Header Ads

LightBlog

KILIO CHA ALBINO KAMA MACHOZI YA SAMAKI?
SERIKALI NA ALBINO
(Msimu wa kuua albino)

Sikiliza na usikie
Wanasiasa wananena
Ni mwaka wa mapambano
Ni kufa tu!
Kupona majaliwa
Kinga walia kinga
Dawa! Dawa! Kinga!
Mtoa dawa analonga
Kipi kiende na kinga
Kipi kiende na ushindi.

Hapo! Albino wanawindwa
Albino wanakatwa viungo
Albino wanapotea
Albino wanauawa
Eti nini?
Kutengeneza dawa na kinga
Dawa za kwendea ikulu
Dawa za kwendea bungeni
Dawa za kupatia udiwani
Kinga dhidi ya washindani
Eti kikolezo albino.

Msimu gani huu
Wa mawindo ya urais
Mawindo ya albino?
Msimu gani huu
Wa mawindo ya ubunge
Mawindo ya albino?
Msimu gani huu
Mawindo ya udiwani
Mawindo ya albino?

Kumbe!
Ujinga waenda ikulu
Ujinga waenda bungeni
Ujinga waenda udiwanini
Ujinga wajaa mitaani
Ujinga unaoua
Unaoangamiza albino.

Na liserikali lipo
Lipo kama halipo
Halipo kama lipo
Wanasema lipolipo tu
Kwa maana ya halipo
Kama lipo mbona halipo
Mbona halitendi?
Albino wanaangamia.

Halipo limelala
Halipo limesinzia
Halipo linakoroma
Halipo halisikii
La nani sasa la nini
Albino wauliza;
Kama si lao si letu.

Kama si letu si lao
Sote twaweza toweka
Njia hii ya albino –
Albino Mtu
Na raia wa dunia.

ilichapishwa kwenye www.facebook.com/ndimara.tegambwage
3 Machi 2015.

No comments

Powered by Blogger.