Header Ads

LightBlog

UVUNJAJI HAKI ZA BINADAMU + +

Viongozi waoga, katili wa Bukombe

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI viongozi wa wilaya ambao uwezo wao wa kufikiri ni mdogo na ambao wana haraka na uchu wa kutenda makosa.

Viongozi wa aina hiyo ni kama aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Bukombe, mkoani Shinyanga, Magesa S. Mulongo na kamati ya ulizi na usalama ya wilaya hiyo ambao wanalalamikiwa kwa kuwafukuza baadhi ya waandishi wa habari kutoka wilayani humo.

Madai ya mkuu wa wilaya na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama yametajwa kuwa “waandishi wa habari kukiuka maadili ya kazi zao.” Hapa ndipo penye mnofu wa mjadala na uchambuzi.

Hivi nani hasa anapaswa kujua maadili ya kazi au taaluma fulani? Naomba kujibu haraka. Ni yule mwenye taaluma au kazi husika. Kwamba muhusika anaweza kutenda kinyume, haina maana kwamba hajui maadili. Anaweza kuwa ananufaika binafsi kwa kutofuata maadili.

Kama kuna mwingine ambaye anaweza kuwa anajua maadili ya kazi au taaluma yoyote, ni yule anayefanya utafiti na anayejali kufuatilia misingi na utekelezaji wa kazi inayohusika.

Najenga mashaka juu ya uwezo wa mkuu wa wilaya ya Bokombe kujua kinachoitwa “maadili ya waandishi wa habari.” Najenga mashaka pia juu ya uwezo wa wajumbe wa kamati ya ulizi na usalama wa wilaya ya Bokombe kujua nini hasa kinaitwa uandishi wa habari, unavyofanywa na maadili yake.

Kwa nini? Kwa sababu viongozi wa ngazi hii wameumbwa kwa woga. Ni katope wa tuhuma, shutuma na hata malalamiko. Wanayeyuka kwa sentensi moja ambayo mwandishi amenukuu kutoka mdomoni mwa mwananchi mmoja mwenye malalamiko halali.

Najenga mashaka, juu ya tabia ya viongozi wa wilaya, ya kuogopa hata kishindo cha paka, inavyoweza kujua kazi na maadili ya waandishi wa habari.

Naharakisha kusema, tena kwa uhakika, kwamba hakuna hata mmoja kati ya walioshiriki uamuzi wa kufukuzwa waandishi wa habari kutoka wilayani Bukombe, ambaye anajua hata msingi mmoja na muhimu – ule wa kuandika au kutangaza ukweli – wa taaluma ya habari.

Wanasiasa hawa wa ngazi ya wilaya, kama baadhi ya wale wa ngazi ya kitaifa, na hasa tunapojadili suala la habari, uhuru wa habari na haki na uhuru wa kupashana habari, siyo watu wa kutumainiwa kutoa maamuzi.

Watu waliotengenezwa ama kwa hariri au mabonge ya barafu, ni watu hatari sana. Watachanika kwa upepo mdogo au watayeyule kwa joto la mpakato tu. Kwa hiyo sharti waishi kwa mashaka na woga, wakidhani kila mmoja anataka kuwachana au kuwayeyusha.

Wanasiasa wa Bukombe wanawatilia mashaka waandishi wa habari. Wanawaona, wanaamini, na ni kweli, kwamba hata waandishi wanawaona viongozi hao. Lakini viongozi wanataka sura zao, matendo yao na hata fikra zao, viishie Bukombe ambako wamewafungia wananchi katika giza la taarifa na kuwaaminisha kuwa wanafikiri kwa niaba yao.

Yeyote anayeweza au anayejaribu kuonyesha sura halisi ya wanasiasa hao; jinsi wanavyotenda na wasivyotenda; jinsi walivyoshindwa au wasivyoweza kutenda, lazima ataonekana mbaya, mchafu, mfitini, mchochezi.

Niliwahi kufukuzwa mkoani Ruvuma. Ilikuwa katika miaka ya 1970. Mkuu wa mkoa Athumani Kabongo, akikaa na kamati yake, alinilazimisha kuhudhuria kikao ndani ya ofisi ya TANU na kudai mbele ya wajumbe kuwa nimeandika uwongo.

Alichukua hatua baada ya siku tatu za kuzungukia kata mbalimbali, ikiwemo kata ya Kilagano kujionea mwenyewe na wajumbe wake kwamba mahindi yalikuwa yanaoza wakati taifa likikabiliwa na njaa kubwa. Nilikuwa nimeandika taarifa hizo.

Amri ya mkuu wa mkoa ilitolewa saa mbili tu baada ya mkoa kuunda kile ulichoita Operesheni Okoa Mazao ikisimamiwa na mkuu wa polisi mkoani. Angalia unafiki huu wa kiwango cha juu!

Lakini niliwaambia viongozi kuwa sifukuziki. Badala ya kuondoka mkoani, nilichukua usafiri wa lori na kujichimbia wilayani Mbinga ambako niliibua makali zaidi.

Nakumbuka mwandishi wa Radio Tanzania wakati huo, Abysai Stephen alinikuta Mbinga na kunieleza kuwa ameagizwa na mkuu wa mkoa anambie kuwa niondoke mkoani vinginevyo wangenikamata na kunifunga.

Kuna somo hapa. Nilikataa kuondoka mkoani. Niliendelea kuandika. Viongozi na polisi waliendelea kunisaka. Mkurugenzi wa wilaya aliona umuhimu wa kazi yangu. Akanipa gari la kwenda hadi Lipalamba na Mitomoni, kwenye mpaka wa Tanzania na Msumbiji. Niliibua mengi.

Kwa ukaidi huu na kwa kazi iliyojaa usahihi wa aina ya kipekee, umma ulinufaika na serikali ilijua nani alikuwa anasema uwongo. Kilichofuatia ni viongozi wengi kuhamishwa, akiwemo mkuu wa mkoa, Athumani Kabongo.

Wanasiasa wa ngazi ya kijiji, kata, wilaya, mkoa, taifa, hata kokote walipo, hawana uwezo wala mamlaka ya kuamua juu ya taaluma ya habari isipokuwa kwa sheria kandamizi ambazo wamezitunga.

Hawana uelewa katika taaluma hii. Hawana nia njema kwa uandishi na waandishi. Lakini hakuna anayewazuia kuwa na maoni. Acha wawe hivyo, nasi tuwashangae. Lakini wakitaka kuchukua hatua yoyote ya kuzuia waandishi kufanya kazi yao, sharti wafikirie kwanza uhuru wa wengine.

Mwenye uwezo wa kutoa uamuzi juu ya malalamiko yao ni mahakama. Waende huko. Washindwe. Warudi kwenye vigoda vyao na kupiga miayo; kwani katika mazingira haya, hakuna mahakama yenye uwezo wa kutoa hukumu ya kuzuia, kuzima wala kunyang’anya uhuru wa habari.

Lakini sharti waandishi wa habari nao wakatae kufukuzwa. Ukondoo haulipi. Afadhali mwandishi akakamatwa, kuswekwa lupango na kuondolewa kesho kwa amri ya mahakama, kuliko kubaki huru mitaani lakini kichwa chini kama kondoo.

Hapo ndipo somo litakolea. Tujifunze kusema: Hapana.

0713 614872
ndimara@yahoo.com

(IMECHAPISHWA KATIKA GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI)

No comments

Powered by Blogger.