Header Ads

LightBlog

UMASIKINI TISHIO LA AMANI


                       

Padri aonya juu ya umasikini uliokithiri

Na Lilian Tegambwage

PADRI Dennis Massawe wa Parokia ya Tegeta nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam amesema, “…wanyonge wa nchi hii wakichoka unyonge wao, yatatokea machafuko makubwa.”

“Tuombe kwa ajili ya wanyonge. Hawa ni wale wanaolala njaa; wanaokwenda hospitali na kuambiwa hakuna dawa; watoto wao wanashindwa kwenda shule kwa kuwa hawana daftari…” amesema Padri Massawe.

Alikuwa akihubiri leo Jumanne, kwenye Misa ya Krismasi katika Kigango cha Mtakatifu Petro cha Parokia ya Tegeta kilichoko Tegeta Masaiti.

Amesema wanyonge wakichoka Tanzania kutatokea “machafuko makubwa sana;” akiongeza, “Tuombe sana kwa ajili yao. Tuombe wasichoke.”

Mahubiri ya Padri Massawe yamechukuliwa kama njia mojawapo ya kukumbusha na kuonya watawala kuhusu “bomu la umasikini” ambalo linaweza kulipuka wakati wowote pale waliotupwa nje ya mzunguko wa kunufaika na raslimali za taifa watakapoamka na kudai haki zao.

Kwa upande mwingine, padri alikuwa akiwatekenya wanyonge wenyewe kuvua unyonge wao na kuelekeza madai ya haki na matakwa yao kwa waliopewa mamlaka ya utawala wa nchi.

Kauli ya padri ilifananishwa na mahubiri ya mapadri wa nchi za Amerika Kusini ambao miongo minne iliyopita walianza kuhubiri kwamba sharti wananchi wao waanze kuishi hapahapa duniani maisha bora ambayo wanahubiriwa.

Ni kauli hizi ambazo ziliunganisha waumini Wakristo na watu wa madhehebu mengine, kwa upande mmoja, na wanaharakati na wapigania mabadiliko, kwa upande mwingine, katika kupigania haki na usawa katika nchi zao.

Akigeukia waumini, Padri Massawe amesema, “…wengine tumekuwa tunakuja hapa kwa mazoea tu. Tunakuja kanisani kujifurahisha. Tukitoka kanisani, sisi ndio tunakuwa vinara wa maovu kama ufisadi, ngono, wizi na chuki.”

Padri alitoa mfano wa waziri mmoja wa India ambaye alimnukuu akisema anampenda sana Yesu Kristo kwa kuwa amefanya kazi kubwa katika dunia; lakini hapendi wakristo kwa sababu hawaishi kama Yesu na kama biblia inavyosema.

Biblia, kiongozi cha madhehebu ya Kikristo, ni moja ya vitabu vilivyosomwa na kuchambuliwa sana duniani; kikiwa kimesomwa na wanaoamini na wasioamini katika madhehebu hayo.

Leo ni siku ya Krismasi inayoadhimishwa rasmi na wakristo kote diniani kwa kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo zaidi ya miaka 2,000 iliyopita.

Kigango cha Mtakatifu Petro kilifurika waumini waliotumbuizwa na kwaya ya Mtakatifu Andrea ya kigangoni hapo.

Padri aliwaombea waumini wote akisema washerehekee Krismasi kwa amani.

Katika hatua nyingine, washiriki walisimama kwa dakika moja kukumbuka muumini maarufu Erasmus Lunaga, mwenyekiti wa Jumuiya ya Timotheo, Machakani-Sinza, aliyefariki siku ya Krismas mwaka jana.
(Lilian anasomea diploma ya IT (University of Dar es Salaam Computing Centre). Alikwenda kanisani leo asubuhi. Aliporudi nikamwomba anieleze kwa maandishi, kile ambacho kimehubiriwa. Akakaa chini na kuandika taarifa hiyo hapo juu. Nimeongeza aya moja tu. Naona anaweza huko aendako).
  •  Picha juu: Polycap Kardinali Pengo
 
 
 
Powered by Blogger.