohusu kupanda kwa nauli umetokana na kile wanachoita “utafiti” wa taasisi, tena ya serikali, basi wadau hawa wenye magari hushangilia na kuona kwamba “huu ndio wakati wa mavuno.”

Na ndivyo ilivyokuwa jijini Dar es Salaam, Ijumaa wiki iliyopita. Baada ya kufanya kile kilichoelezwa kuwa mjadala, wadau wengi wameripotiwa kujiridhisha kuwa “hali ya maisha ni ngumu,” kwa hiyo wanafunzi walipe nauli ya Sh. 100 badala ya Sh. 50 za sasa.

Hii ina maana kwamba nauli ya Sh. 100 ndiyo itatoa motisha kwa kondakta na dreva kubeba wanafunzi; tofauti na sasa ambapo wanaachwa vituoni kwa kuwa wanalipa Sh. 50.

Huu ni uzandiki wa hali ya juu. Nani amesema nauli ya mtu mzima itaendelea kuwa Sh. 250 au 300 au 350 wakati wote? Hivi hawa wanaojiita watafiti hufanyia wapi utafiti wao? Vyumbani? Kwenye kompyuta tu?

Nenda kituo cha mabasi cha Mwenge. Nauli hutegemea wakati au muda maalum. Asubuhi inaweza kuwa Sh. 300 kwa safari ya Mwenge kwenda Tegeta. Inakuwa 250/- kati ya saa saba na saa 10. Kuanzia saa 12.30 hadi saa 2 usiku, inapanda na kuwa Sh. 500 au hata 1,000 kwa kichwa.

Hii ni kwa baadhi ya magari madogo. Magari makubwa ambayo yamekatisha njia katika sehemu nyingine, hutoza kati ya Sh. 300 na 500.


Je, kunapokuwa na “mavuno” makubwa kwa njia ya unyang’anyi, mbona bado wanafunzi wanaendelea kunyanyaswa? Asubuhi wanaachwa vituoni kwa kuwa hawana nauli “kubwa.” Jioni wanaachwa kwa kuwa magari yanabeba walio tayari kulipa zaidi ya nauli inayofahamika.

Leo nauli ni Sh. 300 (kituo hadi kituo) na wanafunzi au watoto wanatozwa Sh. 100. Je, nani kasema nauli haitapanda zaidi? Je, nauli kwa wakubwa ikiwa Sh. 500, si wenye mabasi watataka mwanafunzi alipe Sh. 250 au 300, vinginevtyo wataendelea kumwacha kituoni?

Tasnia ya usafirishaji abiria, hasa jijini Dar es Salaam, ni soko holela lisilokuwa na mpangilio maalum. Miongoni mwa wasafirishaji ni mawaziri, makatibu wakuu, watendaji wakuu wengine serikalini, wakurugenzi wa kila ngeli katika mashirika na kampuni.

Humohumo kuna magari ya wafanyabiashara wakubwa, mainjinia, maprofesa wafunza vyuoni, makarani, walimu, watunza hesabu, wajane, polisi wa vyeo vya juu, askari wa ngazi za juu jeshini na yeyote yule aliyewahi kupata fedha, kwa njia yoyote ile, za kununulia gari la abiria.

Kila aliyeweka gari barabarani anataka kupata faida isiyomithilika. Dereva na kondakta wake hawatajali sheria wala kanuni za barabarani. Watajali kasi inayowawezesha kufika waendako haraka na kukusanya kiasi kikubwa cha fedha.

Na hao matajiri – wenye magari – wameyatupa magari yao barabarani na kusubiri mapato mwishoni mwa siku. Lakini sikiliza mjadala wa kondakta na dereva, tena mbele ya abiria.

Dereva atasema, “Nakwambia, huyu hata akinitia kidole jichoni, sitaondoka. Lakini nikija kutoka hapa, tayari nina gari langu mwenyewe.” Kondakta atadakia, “Eh, kama alivyofanya Juma. Sasa ana magari mawili ingawa moja linampa matatizo kidogo.”

