Dk. Slaa hatarini
Tishio kwa maisha ya Dk. Slaa lisipuuzwe
Na Ndimara Tegambwage
MAISHA ya Dk. Willibrod Slaa yametajwa kuwa hatarini. Chama chake
kinasema kuna “mradi” wa kuzimisha maisha yake kwa kutumia sumu.
Dk. Slaa ni Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema). Mbunge kwa miaka 15. Mgombea urais mwaka 2010; na bado kuna
uwezekano wa kumtuma tena mwaka huu.
Dk. Willibrod Slaa
Dk. Willibrod Slaa
Kinachoshangaza wengi ni kutosikia taratibu za kupima afya ya Dk.
Slaa ili kuona kama tayari amedhurika.
Kama kuna taarifa za kutaka kumuua kwa sumu, ina maana anaweza kuwa amelishwa sumu tayari ambayo inaua taratibu.
Kama kuna taarifa za kutaka kumuua kwa sumu, ina maana anaweza kuwa amelishwa sumu tayari ambayo inaua taratibu.
Tishio kwa maisha siyo jambo la kudharau. Félix-Roland Moumié wa Cameroon aliuawa kwa
kula sumu aina ya thallium aliyowekewa
katika chakula, mjini Geneva, Uswisi tarehe 3 Novemba 1960. Taarifa zilitaja
maofisa wa Idara ya Usalama ya Ufaransa (SDECE) kuhusika na kifo hicho.
Félix-Roland Moumié
Félix-Roland Moumié
Moumié aliauwa miaka miwili baada ya kuchukua uongozi wa chama cha
kizalendo cha nchi hiyo – Union du Peuple Camerounais. Aliyekuwa kiongozi wa
chama hicho, Ruben Um Nyobe aliuawa kwa njama hizohizo Septemba 1958. Ni
mazingira hayahaya.
William Bechtel anayetajwa kutumia sumu hiyo kumuua Moumié,
alifahamika kuwa mwanachama wa kikundi cha kishushushu kilichoitwa Main Rouge
(mkono mwekundu); kilichokuwa na jukumu la kuua wazalendo Afrika ambao walipingana
na utawala uliokuwapo; na ulioungwa mkono na Ufaransa.
Alexander Litvinenko wa Urusi alifia mjini London, Uingereza, Novemba 2006,
wiki tatu baada ya kulishwa sumu iitwayo
polonium-210.
Alifariki akidai kuwa kilichomkumba kwa wiki tatu za mahangaiko,
kina mkono wa rais wa sasa wa Urusi, Vladimir Putin; madai ambayo yalileta
tetemeko katika uhusiano wa Urusi na Uingereza.
Alexander Litvinenko
Litvinenko, aliyekuwa ofisa katika idara ya ushushushu nchini
Urusi (FSB) na
shrikika la kijasusi la nchi hiyo (KGB), alikimbia mashitaka katika mahakama za Urusi.
Akiwa nchini Uingereza alifanya kazi katika idara za kishushushu –
za MI5 kwa mambo ya ndani ya nchi; na MI6 kwa ushushushu nje ya nchi. Alikufa.
Georgi Markov wa Bulgaria alifariki tarehe 7 Septemba 1978 kutokana na sumu iitwayo ricin. Mmoja wa
wapinzani wa serikali, Markov alifia mjini London alikokuwa mkimbizi.
Georgi Markov
Markov alivuka daraja la Waterloo. Akasimama kwenye kituo cha
mabasi ili aende shrika la utangazaji la Uingereza, BBC. Mara akasikia mchomo
kwenye paja lake la kulia. Alipogeuka alikuta mwanaume mmoja akiokota mwavuli.
Mwanaume huyo alimwambia, “Oh, samahani!” iliyosikika katika
lafudhi ya kigeni na siyo ile ya London. Halafu mwanaume huyo akasimamisha
teksi na kuondoka. Siku nne baadaye, Markov alifariki.
Kilichomuua Markov ni mwavuli ambao ncha yake ilikuwa na sumu. Kwa
mara nyingine, Urusi ilitajwa; mara hii kwa kushirikiana na Bulgaria “kuua
mpinzani.” Hata ndani au nje ya nchi, watakuwinda!
Daktari
alipokata kipande cha nyama pajani ambako Markov alichomwa na kukichunguza,
alikuta kitu kama kidonge chenye ukubwa wa milimita 1.52 kilichotengenezwa kwa
kemikali za platinum na iridium.
Ndani ya kidonge
hicho chenye matundu mawili yaliyozibwa kwa nta, ndiko ilikuwa imemwagwa sumu
ipatayo moja ya tano ya milimita (1/5).
Nta hiyo
iliyeyuka kutokana na joto la mwili na kuachia sumu iitwayo ricin kumiminika mwilini mwa Markov;
kushambulia tezi la limfu, kusababisha damu kuvuja mwilini; na katika siku ya
nne, figo na moyo kushindwa kufanya kazi. Alikufa.
