'WAUMINI' WANAOANGAMIA KIMYAKIMYA
Serikali isiyojali maisha ya ‘Masalia’
Na Ndimara Tegambwage
SITAKI serikali ichukue nafasi ya mtazamaji tu pale maisha ya watu yanapokuwa hatarini; hata kwa madai kuwa huo ni utashi wa waliomo hatarini.
Hili linahusu wale wanaojiita Wasabato Masalia. Hii ni klabu ya wanaojiita waumini katika imani fulani wanayoona inaweza kuwafikisha kwa Mungu au kuwaweka katika njia ielekeayo kwake.
Waumini hawa wanajiita “masalia.” Kwa jina hilo tu, utaona kuwa wao ni “mabaki.” Yaweza kuwa mabaki baada ya wenzao kuangamia au kupotea. Yaweza kuwa mabaki baada ya kuchekecha na wao kubaki makapi. Yaweza kuwa mabaki kwa uamuzi wao kuwa watabaki walivyo na hawataki kubadilishwa.
Katika hali ya kawaida, masalia ni masazo; yale yaliyoachwa, siyo kwa utashi wa masazo bali kwa utashi wa waliokuwa na uamuzi. Hatua ya kijiita masalia au masazo ni hatua ya kukata tamaa. Hatua ya kuwekwa pembeni na hata kutengwa.
Wasabato Masalia walitoka mikoa mbalimbali nchini na kwenda Dar es Salam kwa shabaha moja: Kutumia uwanja wa ndege wa kimataifa – Julius Nyerere Airport (JNA) kwenda sehemu mbalimbali za dunia kuhubiri “Neno la Bwana.”
Kilichowakwamisha hakina uhusiano na masuala ya jinsia; kwamba walitaka kuhubiri “Neno la Bwana” bila kuhubiri “Neno la Bibi.” Walikwamishwa na sheria, kanuni na taratibu za safari.
Walitaka kukaa uwanja wa ndege JNA, hadi hapo “Bwana” atakapoamua kuwachukua, tena kwa ndege, bila wao kuwa na pasipoti; bila vibali vya kusafiria kwenda nchi za nje (viza) na bila tiketi.
Hiyo ni miezi tisa iliyopita. Walikuwa 52; sasa wamebaki 30. Kuna madai kuwa hao pungufu (12) wameachana na imani isiyotekelezeka. Hilo laweza kuwa kweli au si kweli. Bali hao 30 bado wanakaa Tabata-Segerea, kwenye viunga vya Dar es Salaam wakisubiri “meli ya angani” iwapeleke kuhubiri nchi za nje.
Kwa kipindi chote, serikali imekaa kimya, ikiangalia mabaki ya wasabato yakilazimisha pumzi kutoka ndani ya miili yao, lakini bila mafanikio. Na kwa kuwa wameachwa bila ukaguzi, uangalizi na ufuatiliaji wa karibu, yawezekana hata hao 20 wanaosemekena kukana imani, siyo kwamba wamehama kambi, bali wamekufa.
Usiri uliowaweka pamoja katika kuamini kisichoaminika wala kuaminiwa; ni usiri huohuo unaoweza kuwafanya wasitoe taarifa juu ya wagonjwa na waliokufa.
Kushindikana kwa utekelezaji wa mpango wao; au tuseme ile hatua ya Mungu ya kukataa kuwapelekea ndege isiyodai pasipoti, nauli na tiketi wala viza; mawili haya yanawafanya waone aibu na hivyo kushindwa kurejea kwenye jamii za awali.
Ving’ang’anizi au masalia waliosalia kati ya 50 wa awali, waweza kuitwa wenye “imani kali.” Maana ya imani kali (entuhi), ni ukaidi usio na mipaka; usiojali hoja, fikra wala hekima. Katika hili mambo kadhaa yaweza kujitokeza.
Kwanza, masalia waweza kuendelea kuishi Segerea; wakiugua na hata kufa mmojammoja na kimyakimya, hadi pasiwepo na masalia wa masalia.
Pili, masalia waliosalia au watakaokuwa wamesalia hapo baadaye, waweza kuamua kutorudi makwao; wakatawanyika miongoni mwa jamii wanamoishi na kuwa mzigo kwa jamii hiyo ambako watakuwa ombaomba hadi mwisho wa uhai wao.
