Header Ads

LightBlog

Tumesubiri sana, tunaweza kusubiri kidogo

 MISWADA YA SHERIA ZA HABARI
Tuisome kwanza, wananchi waijadili

KUNA taarifa kwamba serikali inataka kupeleka bungeni miswada miwili - Sheria ya Kupata Habari (Freedom of Information) na Sheria ya Vyombo vya Habari (Media Services).

Kwa haraka tunaweza kusema ni VEMA; serikali imezinduka. Ni miaka minane au tisa tangu serikali ikabidhiwe maoni ya wadau wa habari ambayo yanapendekeza jinsi sheria hizo zinavyotakiwa kuwa. Kwa muda wote huo serikali imekaa kimya - bila kutoa sababu yoyote kwa kimya hicho.

Rais Jakaya Kikwete 
Lakini leo, wakati serikali inasema itapeleka miswada bungeni, kuna taarifa kuwa itafikishwa mezani kwa hati ya HARAKA. Hili lazima limstue kila moja. Miaka tisa, kimya. Leo bungeni, haraka! Spika Anne Makinda alisema bungeni kuwa yeye haja hajapokea "hati ya haraka."

Haraka au bila haraka yaweza kuwa hoja dhaifu. Hoja ni: Kwanini serikali ilikalia maoni ya wadau kwa miaka yote hiyo? Kwanini inaleta miswada hiyo leo? Kuna nini leo ambacho hakikuwepo miaka yote? Kuna msukumo wowote wa ndani - shinikizo la nyongeza kutoka kwa wadau? Kuna shinikizo kutoka nje - wadau na wafadhili? Kuna masharti ya kupewa au kunyimwa hili au lile iwapo miswada haikupelekwa bungeni leo?

Hoja kuu ni: Serikali INAPELEKA nini bungeni? Je, ni mapendekezo kama yalivyoandaliwa na wadau? Haiwezekani. Ni miswada iliyoandaliwa na mwandishi wa sheria wa serikali? Ndiyo. Kama hilo ndilo jibu, tujiulize: Ameandaa nini?

Nimejitahidi kuongea na zaidi ya wadau 30 waliokuwa mbele katika maandalizi ya mapendekezo ya miswada kwa serikali. Wote - hakuna anayejua kilicho katika miswada ya serikali. Hii ni miswada inayohusu uhuru wa watu; uhuru wa wananchi. Uhuru wa kufikiri. Uhuru wa kutoa maoni. Uhuru wa kutafuta, kuandaa na kusambaza taarifa na habari. Inatosha kusema, UHURU.

Serikali iliyopokea mawazo/mapendekezo ya wadau wa habari kuhusu umuhimu wa kuwepo sheria inayolinda uhuru unaotambuliwa kikatiba - uhuru wa kuzaliwa nao (uhuru wa kufikiri na kutoa maoni); haistahili kuketi chini, kuandika miswada na kupitia pembeni kwenda bungeni kuwasilisha "kitu" ambacho wadau wakuu hawajaona.

Hili linaleta ukakasi. Linasababisha wananchi kujenga shaka; na shaka hili ni halali: Serikali inaficha nini? Serikali inaharakisha nini? Serikali ina nia gani?

Katika mazingira ya kawaida, serikali ilipaswa kuweka wazi miswada hii; tena kwa muda mrefu - kama miezi mitatu hadi sita; wananchi wasome, walinganishe maoni yao na kile ambacho serikali inataka. Watoe maoni. Serikali ipate mrejesho na kuufanyia kazi. Hatua hiyo pekee ingeonyesha kuwa serikali inajali na kuthamini UHURU wa wananchi na iko tayari kuulinda.

Miswada hii ya sheria inapaswa kutoka katika nyoyo za wananchi ambako baadaye, inapaswa kwenda kuimarisha uhuru wao wa kufikiri; na kuneemesha matendo yao. Haipaswi kuandaliwa na kuwasilishwa kwa kasi inayofuja akili ya wananchi na hivyo kufunika uongo, hila na husuda.

Tumesubiri miswada hii kwa muda mrefu. Ninaweza kuwasemea wengine kuwa tuko tayari kusubiri kwa "miezi mingine michache" ili tusome, tujadili na tupitishe kilichobora kwa ajili ya haki na uhuru wa watu wa Tanzania.

Tusome miswada hiyo kwanza. Wananchi waijadili kabla ya kupelekwa bungeni. Hapa, kuna mafao. Tutaboresha miswada kwa kuijenga vema kwenye misingi ya UHURU wa kujieleza ambao wananchi wamekuwa wakipigania. Tutasaidia serikali kuepuka aibu ya kuja kushurutishwa na wananchi na jumuia ya kimataifa, iwapo sheria mbaya itapitishwa na kukataliwa.

Ndimara Tegambwage
www.facebook.com/ndimara.tegambwage

No comments

Powered by Blogger.