Header Ads

LightBlog

Uwongo wa Butiku, Kitine na Warioba

Na Ndimara Tegambwage


Uwongo wa Butiku, Kitine na Warioba


SITAKI kusikia vilio vya wasioambilika. Hapa Joseph Butiku. Kule Joseph Warioba. Huku Hassy Kitine. Sitaki!

Sasa imekuwa nongwa. Tumsikilize nani? Mara Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepoteza dira. Mara nchi inaendeshwa kienyeji. Mara CCM inatapatapa. Tumsikilize nani na nani hasa mkweli.

Wewe ni mwanachama wa chama kikongwe. Kilichokupa madaraka hadi ukayachoka au hadi kikakunyang’anya. Bado umo tu – CCM ndiyo baba, CCM ndiyo mama! Halafu unalalama kila kukicha: CCM mbaya! Hawana uongozi. Hawana dira.

Hivi nani hasa atakuamini? Unatafuta nini wewe mwenye dira mahali ambako hakuna dira? Nani kakushikia huko? Utamu upi usioweza kuutema?

Imetokea vipi ukawa na dira katikati ya wasio na dira? Au dira ipo na wewe umeanza kushindwa kuisoma. Au dira imepotea kweli na wewe unasema, “potelea mbali” tutakufa wengi huko anga za mbali au maji marefu. Hutaki kuachana na chombo ingawa una mwavuli; ingawa una chombo cha kuelea. Unataka kuponea humohumo au kufia humohumo.

Eh! Hata baada ya kujua kuwa chombo chako hakina dira; waongozaji wanatapatapa na chombo chenyewe kinaendeshwa kienyeji; bado hutoki? Hivi wewe ukoje? Ni kauli za dhati au za kufurahisha baraza?

Hivi ni kweli dira ya CCM imetoweka au wajanja wameipoteza, kwa hiyo haipo? Nani alikuwa ameishikilia mara ya mwisho? Ameiweka wapi? Yeye anasemaje? Amehojiwa? Au dira ipo lakini “wazee” hawa hawawezi tena kusoma; hawawezi tena kuelewa hata wakisoma?

Sikiliza. Kitine anasema hali iliyopo inahatarisha “usalama wa taifa.” Anasema nchi inaendeshwa kienyeji; uchumi na maliasili za taifa vimeshikwa na wageni wakati wazalendo wakifangia barabara na kufanya kazi za uboi.

Anajua hayo yanafanyika chini ya utawala wa CCM. Bado ni mwanachama wa CCM na bado hataki kutoka katika chama hicho. Anataka kulalama, kusikika na kurudi ukimyani. Basi. Huyu mkweli, mwongo?

Anayotaja Kitine yameanza kuwa hivyo tangu lini? Si yalikuwepo alipokuwa mkuu wa mashushushu nchini? Si yalishamiri wakati akiwa waziri, Ofisi ya rais, anayeshughulikia “Utawala bora?” Je, wakati huo hayakuonekana katika dira ya chama chake?

Butiku na Warioba wamekuwa wakilalamikia CCM na serikali kukosa mwelekeo katika mambo mbalimbali. Niliwahi kushikana mashati na Warioba katika safu hii hadi akanipigia simu na kuniuliza, “Wewe…ulikuwa umelewa wakati unaandika makala hii?” Tulicheka. Yaliisha.

Mara hii Butiku anatumia mkutano wa uchaguzi wa Chama cha Wananchi (CUF) kupeleka ujumbe kuwa chama chake “kinatapatapa” na kwamba hakina uongozi thabiti.

Joseph Butiku ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere. Alikuwa msaidizi maalum wa Mwalimu kwa zaidi ya miaka ishirini. Warioba alikuwa Waziri Mkuu, Waziri na sasa wakili; lakini mtu mwenye uzito wa aina yake katika jamii na kauli yake inasikika na kuheshimika.

Ukitaka kuwatendea haki Butiku, Kitine na Warioba, sharti kwanza ukubali kuwa ni watu, raia wa Tanzania , wenye haki ya kuwa na maoni juu ya mambo yanayowahusu wao na nchi yao . Wana haki ya kuona kama wanavyoona.

Pili, sharti ukubali kuwa wana haki ya kushawishi wengine kuona kama wenyewe wanavyoona. Hili hasa ndilo linafanya watoe kauli zao hadharani; bila woga wala kificho. Sasa tatizo liko wapi?