Hizo siyo kauli za soga. Wanaambizana ukweli. Wanachuma. Wanatafuta panono. Wanabeba wenye nauli kubwa. Wanaomba kila siku nauli ipande ili waweze kuchuma.

Hivyo kuna wachumaji wa aina mbili katika biashara moja ya gari moja. Mwenye gari anachuma anachopelekewa. Dereva na kondakta wanachuma wanachoweza kusogeza nje ya kile walichoagizwa kuleta. Ni biashara ya ua nikuue. Anayeumia ni abiria.

Hapa ndipo zinaingizwa kauli za kipuuzi, lakini za kimaslahi kwa wanaozitoa, ambao ni baadhi ya viongozi nchini, kwamba ili kuwapunguzia wanafunzi matatizo ya usafiri, waende shule zilizoko karibu na wanapoishi.

Shule ninapoishi haijawahi kutoa mwanafunzi hata mmoja wa kwenda sekondari kwa zaidi ya miaka 15 sasa. Hapo ndipo unaambiwa upeleke mtoto wako. Hapo, kwenye kituo cha kujifunzia umbeya, uvutaji bangi na hata ukabaji!

Jijini Dar es Salaam, kama ilivyo katika baadhi ya sehemu nyingi nchini, kuna shule ambazo huwezi kutamani kuweka mtoto wako, hata kama ni kwa kukulia hapo tu.

Shule hizo ni chafu kwa maana ya ukosefu wa walimu, madarasa, madawati, vitabu, vifaa mbalimbali na kutokuwepo mazingira ya kupata elimu.

Mzazi atapenda kulipa zaidi kwa njia ya nauli, ili mtoto wake asake elimu mbali na nyumbani. Lakini kwa kuwa hakuna mpango mahususi wa usafirishaji jijini, nia na shauku ya kuwapa watoto elimu, inakandamizwa na kudidimizwa; na ulafi wa wenye magari unaneemeshwa usiku na mchana.

Serikali Kuu na serikali ya Dar es Salaam zimekataa kuweka utaratibu muwafaka wa usafirishaji. Zimefanya kila mwenye gari kuliingiza barabarani na kufanya anavotaka.

Serikali hizi zimekataa kuweka magari chini ya usimamizi mmoja wa kampuni, shirika au ushirika ambako magari yatachunguzwa uimara wake, yatawekewa ratiba, yatasimamiwa kitaaluma na madereva na makondakta watakuwa watu wenye ujuzi huo.

Nchi hii ina Vyuo Vikuu, Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra); ina Idara ya Usalama Barabarani na wadau wengine katika tasnia hii.

Kwa hali hiyo, leo kusingekuwa na watendaji serikalini, ambao ni pamoja na Waziri Mkuu, wanaolialia juu ya “tatizo la usafiri wa wanafunzi” au msongamano wa magari barabarani. Kusingekuwa na wanaotoa sababu kiwete kwamba wanafunzi wakilipa nauli ya Sh. 100 tatizo lao la usafiri litaisha.

Serikali ikikubali kila mwenye gari alisajili katika kampuni au ushirika mmoja, na asubiri malipo yake kwa mujibu wa mkataba wake, kile kinachoitwa tatizo la usafiri wa wanafunzi kitaisha.

Magari yatakuwa katika ubora unaotakiwa; ajali zitokanazo na uchakavu zitaisha; uzembe uletao ajali utapungua; heshima kwa abiria itatunzwa; viwango vya nauli vitalindwa; njia za mabasi zitaheshimiwa, utamaduni wa matumizi bora ya barabara utaanzishwa na mwanafunzi atakuwa abiria kama abiria mwingine.

Lakini kwa kuwa serikali kuu na serikali ya Dar es Salaam zinaendeshwa na baadhi ya viongozi wenye maslahi katika uholela wa usafirishaji Dar es salaam, kilio cha watoto na wazazi wao kitaendelea hadi wahusika watakapovuliwa mamlaka na madaraka.

(Mwandishi wa makala hii itakayochapishwa katika Tanzania Daima, Jumapili 18 Novemba 2007, anapatikana kwa simu: 0713 614872, imeili: ndimara@yahoo.com)

No comments

Powered by Blogger.