Tatu, masalia wa masalia waweza, hasa baada ya kuona Mungu amekataa au amedharau au ameshindwa kuwapelekea ndege, kuamua kuondoa maisha yao, tena kwa pamoja, ili kukwepa kimbunga cha aibu na hasira ya wanafamilia wao.
Nne, masalia wa masalia waweza kuanzisha ushawishi mpya; tena kwa nguvu zaidi; kupata wafuasi wengine wanaojifikiria kuwa wameachwa na kwa pamoja kuunda jamii ya waliosazwa – wasiolima, wasiochuuza wala kufanya kazi yoyote, bali kuwa waumini wa kisichoaminiwa na kubaki ombaomba.
Tano, masalia wa masalia wanaendelea kujamiiana na kuzaa watoto masalia wa masalia wa masalia. Kizazi hiki ni bomu kubwa na hatari kwa maisha yao wenyewe na taifa kwa ujumla.
Sita, masalia waliofikia hatua ya kujiaminisha kuwa Mungu atawapelekea ndege ili wasafiri bwerere kwenda watakako duniani kote, tayati ni watu hatari kwao wenyewe na jamii wanamoishi. Mbegu yao yaweza kuzaa gugu lenye uwezo wa kuangamiza bustani za fikra na hekima.
Lakini serikali imekaa kimya juu ya maisha ya hatari ya wasabato masalia. Na hapa hatuongelei imani. Hakuna imani hapa! Kuna kuemewa kwa akili ambako kuna msingi katika mambo mengi yakiwemo, umasikini uliokithiri na ujinga uliowazonga na kuwafanya kujifungia na kufanya kazi moja tu maishani: Kuomba.
Alikuwa Mama Theresa wa Calcutta (mzaliwa wa Albania); mtumishi wa watu aliyejizolea heshima na utukufu kwa njia ya kutumikia watu. Siku moja alikuta masista aliokuwa akifanya nao kazi wametoka kwenda “kusali.” Aliwashangaa sana.
Katikati ya kitongoji cha Calcutta; jiji linalochukuliwa kuwa chafu zaidi na lililojaa masikini wa viwango vya kufa nchini India, Mama Theresa alikemea mtindo wa kusali, kusali, kusali!
Aliwaambia masista, walipokuwa wamerejea kutoka kusali, kwamba kamwe wasithubutu tena kuweka muda maalum wa kusali.
Alisema, kwa kila tendo jema wanalofanya – iwe kuosha vidonda vya masikini, vya waliopata ajali, kulisha walio taabani na hata kusikiliza matatizo ya wanyonge – wanakuwa wamesali. Kusali kwa njia ya vitendo. Kusali kwa njia ya utumishi. Kusali na kutukuza Mungu kwa njia ya kutumikia wengine na kujitumikia.
Leo, katika viunga vya jiji la Dar es Salaam, wasabato masalia wanajiua polepole – kwa kukaa na kuomba; kusubiri kisichopo; kutokuwa hata na kazi ndogo ya kujilisha, wao na familia zao; wanatenda jinai ya kujaribu kuondoa uhai wao kwa kisingizio cha kuomba Mungu na kusubiri maajabu.
Hakuna mwenye busara ambaye atapendekeza serikali itumie nguvu kukamata na kuondosha masalia. Wala hakuna mwenye busara atakayependekeza serikali iache masalia wafe kwa kisingizio cha “demokrasi na uhuru wa kuabudu.”
Kuwaacha wafe mmojammoja au hata kwa makundi, ni kukiri kushindwa wajibu wa kulinda watu/raia na mali zao – jukumu kuu la serikali. Na masalia hawajaisha kabisa. Bado wana uhai na walichonacho ndiyo mali iliyosalia.
Serikali inayojali yaweza kuokoa maisha ya Wasabato Masalia. Na itende.
0713 614872
ndimara@yahoo.com
(Makala hii itachapishwa katika Toleo la Tanzania Daima Jumapili la 22 Machi 2009 katika safu ya SITAKI)

No comments
Post a Comment