Tatizo liko katika kulalamika. Tuanze hivi: Kulalamika kunatokana na kutokubaliana jinsi mambo yanavyoendeshwa – utawala, miliki ya raslimali za taifa na mengine. Kunatokana na wao kutokuwa kwenye nafasi ya kuweza kuleta mabadiliko wanayoona ni muwafaka.

Kwa nyakati tofauti, hawa walikuwa kwenye nafasi za madaraka. Hawakulalamika. Labda hawakuona au waliona lakini wakazidiwa nguvu; au waliona ni mambo ya kawaida. Jana na leo ni tofauti; kila siku inayokuja na kupita, ni mwalimu na wakati huohuo ni maarifa.

Lakini siku zimepita nyingi. Walimu, tena walimu bora, wamekuwa wengi na maarifa yanapaswa kuwa yameongezeka. Bahati mbaya kwa Butiku, Warioba na Kitine, maarifa hayaongezeki na wingi wa walimu bora si hoja.

Inafikia wakati unalazimika kufikiri kuwa watu hawa ni waongo; tena waongo sana . Kuna tatizo; wanasema linawauma na kuwasumbua. Linawakera. Wanaelewa kiini chake. Lakini mbona hawachukii, na badala yake wanabakia kulalamika tu?

Siyo hoja mpya, kwamba ukichukia unachukua hatua. Hakika hatua haiwezi kuwa malalamiko katika vyombo vya habari au mikutanoni. Kuchukia siyo kuendelea kujiviringisha kwenye tope; kulialia huku ukiendelea kujizamisha miongoni mwa unaolalamikia.

Katika mazingira ya sasa nchini, kuchukia siyo tena kuendelea kuimba wimbo uleule wa kusubiri Mwenyezi Mungu alete fikra mpya na kupitia kwa kiongozi mkuu wa chama au serikali. Hapana!

Ni ukweli usiopingika kuwa Warioba, Butiku na Kitine wamepoteza muda mwingi kupiga porojo badala ya kuwaelekeza Watanzania nini kifanyike ili kuondoa kile ambacho wanaona hakifai.

Naye aliyeko madarakani, chukua mfano wa Rais Jakaya Kikwete, ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, wala hana papara. Amewapa kamba ndefu ili kila mmoja ajinyonge kwa wakati wake.

Ijumaa wiki hii aliwaambia waliostaafu uongozi wakae kimya kama Mzee Rashid Mfaume Kawawa na siyo kuwa “kilomolomo” wakati wao walishindwa yao walipokuwa kwenye uongozi. Amewachoka!

Kama Butiku, Kitine na Warioba wamesikia hayo na wangekuwa makini, wasingebakia CCM na kulalama kila kukicha. Kwa mfano, jinsi Butiku na Kitine walivyoongelea utawala na CCM, hawana sababu ya kubaki kwenye chama hicho “hatari.”

Wana kila sababu, pamoja na Warioba na wengine, kuhama chama hatari wanachosema kinatapatapa, kinauza nchi, kinaongoza kwa njia ya ubabaishaji; na kuanzisha chama kipya au kujiunga na kilichopo kwa ajili ya kuleta mabadiliko wanayotaka.

Kutofanya hivyo na badala yake kubakia kulalama, ni kupoteza muda na fursa mwanana ya kufanya jambo la maana katika maisha yao na maisha ya taifa lao. Ukichukia sharti uchukue hatua na hatua sahihi ni kuhama na kuelekeza umma wapi pa kuweka nguvu ili kukamilisha matumaini yao .

Hadi hapa, ningeombwa kutaja mafanikio ya CCM, nisingeacha kutaja “uwezo” wake wa kufyonza nguvu za mwili, roho na akili za viongozi na wanachama wake wengi, kiasi kwamba hata wanapokuwa hawakubaliani nacho, hubaki makasha yasiyoweza kufanya maasi.

Hiyo nayo ni sababu tosha ya kukataa mikatale ya CCM. Warioba, Butiku na Kitine, mpooo? Kuendelea kulalamikia CCM na utawala wake, na wakati huohuo kubaki kwapani mwake, ni kudhihirisha udhaifu, uwongo na unafiki.


(Makala hii ilichapishwa katika safu ya SITAKI katika toleo la
Tanzania Daima Jumapili la 1 Machi 2009)

0713 614872
ndimara@yahoo.com

No comments

Powered by Blogger.