Magufuli avunja Mayai ya Maafa
Siyo kila chenye watatu au vitatu ni cha “Utatu.” Ndiyo maana kuna
“matatu” ambayo hayana uhusiano na waumini katika Utatu wa Maandiko.
Jina la Matatu la Kenya linatokana na magari madogo ya abiria yaliyokuwa
yakitoza “mapeni matatu” – senti 10 tatu – zilizokuwa nauli katika miaka ya
1950 katika miji mingi ya nchi hiyo.
Matatu au utatu
wa sasa umetoswa kabla haujachipuka. Ni Rais John Pombe Magufuli aliyetosa
utatu wa Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Mbunge Juma Mkamia na muumini wa CCM,
Lawrence Mabawa.
Mwinyi: Kama siyo kwa Katiba ya nchi,
ningependekeza Magufuli awe rais wa kudumu/milele.
Mkamia: Nitawasilisha hoja bungeni ya kuondoa
ukomo wa urais wa vipindi viwili.
Mabawa: Nitazunguka nchi nzima nikifanya
kampeni kushawishi kuungwa mkono kwamba Rais Magufuli aendelee kuwepo kwa zaidi
ya vipindi viwili.
Pote yalipoanza
maasi ya aina hii dhidi ya Katiba, yalianza namna hii: Watu wachache. Nje ya
Ikulu. Nje ya nyumba ya rais. Mbali na rais. Wakitamani. Wakinong’ona.
Wakisema. Wakiimba. Wakifyatuka: Rais aendelee. Na rais alisikia.
Alishawishika. Alikubali. Alijiandaa. Alibaki.
Huo ni ushawishi
unaotaga mayai ya maafa! Mayai hayo
yakiachwa hadi kuanguliwa, huleta vifaranga ambavyo hujenga woga miongoni mwa
watawala ambao huanza kushuku kila mmoja kuwa siyo mwenzao, anawapinga; kuwa
anawasema vibaya, kuwa anataka kuwang’oa, kuwa ana njama za “kuwamaliza!”
Kadri vifaranga
vinavyokua, huchochea uadui usio wa kisiasa dhidi ya wapinzani wa kisiasa;
huongeza woga miongoni mwa walio karibu na mtawala wanayetaka aishi madarakani;
huanza kutafunana wenyewe kwa wenyewe kama senene – kila mmoja akimshuku
mwenzake katika kupigania kupendwa na kuaminiwa; huwaingiza katika ndumba na
ushirikina.
Rais Magufuli
amenukuliwa wakati wa ziara ya mkoa wa Tanga wiki iliyopita akisema, katika
hili atasimamia kulinda Katiba; atatumikia kwa kipindi chake na kipindi hicho
kikiisha, atakabidhi “kijiti kwa mwingine.”
Kwa kauli hiyo,
amevunja mayai ya husuda kabla hayajaanguliwa na kutawanya sumu ya kutawala
milele au kwa muda zaidi ambayo tayari kwingine imeleta kutoaminiana, kusutana,
kugombana, kupigana na kuuana.
Lakini nani
anasema washawishi wamekoma baada ya kushushuliwa? Wanaweza kuendelea. Wanaweza
kuongezeka. Wanaweza kukusanyana na kupeleka ujumbe badala ya kutoa kauli
zilizotawanyika. Wanaweza!
Kisingizio chao
kitakuwa kwamba wana uhuru wa kufikiri na kutoa maoni. Kweli wanao. Lakini waletacho
ni maoni binafsi yenye sumu; yanayolenga kuangamiza misingi mikuu iliyowekwa na
Katiba; lakini pia yanayolenga kuua utashi, uhuru na haki za wengi wengine kwa
kutumia sheria au marekebisho ya Katiba.
Afrika ina somo
moja kuu. Kule wenye fikra hizo walipojaribu na kufanikiwa; hata wanaotawala
hawana raha. Hawana furaha ya kuwa madarakani. Hawana amani. Hata kinachoitwa
ushindi wa mia kwa mia, hakileti tabasamu kwenye nyuso zilizokunjamana kwa woga;
na nyoyo zilizofura kwa mihuri ya suto.
Je, Magufuli
anahitaji kukumbushwa mara zote juu ya hili, ili ajenge uthabiti na
asitetereke? Au, akumbushwe pia maeneo mengine mengi ambako Katiba imesema na
kuzingatia lakini hajapatamka kwa uthabiti huohuo?
No comments
Post a Comment