Victor Yushchenko, rais wa sasa wa Ukraine aliponea chupuchupu mwaka 2004.
Alilishwa sumu aina ya dioxin. Uchunguzi
katika jaribio hili la kutaka kumuua, ulianza mwaka 2007, lakini hakuna hata
mshukiwa aliyewahi kufikishwa mahakamani.
Daktari wake, Mykola
Korpan anasema rais anaendelea vizuri na sura yake iliyokuwa imepotea katikati
ya vipele na msinyao, sasa inaanza kurejea kwa kasi.
Mwendesha
mashitaka mkuu wa Ukraine amekuwa akidai kuwa ni nchi tatu tu ambazo zinaweza
kuwa zimefanya jaribio hilo, “Urusi ikiwemo.” Urusi, hata hivyo, imekuwa
ikikana.
Yushchenko alilishwa sumu muda mfupi kabla ya kuchukua urais mwaka
2007, akimwondoa madarakani waziri mkuu Viktor
Yanukovych aliyekuwa akidaiwa “kushinda uchaguzi kwa wizi.”
Turudi nyumbani. Madai ya kuua,
kujeruhi, kupoteza na kudhuru kwa njia mbalimbali, hayawezi kupuuzwa. Hii ni
kwa sababu nchi hii siyo kisiwa; na hata visiwa vinafikika na kuzama katika
matendo ya kiharamia.
Ni Chadema waliokosesha Chama Cha
Mapinduzi (CCM) usingizi mwaka 2010; kwani waliporomosha umaarufu wa Rais
Jakaya Kikwete (wa 2005), kutoka asilimia 80.28 za kura hadi asilimia 62.83
katika uchaguzi uliopita.
Ni Chadema waliozoa, katika uchaguzi
wa serikali za mitaa mwaka jana, vijiji, vitongoji na mitaa mingi kuliko wakati
wowote tangu uchaguzi katika mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Ni Chadema na UKAWA sasa ambao
wameshikia bango kashfa hii na ile ambazo zimeikumba serikali ya Rais Kikwete na
kujipa jukumu la kueleza wananchi na dunia nzima kuwa “watawala wamechafuka; wamechoka,
wakae pembeni.”
Ni vyama vya upinzani ambavyo kila
kukicha vinazuiwa kufanya mikutano na kufanya maandamano. Vinafyatuliwa risasi
na mabomu ya pilipili.
Ni vyama hivi ambavyo viongozi wake
maeneo ya shamba – vijijini, wanatishwa, wanawekwa rumade bila sababu za
msingi; na mwaka jana wengi waliporwa fursa na haki ya kugombea nafasi
mbalimbali katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Katika mazingira haya, huwezi
kupuuzia kauli au tuhuma au madai tu kuwa kiongozi huyu au yule ameundiwa njama
za kumjeruhi, kumuua au kumpoteza. Ni mazingira tete. Ni mazingira hatarishi.
Ni wakati wa kujenga shaka kwa kila kitu na kila kauli.
Mazingira haya katili yanaimarishwa
na kauli, kwa mfano kutoka Sauti ya Kisonge (Mwembe Kisonge) Zanzibar, kuwa wao
(CCM) hawatoi “nchi kwa yeyote.”
Ni kauli zinazoimarisha utukutu
katika siasa; hadi viwango vya wanasiasa wa CCM kuviambia vyama vingine vya
siasa na kuvitolea kauli kama, “ikulu mtaisikia redioni!”
Hizi ni kauli za ujambazi kisiasa.
Haziashirii mwafaka wa aina yoyote. Ni kufa tu. Hakuna kupona. Katika mazingira
haya, tena karibu na uchaguzi mkuu, madai na tuhuma za aina yoyote ile zaweza
kuwa kweli.
Nchi hizi – Tanganyika na Zanzibar,
ni zetu sote. Kupata mwafaka – kwa njia ya mashindano huru na haki – kwenye
sanduku la kura, ndiko kila mmoja mwenye nia safi anatafuta na angetarajiwa
kutafuta.
Kuua kwa sumu au silaha, visiwe
sehemu ya msamiati, vitendo, wala imani za Watanzania. Dk. Slaa awepo kama
wengine. Ulingo wa siasa uwe wazi na anayetaka kushindana naye apande jukwaani
tumuone: Pale!
0713 614872
ndimara@yahoo.com
Imechapishwa gazeti la MAWIO, 12 Machi 2015.
1 comment
We From SEO Milanisti Introduces Its Sales Sells Herbal Products Men And Women ALL PRODUCTS FROM our clients in Down's.
pembesar penis | obat pembesar penis
parfum pemikat wanita | perangsang wanita
Post a Comment