Nape, CCM na Kadi ya Dk. Slaa
Mjadala Kadi ya Dk. Slaa 'kiinimacho'
Sina kadi ya Tanganyika African National Union
(TANU) - chama kilichoongoza wananchi kupigania uhuru. Sikuwahi kukata kadi ya
chama hicho. Lakini nina kadi ya Umoja wa Vijana wa TANU (Tanu Youth League -
TYL). Nilikuwa mwanachama na mwenyekiti wake nikiwa sekondari, Kahororo.
Niliishia hapo. Sikuwahi kuwa na kadi ya TANU. Sikuwahi kuwa na kadi ya litoto
lake CCM. Sikuwahi kuwa na kadi ya Umoja wa Vijana wa CCM.
Lakini bado nina kadi yangu ya TYL. Kadi hii bado imewekwa
mahali salama. Imefanyiwa uzuderi (lamination) isije kupauka. Itakaa sana.
Siichani. Siitupi. Simpi mtu. Ni mali yangu. Acha historia inukuu ushiriki
wangu hata katika kuchanga senti 50 kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Vijana,
Lumumba, Dar es Salaam ambalo sasa "vijana" wa chama kinachoheshimu
na kulinda mafisadi (CCM) wameuza kwa pesa mbili.
Pointi:
Kadi ni mali yangu. Rudi Darasa la Kwanza miaka yetu. Mwalimu anaanza
kutufundisha Kiingereza: This is my book. It is my book. It is mine.
Sasa rudi kwenye kadi: This is my TYL card . It is my card. It is mine. Nikitaka kugawa, naigawa. Nikitaka kutupa, naitupa. Nikitaka kuchoma moto, naichoma. Nikitaka kuuza kwenye mnada, naiuza. Sasa kwanini Dk. Slaa asibaki na kadi yake na hata nyingine zozote atakazoweza kuwa nazo (sasa na baadaye) hadi pale atakapotaka kuachana nazo?
Bali mjadala wa "Kadi ya Dk. Slaa" una maana pana.
Unaonyesha jinsi viongozi wa chama kilichopanga ikulu kwa miaka 51 wanavyoweza
kuacha hoja kuu za kufikirisha mtu binafsi na jamii; na badala yake
kujiviringisha na kuviringisha wananchi katika malumbano dhaifu (triviality)
ili kupoteza muda na kuondoa akili zao kwenye hoja kuu za wakati tuliomo.
Ndiyo, ni ndoana. Lakini nani ataimeza wakati anajua ni ndoana?
ndimara
No comments
Post a Comment