TUSOME WOTE, TUSIKIKE WOTE
Rafiki yangu amenipelekea andishi hili. Nimelisoma. Naona niliweke hapa nawe uweze kulisoma. Haya!
Wanaopaswa kuwa gerezani,
nao wanatafuta
urais?
Na Lawrence Kilimwiko*
NANI
wanataka kuwa rais nchini Tanzania? Wana nini? Historia yao ikoje? Wanaishi
maisha ya kiwango gani? Wana mali kiasi gani au ni masikini kiasi gani?
Wanalipa kodi au ni wakwepa kodi?
Nani
anafahamu yeyote anayetaka kugombea urais ili atupe taarifa na ikiwezekana
atusaidie kujibu maswali yaliyoulizwa hapo juu?
Tanzania
inaingia katika uchaguzi mkuu wa 2015 ikiwa katika mazingira yanayohitaji
uchunguzi na uchambuzi wa aina ya kipekee.
Kuna watuhumiwa
wa makosa makubwa, ukiwemo ukwapuaji Benki Kuu (BoT) wa zaidi ya shilingi
bilioni 290. Unaitwa kashfa ya EPA. Kuna
uwindaji haramu wa tembo na faru na usafirishaji nje ya nchi wanyama hai kutoka
mbugani. Kuna uzawadiaji mikataba kama ule wa Richmond wa kufua umeme wa
dharura ambao, hata hivyo, haukupatikana.
Kuna
wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya
ambao Rais Jakaya Kikwete aliwahi kuliambia taifa kuwa ana orodha yao wote;
lakini hajawahi kuiweka wazi hadi leo.
Kuna wezi wa
fedha za umma kupitia akaunti ya Tegeta Escrow ndani ya BoT. Hata watumishi wa
ikulu wako kwenye orodha ya waliochotewa mamilioni ya shilingi.
Je, miongoni
mwa wote hawa na wengine, hakuna anayetaka kugombea urais? Hakuna ambao wamejichomeka
kwenye ulingo wa siasa ili kuepuka kushitakiwa; na sasa wanatafuta urais ili
kuficha zaidi sura na ukwasi wao unaotokana na wizi, ukwapuaji na ujambazi
kiuchumi?
Tanzania
haiwezi kuwa tofauti. Angalia Italia. Silvio Berlusconi, waziri mkuu wa zamani
wa Italia, ni mmoja wa mamilionea wa
ki-Italia aliyekuwa akimiliki utajiri wa thamani ya dola za Marekani 6.2
bilioni.
Historia yake
inaonyesha kuwa alianza maisha akiwa mchezadisko kwenye vilabu vya pombe na
vingine. Baadaye alisoma na kuhitimu sheria mwaka 1961.
Biashara
zake zimo katika maeneo kadhaa kuanzia kampuni ya ujenzi, televisheni kubwa ya
Telemilano na nyingine mbili, kampuni ya uchapaji magazeti ya Giomele, redio,
Shirika la habari la Rai pamoja na
kumiliki klabu maarufu ya kandanda ya A.C.Milan.
Mwaka 1993
Berlusconi alianzisha chama cha siasa cha Forza
Italia na kujitumbukiza kwenye siasa.
Alitambua mapema kabisa kuwa ili aweze kufanikisha malengo yake; na hasa
kukwepa mkono wa sheria kutokana na kufanya biashara nyingi haramu, ilikuwa
muhimu kwake kuingia katika siasa – ili apate mahali pa kujikinga.
Njama hizo
zilimsaidia sana Berlusconi kukwepa mkono wa sheria kutokana na makosa ya
kukwepa kodi, udanganyifu, rushwa na
hata ngono. Kwa ufupi, maisha ya Berlusconi yamejaa mchanganyiko wa sifa
na kashfa.
Alikuwa
waziri mkuu wa Italia kwa vipindi vitatu, na mtawala aliyekumbwa na kashfa
nyingi na hata kuhukumiwa kwenda jela. Lakini hakuwahi kutumikia jela kutokana
na kujificha kwenye kichaka cha siasa.
