Header Ads

LightBlog

DC amchapa viboko baba kisa gari kupigwa mawe

Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga


Na Renatha Msungu, 
Nipashe, Jumamosi, 12 Agosti 2017


MKUU wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga amemcharaza viboko mzazi wa mmoja wa watoto walioshambulia gari lake kwa mawe na kuvunja kioo cha nyuma jana.

Gari hilo lenye namba za usajili STL 669, lilishambuliwa na watoto watatu katika barabara kuu ya Kondoa-Dodoma, kwenye kijiji cha Paranga wilayani Chemba.

Kufuatia kupasuliwa kwa kioo hicho, DC alisimamisha gari hilo na kuwakimbiza watoto waliolipiga mawe, hali iliyozua purupushani kwa muda.

DC huyo aliwakimbiza watoto hao kwa lengo la kuwakamata na kuwaadhibu lakini hakuweza kuwakamata baada ya kumzidi mbio.

Hata hivyo, wananchi walioshuhudia tukio hilo walimtajia DC majina na sehemu wanakoishi watoto hao ili awafuate majumbani kwao.

Ndipo mmoja wa wazazi wa watoto waliohusika na shambulio hilo alikutwa nyumbani akiendelea na shughuli zake na alipohojiwa na DC kuhusu malezi ya mtoto wake, aliingia katika majibizano yaliyomkera DC Odunga.

"Malezi? Malezi gani unataka kwangu? Mtoto ametoka shule, mimi nitajuaje anayoyafanya mtaani?" Aliuliza mzazi huyo wa kiume na kufafanua kuwa "mimi najua (mtoto) yuko shule, sijui kama amevunja kioo chako."

Ndipo DC alipoonekana kukerwa na majibu hayo hivyo kuchukua fimbo na kuanza kumcharaza mzazi huyo huku akimshutumu kwa malezi mabaya.

DC alimcharaza viboko mzazi huyo wa kiume kabla ya kumuingiza kwenye gari la polisi akiwa amefungwa pingu, kwa madai ya kuendelea kujibu kwa jeuri wakati akiulizwa maswali kuhusu  malezi ya mtoto wake.

Mzazi huyo aliendelea kujibu kuwa hastahili kupigwa kwa kuwa kosa si lake na kusema kuwa apelekwe popote pale, lakini haki yake itajulikana kwa sababu wakati watoto hao wanapiga mawe kioo cha gari yeye hakuwepo.

Watoto watatu hao waliofanya tukio hilo wanakadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka saba hadi 10.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia Odunga na mzazi huyo wakivutana huku mzazi akisikika akisema "aliyevunja kioo ni mtoto... chukueni tu hatua vyovyote haki yangu nitaipata".

Mwenyekiti wa kitongoji anakoishi mzazi huyo aliingilia kati na kudai kuwa matukio hayo ya kurushia mawe magari katika eneo hilo yapo na walishayakemea katika mkutano wa kitongoji yakapungua.

Alisema wahusika huwa ni watoto na vijana wa eneo hilo.
Akizungumzia tukio hilo, Odunga alisema kijiji hicho kimekuwa na tabia ya kuweka mawe barabarani pamoja na kupiga magari mawe jambo ambalo siyo sahihi.

Alisema wanajipanga kwa ajili ya kuanza operesheni ya kuhakikisha tabia hiyo inakomeshwa kabisa "kwa sababu ni hatari kwa wasafiri na jamii kwa ujumla".

Alisema wataendelea na msako wa polisi ili kubaini familia ambazo zina vijana wenye tabia hiyo kupitia jamii inayowazunguka.

Kufuatia purukushani hiyo gari la polisi wilaya lilitinga katika eneo hilo na kuwachukua watu sita wakiwahusisha na upigaji mawe magari, akiwemo mtoto mmoja aliyetajwa kuhusika jana.

Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Lazaro Mambosasa, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akisema ameagiza watu hao waliokamatwa watolewe rumande.

Alisema Jeshi la Polisi litaendelea na upelelezi kwa ajili ya kukusanya ushahidi wa tukio hilo na baadaye hatua zaidi zitachukuliwa kwa wahusika

Kamanda Mambosasa alisema amechukizwa na kitendo cha Mkuu huyo wa Wilaya kujichukulia sheria mkononi na kumjeruhi mzazi huyo.

"Amemjeruhi maeneo ya kichwani kwa rungu na mkono wake umevimba kutokana na kipigo alichokipata." alisema Kamanda Mambosasa. "Hii si haki kiongozi kujichukulia sheria mkononi…"


No comments

Powered by Blogger.