UMASIKINI TISHIO LA AMANI
Padri aonya juu ya umasikini
uliokithiri
Na Lilian Tegambwage
PADRI Dennis Massawe wa Parokia ya Tegeta nje
kidogo ya jiji la Dar es Salaam amesema, “…wanyonge wa nchi hii wakichoka
unyonge wao, yatatokea machafuko makubwa.”
“Tuombe kwa ajili ya wanyonge. Hawa ni wale wanaolala njaa; wanaokwenda hospitali na kuambiwa hakuna dawa; watoto wao wanashindwa kwenda shule kwa kuwa hawana daftari…” amesema Padri Massawe.
Alikuwa akihubiri leo Jumanne, kwenye Misa ya
Krismasi katika Kigango cha Mtakatifu Petro cha Parokia ya Tegeta kilichoko
Tegeta Masaiti.
Amesema wanyonge wakichoka Tanzania kutatokea
“machafuko makubwa sana;” akiongeza, “Tuombe sana kwa ajili yao. Tuombe
wasichoke.”
Mahubiri ya Padri Massawe yamechukuliwa kama
njia mojawapo ya kukumbusha na kuonya watawala kuhusu “bomu la umasikini”
ambalo linaweza kulipuka wakati wowote pale waliotupwa nje ya mzunguko wa
kunufaika na raslimali za taifa watakapoamka na kudai haki zao.
Kwa upande mwingine, padri alikuwa
akiwatekenya wanyonge wenyewe kuvua unyonge wao na kuelekeza madai ya haki na
matakwa yao kwa waliopewa mamlaka ya utawala wa nchi.
Kauli ya padri ilifananishwa na mahubiri ya
mapadri wa nchi za Amerika Kusini ambao miongo minne iliyopita walianza
kuhubiri kwamba sharti wananchi wao waanze kuishi hapahapa duniani maisha bora
ambayo wanahubiriwa.
Ni kauli hizi ambazo ziliunganisha waumini
Wakristo na watu wa madhehebu mengine, kwa upande mmoja, na wanaharakati na
wapigania mabadiliko, kwa upande mwingine, katika kupigania haki na usawa
katika nchi zao.
Akigeukia waumini, Padri Massawe amesema,
“…wengine tumekuwa tunakuja hapa kwa mazoea tu. Tunakuja kanisani
kujifurahisha. Tukitoka kanisani, sisi ndio tunakuwa vinara wa maovu kama
ufisadi, ngono, wizi na chuki.”
Padri alitoa mfano wa waziri mmoja wa India
ambaye alimnukuu akisema anampenda sana Yesu Kristo kwa kuwa amefanya kazi
kubwa katika dunia; lakini hapendi wakristo kwa sababu hawaishi kama Yesu na kama
biblia inavyosema.
Biblia, kiongozi cha madhehebu ya Kikristo, ni
moja ya vitabu vilivyosomwa na kuchambuliwa sana duniani; kikiwa kimesomwa na wanaoamini
na wasioamini katika madhehebu hayo.
Leo ni siku ya Krismasi inayoadhimishwa rasmi
na wakristo kote diniani kwa kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo zaidi ya
miaka 2,000 iliyopita.
Kigango cha Mtakatifu Petro kilifurika waumini
waliotumbuizwa na kwaya ya Mtakatifu Andrea ya kigangoni hapo.
Padri aliwaombea waumini wote akisema
washerehekee Krismasi kwa amani.
Katika hatua nyingine, washiriki walisimama
kwa dakika moja kukumbuka muumini maarufu Erasmus Lunaga, mwenyekiti wa Jumuiya
ya Timotheo, Machakani-Sinza, aliyefariki siku ya Krismas mwaka jana.
(Lilian anasomea diploma ya IT (University of Dar es Salaam Computing Centre). Alikwenda kanisani leo asubuhi. Aliporudi nikamwomba anieleze kwa maandishi, kile ambacho kimehubiriwa. Akakaa chini na kuandika taarifa hiyo hapo juu. Nimeongeza aya moja tu. Naona anaweza huko aendako).
Picha juu: Polycap Kardinali Pengo
3 comments
Mantap, i like it
Anaweza aendeleeeee
Anaweza aendeleeeee
Post a Comment