Hata hivyo,
baada ya kukwepa kwenda jela kutokana na makosa ya rushwa, ubakaji, kukwepa
kodi na udanganyifu; hatimaye alijikuta akining’inizwa baada ya kutiwa hatiani
na mahakama kwa kosa la kukwepa kulipa kodi mwaka 2013.
Kama hiyo
haitoshi, alihukumiwa pia adhabu ya miaka saba jela kutokana na kufanya ngono
na “kahaba” aliye chini ya umri wa mtu mzima. Adhabu hiyo, hata hivyo,
ilibadilishwa na kuwa ya kutumikia jamii kwa mwaka moja kutokana na umri wake
mkubwa – miaka 77.
Hiki
kilikuwa kitu kipya kabisa kwa raia wa Italia ambao walifikia kuamini kwamba
Silvio Berlusconi haguswi na mkono wa sheria kutokana na ukubwa kisiasa na
utajiri wake.
Nchini
Tanzania, wenye utajiri mkubwa walianza kwa kujipenyeza kwenye michezo kupitia
vilabu vikubwa. Ukweli ni kwamba kelele za wanachama na mashabiki wa klabu, huweza
kumsetiri mwizi na hata kuhakikisha kuwa hakabiliwi na mkono wa sheria.
Baada ya
kugundua mbinu hiyo inafanya kazi, inawezekana sasa kuna waliojiingiza katika siasa,
tena kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) au vyama vingine.
Siyo siri
kwamba wizi na ufisadi wote uliotajwa hapo juu, umo nchini Tanzania. Siyo siri
kwamba wizi mkubwa umewahusu viongozi wa serikali ambayo inaongozwa na CCM.
Siyo siri
kwamba miongoni mwa wanaotaka kugombea urais, Oktoba mwaka huu, tena kupitia
CCM, wamo watuhumiwa wakuu wa ama hujuma, wizi au ukwapuaji mabilioni ya shilingi kupitia
wizara ya fedha na BoT.
Ripoti ya
hivi karibuni ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa fedha za serikali (CAG);
inaonyesha kuwa serikali inatumia vibaya fedha inazopewa; inapoteza fedha, na
watumishi wake waliokabidhiwa dhamana kuu, wanatafuna fedha kama njugu kutoka
shamba la bibi!
Ni kula!
Kula! Kula! Ni kula faida na ziada; na hatimaye kula mbegu; kana kwamba mwakani
hakuna kupanda!
Kinachostua
wananchi wengi wapenda nchi yao, ni kuona waliotajwa na CAG – na huwataja mwaka
hadi mwaka – kuwa watuhumiwa ubadhilifu,
wezi moja kwa moja, wakwapuaji na, au waandaa mipango ya uhujumu uchumi; ni
miongoni mwa wanaotangulia kutangaza kugombea urais na ubunge.
Yuko wapi
mwandishi wa kuwaanika hao? Yuko wapi mwandishi wa kuwahoji?
Kwa wizi wa
waziwazi alioanika CAG, kuna wanaopaswa kuwa jela wakati huu au wakati wa
uchaguzi, Oktoba. Serikali inayowaajiri, inayowakinga, inayostahili kuwafukuza
au kuwakamata na kuwashitaki, iko kimya.
Ni serikali
hiyohiyo ya chama hichohicho, inayotuhumiwa na kushutumiwa na CAG ambayo inasimamia
upatikanaji rais kutoka miongoni mwa watuhumiwa - Chama Cha Mapinduzi.
Katika
mazingira haya, hakika hakuna kulala – kwa upande wa CCM na serikali yake. Wanataka
kuhakikisha kuwa anapatikana mgombea na labda baadaye, rais atakayefunika kombe
ili mwanaharamu apite.
Wanataka
rais aendelee kutoka katika chama chao – CCM – kilichojaa viongozi wa serikali
wanaotuhumiwa na kushutumiwa kwa wizi na ufisadi wa viwango mbalimbali; kuanzia
kijijini hadi ikulu.
Wanataka
kuendelea kujenga kinga kwa wahalifu wanaowafahamu, waliowaweka madarakani,
waliowalea na watakaoendelea kulinda, kuhifadhi na hata kuenzi genge la wezi wa
tunda la jasho na damu ya Watanzania.
Chama Cha
Mapinduzi kinaweza kufananishwa na mtu mmoja aitwaye Robert Mugabe, rais wa
Zimbabwe, ambaye aliapa kufia ofisini kwa hofu ya kukamatwa na kushitakiwa,
pale tu atakapotoka ikulu.
Kuiba fedha
za umma, kushiriki kuiba, kuruhusu kuiba na, au kunyamazia kuiba, ni kosa kubwa
kimaandili, kisiasa na kisheria.
Wizi
usioadhibiwa, au usiokemewa; na badala yake ukawa wizi wa kuendeleza kwa
“gharama yoyote ile,” alimradi mtu amebaki madarakani; ndio unafanya vyama na
watawala watake kufia madarakani; kama inzi anavyofia kwenye kidonda. Hawaoni
usalama wao nje ya madaraka ya dola.
Watajipitisha
makanisani, misikitini, misibani, kwenye harusi na matanga; wakijifanya wacha-Mungu
na wenye kuwahurumia wasumbukao kwa njaa, maradhi na kiu; wakiwalaghai watu kwa
vitenge, kanga, pilau au kofia za chama au ahadi za ajira, ili wapate kubaki
madarakani.
Hakika, Watanzania
wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuacha ngonjera za kuthamini “uasisi” na “kuleta
uhuru.” Siyo siri kwamba vyama vilivyopigania uhuru Afrika na kwingineko, vingi
viliingiliwa na kirusi cha wizi na ufisadi na hatimaye kuangushwa na umma.
Tanzania
siyo kisiwa! Watanzania wanaona, kusikia na kunusa. Kama mwizi wa mali yao
hakamatwi, basi wasiomkamata wasiwaombe kura ya kuendelea kutawala. Au
wakiwaomba kura, basi wawakatalie.
CCM haikuundwa
ili ilee wezi, iwatukuzwe na iwaweke madarakani. Hapana! Kwa kauli za Mwalimu
Nyerere, iliundwa kulinda na kudumisha uhuru wa nchi na raia wake; kusimamia
haki na maendeleo ya wakulima na wafanyakazi, kuhakikisha kuwa matumizi ya
utajiri wa taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi, na hasa jitihada za
kuondosha ujinga, maradhi na umaskini.
Kama
walioahidi na wanaopaswa kuamini hayo ndio wenye serikali inayoanikwa na CAG
kuwa ni badhilifu kupindukia; basi wameandika barua ya maombi kwa umma wakitaka
kufukuzwa kazi. Watafukuzwa!
Kuwafukuza
kazi ni kutowachagua; lakini kwanza ni kuwataka wagombea wao, hasa wanaotaka
urais, kutaja walikopata fedha wanazomwaga misibani, michezoni, misikitini na
makanisani; na jinsi watakavyozirejesha.
Isemwe tu basi,
kwamba CCM bado ina nafasi ya kujisahihisha kwa kuwaengua wagombea urais,
ubunge na udiwani – wote wasio waadilifu
– wahujumu, wezi, matapeli, walafi, wababaishaji na mafisadi.
Kama hilo
litaigharimu kushindwa katika uchaguzi mkuu huu, isiwe hoja. Wakae pembeni.
Wajipange upya na kurudi kwenye misingi walioyiacha, ndipo warejee kwenye
kinyang’anyiro wakiwa wasafi na wenye sifa ya kushindana na hata kushinda.
*Lawrence Kilimwiko
ni mshauri wa habari na mwandishi wa vitabu kutoka asasi ya Interlstar
Consults, Dar es Salaam: lkilimwiko2015@gmail.com, Mob. 0754 321308.
No comments
Post a Comment